2018-03-30 15:55:00

Ijumaa Kuu: Mashitaka ya Yuda Iskarioti, Petro na Hukumu ya Yesu!


Mateso na kifo cha Yesu Msalabani ni Fumbo kuu la Imani. Mbele ya mateso na kifo, hata mitume na wanafunzi wake walirudi nyuma, wakachanganyikiwa na kujifungia ndani ya chumba. Petro aliamua kusema uwongo ili tu kuepa ushahidi, mwanaume mzima akaishia kulia machozi! Yuda akajinyonga. Wanafunzi wawili wakaamua kulihama Jiji la Yerusalemu kukimbilia kijijini Emaus. Ndugu zangu katika mateso na hatari ya kifo yaani mbele ya matatizo mazito ya maisha, ndipo unapoweza kumjua mwenye imani ya kweli kwa Mungu. Juu ya mateso na Fumbo la Msalaba, Mtakatifu Ambrosi wa Milano anasema: “Kama hutaki kuchanganyikiwa na maisha, basi jaribu kuingia kwa undani na kuelewa maana ya Msalaba wa Kristo; Kama unataka kuponywa majeraha yako basi elewa maana ya majeraha ya Kristo; Kama unataka kuupata uzima wa milele, elewa maana ya mateso na kifo cha Yesu; Kama unataka kufufuka, elewa maana ya maziko yake.”

Yesu Kristo hakuchanganyikiwa kabisa wakati wa mateso na kifo chake, bali alijiamini na kumtumainia Baba yake. Baada tu ya kukamatwa kwake, Makuhani wakamfungulia jalada la mashtaka. Mashtaka hao yalipelekwa mbele ya Pilato aliyewakilisha dola na Serikali ya Kirumi. Makuhani walimtuhumu Yesu kwa suala la kidini, kwamba, anajifanya kuwa Mwana wa Mungu. Kwa Wayahudi wanaomwabudu Mungu mmoja [YAHWE], madai ya Yesu yalikuwa ni kufuru na kosa la jinai. Kosa hilo linaendelea kuwa la jinai hadi leo kwa Wayahudi na kwa wasiokuwa wakristo. Haieleweki kwao kusikia Mungu anaweza kuzaliwa na kuwa binadamu kama sisi.

Ili kung’oa mzizi wa fitina na kuwatolea uvivu Wayahudi wakati wa hukumu ya Yesu, Pilato akawakebehi bila kujua kwamba anauthibitisha ukweli wa Fumbo la Umwilisho na la Mateso ya Yesu akaandikia hati ya mashtaka na kubandika Msalabani: “Yesu Mnazareti, Mfalme wa Wayahudi.” Pilato hakuchanganyikiwa. Walipomtaka abadili kauli, akashikilia msimamo na kusema: “Nilichokiandika nimekiandika.” Wayahudi ndiyo waliokuwa wamechanganyikiwa na kujipinga waliposema: “Sisi hatuna mfame isipokuwa Kaisari.” Wasikumbuke kabla walisema kuwa hawamtambui Kaisari kama mfalme isipokuwa YAHWE.

Fumbo la Msalaba katika mahakama ya Yesu hadi hukumu ya mwisho ni fundisho kwa viongozi wa serikali na mahakimu jinsi ya kuendesha, kesi, mashtaka na kutoa kuhukumu ya haki na upendo. Kwa watu wa dini, wajifunze kuchuja thamani iliyojificha katika mazingira mabovu yaani uwezo wa kugundua “dhahabu na madini mengine” katika makinikia ya maisha. Mchakato wa kesi na hukumu ya Yesu unaunganisha pia malumbano yaliyowakumba mitume. Tujaribu kutengeneza kesi na hukumu ya mitume wawili, Yuda na Petro kisha tulinganishe na thamani ya hukumu anayoichuja Yesu dhidi ya mitume hawa wawili.

