2018-03-31 12:02:00

Askofu mkuu Ruwaichi: Ujumbe wa Pasaka na Miaka 150 ya Ukatoliki


Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji Tanzania Bara na kilele chake ni hapo tarehe 7 Oktoba 2018 huko Bagamoyo, Mlango wa imani kwa familia ya Mungu Afrika ya Mashariki. Katika kipindi cha Kwaresima, familia ya Mungu nchini Tanzania imekuwa ikitafakari kwa kina na mapana juu ya swali msingi “Je, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Mw.4:9.  Je, waamini wa Kanisa Katoliki katika kipindi cha miaka 150 wamethubutu kuwa ni walizni wa binadamu wenzao ambao wamefanywa kuwa ndugu kama Familia ya Mungu kupitia kwa Kristo Yesu na Bikira Maria, Mama wa Kanisa?

Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi wa Jimbo kuu la Mwanza, Tanzania akatika mahojiano maalum na “Vatican News” anasema, Pasaka ya Mwaka 2018 nchini Tanzania ni fursa nyingine tena ya kuadhimisha tunu na zawadi ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni ukombozi ambao umepatikana kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Tanzania inaadhimisha Pasaka hii kwa mwaka 150. Hii ni fursa ya kufurahia ushindi wa Kristo na waamini wote sehemu mbali mbali za dunia. Lakini, Fumbo hili la Pasaka kwa mwaka huu linaadhimishwa katika ardhi na mazingira ya Kanisa Tanzania kwa namna ya pekee kabisa! 

Askofu mkuu Ruwaichi anamwomba Mwenyezi Mungu awapatie Wakristo wote nchini Tanzania nguvu, uthubutu na furaha ya kumshangilia Kristo Mfufuka bila woga, kigugumizi na wala bila ubaridi wowote ule! Wakristo washangilie ushindi wa Kristo na kuwashirikisha watu wote wa Mungu furaha hii ya ufufuko wa Kristo. Anakaza kusema, Kristo ni Bwana na Mkombozi wa watu wote. Huu ndio ukweli unaofumbatwa katika Fumbo la Pasaka. Askofu mkuu Ruwaichi anatumia fursa hii kuwatakia watanzania wote heri na baraka ya Fumbo la Pasaka, yaani ya Kristo Mfufuka!

Na Padre Richard. A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.