2018-04-03 10:11:00

Umoja wa Mataifa: Athari za mabadiliko ya tabianchi ni tishio kubwa!


Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya ongezeko la joto duniani linalohatarisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, ni kati ya changamoto kubwa zinazovaliwa njuga kwa sasa na Umoja wa Mataifa. Athari za mabadiliko ya tabianchi zinatishia sana maisha ya watu wengi duniani, kumbe, Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kuhakikisha kwamba, inashikamana kwa dhati ili kudhiti athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kutekeleza kwa vitendo makubaliano ya Mkutano wa 21 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mkataba wa Mabadiliko ya Tabianchi uliofanyika mjini Paris, nchini Ufaransa, kuanzia tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2015. Jumuiya ya Kimataifa ilipitisha mkataba mpya wa Paris ambao umeweka historia mpya kwa nchi 195 kukubali kushirikiana katika kushughulikia athari na changamoto za mabadiliko ya tabianchi kwa kupitisha mkataba mpya wa kisheria utakaozijumuisha nchi zote katika kupunguza gesi joto.

Haya yamesema hivi karibuni na Bwana Antònio Guterres, Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ambaye anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kushirikiana na kushikamana kwa dhati, ili kufanikisha upatikanaji wa kiasi cha dola za kimarekani bilioni mia moja kwa mwaka, kama ilivyokubaliwa. Ingawa gharama za kuzijengea uwezo Nchi zinazoendelea duniani ili kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi ni kubwa zaidi, ikilinganisha na kiwango kilichoahidiwa na Jumuiya ya Kimataifa wakati wa Mkutano wa Paris.

Wanasayansi wanaitaka Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi kwani bila kufanya hivi anasema Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, watu wengi wataathirika kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa. Mkutano huu umekuwa ni wa maana sana kwani ulitiwa mkwaju na nchi 195, kwa mara ya kwanza katika historia ya Jumuiya ya Kimataifa. Wanasayansi waliokuwa wanashiriki katika Mkutano wa Kimataifa kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi huko Brasilia, nchini Brazil, hivi karibuni, wameonya kwamba, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitajifunga kibwebwe kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi, zaidi ya watu bilioni tano wataathirika vibaya sana kwa kukosa maji safi na salama ifikapo mwaka 2050. Madhara yake ni makubwa hata katika masuala msingi ya kijamii, kiuchumi na kisiasa!

MADHUMUNI YA MKUTANO WA PARIS, 2015: Ilikuwa ni kujadiliana, kukubaliana kuhusu Mkataba mpya wa Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi utakaohusisha nchi zote katika kupunguza gesi joto. Masuala muhimu yaliyojadiliwa na ambayo yatakuwa sehemu ya Mkataba mpya ni:- Misingi muhimu katika kutekeleza mkataba mpya; kupunguza gesijoto; kuhimili mabadiliko ya tabianchi; Upatikanaji wa fedha; Uendelezaji na upelekaji teknolojia za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi; na kujenga uwezo wa nchi zinazoendelea kupambana fika na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayowatumbukiza wananchi wengi katika umaskini na majanga ya maisha !

MAKUBALIANO YA MKUTANO : Kwa ujumla nchi zilikubaliana kwa kauli moja kuwa na mkataba mpya utakaoshirikisha nchi zote katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, ikiwa ni pamoja na nchi zote kushiriki katika kupunguza gesi joto kupitia juhudi za Kitaifa zinazobainisha viwango ambavyo kila nchi itachangia katika upunguzaji wa gesijoto (Intended Nationally Determined Contributions-INDCs). Makubaliano haya yanatoa taswira, mwelekeo, na malengo ambayo nchi zote duniani zitashiriki katika kupunguza gesi joto ili kufikia lengo la dunia la kutokuongezeka kwa wastani wa joto la dunia kwa zaidi ya nyuzi 20C au 1.50C. Hatua hii ni muhimu katika kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi ambazo zimeendelea kuathiri nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania hasa katika sekta muhimu zinazochangia uchumi wa nchi kama vile kilimo, mifugo, uvuvi, utalii nk.

Baadhi ya makubaliano muhimu yaliyofikiwa ni katika maeneo yafuatayo:- Misingi muhimu katika kutekeleza mkataba mpya : Nchi Wanachama zimekubaliana kuwa utekelezaji wa mkataba wa Paris utazingatia misingi ya usawa na majukumu ya pamoja kwa kuzingatia historia ya chanzo cha mabadiliko ya tabianchi na uwezo wa kukabiliana na tatizo hilo (“the principal of equity and principal of common but differentiated responsibilities and respective capabilities, in light of national circumstances – CBDR-NC”).

Upunguzaji wa gesijoto : Nchi zimekubaliana kwamba juhudi za kupunguza uzalishaji wa gesijoto ni lazima zilenge kupunguza wastani wa ongezeko la joto la dunia chini ya nyuzi joto 20C au 1.50C ili kuepuka athari za mabadiliko ya tabianchi, kwa kuzingatia na kutekeleza juhudi za Kitaifa kuhusu kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi (INDCs).

Kuhimili mabadiliko ya tabianchi: Nchi zimekubaliana kuwa na dira ya pamoja ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi itakayohakikisha nchi zinaongeza uwezo wa kuhimili mabadiliko ya tabianchi. Upatikanaji wa fedha: Nchi zilizoendelea zitaendelea kuwa na jukumu la kutoa fedha za kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea. Teknolojia na kujengewa uwezo: Teknolojia za kushughulikia masuala ya mabadiliko ya tabianchi zitatolewa kwa nchi zinazoendelea. Aidha, kumeundwa Kamati maalum ya kujenga uwezo wa kushughulikia mabadiliko ya tabianchi kwa nchi zinazoendelea.

Baadhi ya mambo ambayo Mkutano wa 21 haukufikia makubaliano katika Mkutano wa Paris: Kuondoa vikwazo katika upatikanaji wa teknolojia hususan hati miliki (intellectual property right-IPR). Nchi zilizoendelea zilitaka nchi zinazoendelea zinunue teknolojia hiyo toka kwa makampuni binafsi ambayo huuza kwa bei ghali badala ya kuzitoa bure au kwa bei nafuu. Nchi zilizoendelea zinapinga jambo hili. Utoaji wa fedha kwa ajili ya kushughulikia mabadiliko ya tabianchi: Nchi zinazoendelea zilitaka nchi zilizoendelea ziwekewe viwango vya kutoa fedha za kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi katika kipindi cha kuanzia sasa hadi 2020 ili upatikanaji wake uwe endelevu. Hata hivyo, nchi zilizoendelea ziliahidi kuendelea kutoa fedha kwa hiari katika kipindi hicho kwa kuzingatia hali zao kiuchumi.

Changamoto Zilizojitokeza: Nchi zilizoendelea kutokuwa tayari kupitisha maamuzi yanayolenga kuzibana zitoe fedha za kutosha na uhakika katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kulingana na Mkataba wa awali. Hii inafanya mifuko ya fedha chini ya mkataba kukosa fedha za kutosha kugharamia miradi ya nchi zinazoendelea ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Nchi zilizoendelea kuweka uzito mdogo katika masuala ya kuhimili mabadiliko ya tabianchi ambayo ndio hitaji kubwa la nchi zinazoendelea kutokana na kuwa katika hatari kubwa ya kuathirika na mabadiliko ya tabianchi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.