Kesi ya Yuda Iskariote: CV (Curriculum vitae) Sifa za mtuhumiwa: Yuda Iskariote ni mzaliwa na mkazi mkoani Galilea. Baba yake aliitwa Simoni. Iskariote ni muunganiko wa maneno mawili ya lugha ya kiebrania -Ish maana yake mtu na Kariot ni mtumishi, au mjuaji na mtaalamu. Kwa hiyo Yuda alikuwa “kijumvi”, mjuaji, mtaalamu, mwenye mawazo ya kiulimwengu, mwanamapinduzi anayetaka demokrasia, yaani uhuru. Kazi yake yawezekana alikuwa mjasiriamali wa kujitegemea na aliyependa sana kujikomboa kutoka utawala wa warumi. Aliitwa na Yesu ili amfuate, na alikabidhiwa kuwa mtunza “mkoba” yaani hazina wa kikundi cha Yesu yaani mitume. Yuda anatuhumiwa kuwa msaliti wa Yesu. Kutokana na tuhuma hizo, Yuda anashikiliwa katika mahakama ya wakristo kwa kupanga mipango ya siri ya kumwuza Yesu na hivi kusababisha kifo cha Yesu bila kukusudia.

Uchunguzi na Upelelezi wa mahakama: Kwanza kabisa mahakama imebaini kwamba, Yuda alikuwa katika nafasi kubwa sana ya kumfahamu Kristo hata pengine kumpita Petro. Aidha Yuda alipata nafasi nzuri kama ya mitume wengine ya kusikia mafundisho ya Yesu na kuona mfano wa maisha yake. Tunaweza kusema Yuda alipendwa na Yesu. Lakini yaonekana alitumia vibaya urafiki huo kiasi cha kushindwa kumrudishia Yesu pendo hilo. Katika nafasi moja Yuda alihitilifiana na Yesu kikazi. Pale Yuda alipomwangalisha Yesu kitendo cha kumwacha Maria kumpaka Yesu mafuta ya thamani badala ya kuyauza na pesa kuwasaidia maskini. Yesu akamkaripia na kumtetea Maria amwache afanye tendo la kiroho, kwani “maskini mnao muda wote.”

Kumbe Yuda alikuwa anadokoa hata michango ya wanakikundi (kutoka hazina ya chama) aliyokuwa ameaminishwa kubeba. Yuda alijiaminia sana utaalamu wake alifikiri kwamba Yesu ana njia zake tu za kufanya mapinduzi, na kuwaletea watu uhuru wa kisiasa wa kuwaondoa wakoloni. Hivi alifikiri akimsaliti Yesu, kadiri anavyomfahamu atajitetea tu na kushinda kesi. Aidha, Yuda alihamasishwa zaidi alipomwona Yesu jinsi alivyouteka umati wa watu siku ya Matawi na kuandamana nao kwa amani hadi ikulu. Yuda aliyafasiri kisiasa na kiulimwengu matendo hayo ya Yesu kwa Njia ya Msalaba, hali iliyojenga sintofahamu kubwa na uhuru aliokuwa anapigania Yesu. Mapato yake Yuda akachanganyikiwa, akakata tamaa na kujinyonga.

Hukumu inayoweza kutolewa: Jopo la mahakimu limebaini kwamba uhaini wa Yuda unaweza kutolewa maelezo ya kumwachilia huru. Labda itabidi aonywe tu kuondokana na tabia ya udokozi wa mali ya kikundi, yaani mitume. Ukweli ni kwamba mahakama inakiri kuwa Yuda alikuwa na akili timamu, mwenye bidii ya kazi hasa ya kuangalia rasilimali na ya kutunisha mfuko wa chama. Ni dhahiri pia kuwa Yuda alikuwa mzalendo na mkereketwa aliyeitetea nchi yake dhidi ya ukoloni wa Warumi waliokuwa wanakandamiza demokrasia. Akatumia kila mbinu ili kumwingiza Yesu katika mapambano ya kulikomboa Taifa dhidi ya Warumi hao. Kwa hiyo, hakuna sababu ya kumlaumu Yuda. Lakini kwa kuwa na fikra hizi za uzalendo Yuda amekosea, basi asilaumiwe peke yake bali alaumiwe pia shetani, Ibilisi kwani mwinjili Yohane ameandika kwamba “Baada ya kupata tonge, shetani akamwingia Yuda: (Yoh. 13:27). Yaani Yuda aliingiwa na nguvu za giza zilizofunika akili yake. Tena inasemwa waziwazi: “Akachukua tonge, na kutoka mara moja na ilikuwa giza.” (Yoh. 13:30). Yaani akili iliingiwa na nguvu za giza. Ama kweli giza lilienea mwili mzima. Giza lililosababishwa na tonge (chakula) na makuhani walimwezesha na donge jingine la vipande thelathini vya pesa. Hapo Yuda akapagawa na kuchanganyikiwa zaidi.

Aidha, ni dhahiri kabisa kwamba Yuda hakutaka kabisa Yesu afe ndiyo maana alirudisha ule “mshiko” kwa makuhani wakuu na kujuta kabisa aliposema: “Nimetenda dhambi, nimetoa damu ya mtu asiye na kosa” (Mt 27:4). Lakini haikusaidia “Majuto ni mjukuu.” Kwani makuhani wakamfukuza kama vile wangesema: “kilichoenda kwa mganga hakirudi.” Ili kuonesha kama Yuda kweli alijutia sana alichokifanya, basi akazitupa zile pesa Hekaluni na kwenda kujitundika. Kwa bahati mbaya majuto hayakumwongoa bali yalimpelekea kukata tamaa. Alama wazi ya kukata tamaa ni kujichukulia kesi mkononi, akajinyonga. Kwa hiyo kesi ya mtindo huu wa Yuda na hukumu yake tunaiachia mahakama kuu ya mbinguni, na tunamkabidhi Yuda mikononi mwa Yesu. Ndiye aliyemjua sana hadi akamchagua kuwa Mtume wake na kumkabidhi kutunza mfuko wa hazina. Huwezi kujua katika katika kukata tamaa, na kujuta kulishamkutanisha na Bwana Yesu aliye hakimu mwenye, haki na huruma, na akakumbatiwa naye kwa upendo.

Ndugu zangu Yuda anaweza kuwa kioo cha kujitazama hasa kwa wanasiasa na watu wa serikali, lakini zaidi kioo cha viongozi wa dini. Kadhalika kioo cha sisi sote kwani tunaweza tukafanya alivyofanya yeye.  Yabidi kumtafakari Mungu anataka nini. Kwa wakristo wajihoji daima Yesu anataka nini katika mazingira halisi ya maisha na kutokuchanganyikiwa na chakula na mali. Yuda ni mtu anayetumia akili na uhuru binafsi kama anavyotaka yeye na kujichukulia maamuzi mikononi mwake. Mara nyingi watu wanaojiamini mno na kutafuta “kiki” ili kuonekana wa pekee na kuushangaza ulimwengu wanaishia kujishangaza wenyewe na kukata tamaa na mwisho wanajimaliza wenyewe katika siasa, serikali, dini na katika maisha ya kawaida. Tunamwomba Yesu aaminie bado urafiki wetu, asituone sote kuwa wanafiki na asishange kuona wengine wanakosa uaminifu, hata kama wanaitwa wakristo. Ee Bwana Yesu unitoe kutoka kundi la akina Yuda lisilotaka kubadili misimamo yao ya maisha na kukufuata wewe.

Kesi ya Petro: Wakristo wote mnaalikwa kwenye jopo la mahakimu wa mahakama ya Kanisa ili kumtathmini Petro kama kweli alistahili kupewa hadhi ya kuliongoza Kanisa Moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Tujipange vizuri kesi yake Petro na tumtolee hukumu anayostahili. CV (Curriculum vitae). Sifa ya mtuhumiwa: Petro ni mzawa na mkazi wa Kafarnaumu. Kazi yake ni uvuvi; Ni Baba wa familia mwenye watoto; Aliitwa na Yesu kufanya kazi ya kuvua watu yaani mchungaji; Katika mang’amuzi yake ya kwanza ya uchungaji kwenye mwezi Oktoba wa mwaka 27 alikamatwa na kutiwa nguvuni kutokana na vurugu alizozisababisha usiku kabla ya Pasaka ya mwaka 30 ikiwa ni pamoja na kosa la jinai la kumkata sikio mtumishi wa serikali kwa jambia, silaha ya kijambazi na ya kivita.

Uchunguzi na Upelelezi wa mahakama: Petro ni mmoja wa watu wenye ushuhuda mkubwa juu ya Yesu hadi akaja kuitwa na kutazamwa naye kwa jicho la pekee. Mara ya kwanza aliitwa katika nafasi ya uvuvi ule mkubwa, ndio uliompa jina na kuaminiwa sana. Ndiyo maana Petro alikuwa wa kwanza kuitwa na kukabidhiwa mamlaka sawa kama ya Yesu mwenyewe. Akapata fursa ya kuangaliwa kwa jicho la pekee na Yesu, hata akateuliwa na kupata majukumu makubwa katika ahadi aliyoitoa kule Kaisaria Filipo.  Petro alipewa maagizo ya pekee kutoka kwa Yesu juu ya vipengele mbalimbali vya kazi na alipata pia fursa mbalimbali za kufaidi urafiki binafsi na Yesu.

Lakini Petro, aliyeangaliwa kwa namna ya pekee na Yesu, alilewa sifa na kujiangusha mwenyewe kiasi cha mmoja kushawishiwa kutengua uteuzi aliopewa, yaani “kutumbuliwa”. Hoja ni kwamba, katika nafasi moja alidakiza kauli ya Yesu na kumshauri vibaya hadi ikamlazimu Yesu kumwambia: “Rudi nyuma Shetani.” Aidha kutokana na upelelezi wa kina uliofanyika, imebainika pia kwamba katika mazingira nyeti na ya kushtusha Petro alichanganyikiwa kwa woga kiasi cha kumkana Yesu mbele ya watu. Aidha Petro anapoulizwa maswali na mjakazi, anaruka na kukataa kabisa kwamba hamjui Yesu.

Upelelezi umebaini zaidi kwamba licha ya kumkana Yesu, ametenda kosa la jinai lililosababisha kifo cha Yesu hasa vituko alivyovifanya bustanini Getsemani. Tunajua kwamba mwanaume wa Kiyahudi alikuwa anatembea na jambia kibindoni ili kujitetea wakati wa hatari. Lakini haikutegemewa kabisa kumwona mtu wa hadhi ya Petro kuchomoa jambia na kuanza mapambano. Mbaya zaidi hakuchomoa tu jambia kwa ajili ya kutishia, alikosea hata namna ya kujitetea kiasi cha kumkata sikio mtumishi wa Kuhani. Kitendo kilichotoa picha mbaya kwa kundi zima la Yesu, kwa kufikiriwa kuwa ni chama fulani cha vibaka au kundi la “watu wasiojulikana” au watu wenye msimamo mkali wa kidini. Hata ikamlazimu Yesu kuomba msamaha na kumtaka Petro kurudisha jambia alani.

Utafiti umeendelea na kuthibitisha kuwa wakati wa kumkamata Yesu, badala ya yeye kumfuata Mwalimu wake, badala yake anamkana kwa viapo. Tungetegemea walau kuwakusanya wenzake kumi kupata ushahidi mzuri na kuiwakilisha kesi mahakamani ili walau kuweza kushusha watu vyeo vyao kutokana na kuendesha vibaya kesi ya Yesu. Ukweli ni kwamba hadi kufikia hatua hii, Petro alijishushia hadhi na imani kutoka kwa Yesu. Kutokana na vipengele hivi vyote vya mashtaka vilivyosomwa, ni dhahiri kwamba Petro ana hatia na anatiwa nguvuni.

Hukumu tunayoweza kuitoa: Mahakama imejiridhisha na ushahidi uliotolewa na kutoa hukumu ya haki. Kwa hiyo, mshtakiwa ananyang’anywa cheo, pamoja na haki na malupulupu yatokanayo, yaani “anatumbuliwa”. Hawezi tena kuagizwa wala kuaminishwa madaraka makubwa. Lakini kwa sababu ni mzee wa umri na anayo familia kubwa inayomtegemea, ana mke na watoto na anakaa na mkwe wake aliyeponywa na Yesu homa kali, basi anaweza kupata kazi ya ngazi ya chini sana ili kupata pesa ya kujikimu, lakini itabidi akaguliwe mara kwa mara na kama anaonesha tabia ya kujirekebisha. Aidha itakuwa ni kukosa busara endapo mtu wa aina hii ataaminishwa tena ofisi au kazi muhimu ya uongozi. Tunajiaminisha kwamba mahakama ya Kanisa imetoa hukumu iliyo sahihi. Kwa vyovyote tamko la mwisho tunamwachia Yesu.

Yesu anabatilisha hukumu: Yesu anamfahamu sana Petro, na ameyashuhudia mambo yote aliyotenda Petro, lakini anatengua uamuzi wa mahakama ya kanisa, na anafanya mambo kinyume cha tunachofikiria sisi. Anachofanya Yesu ni kumwamini na kumrudishia imani yake. Yesu nawapenda wanyenyekevu wa moyo. Petro anajiamini sana katika kutenda jambo lakini akikosea anajuta na kumnyenyekea. Petro ni kioo kwetu cha unyenyekevu. Aidha, mahakama ya Yesu ina sheria iliyojikita katika: Haki, Huruma na Upendo. Petro alipata fursa ya kuhojiwa na Yesu mara tatu swali moja tu linalohusu upendo. Petro alifanikiwa kujibu maswali mawili tu na swali la tatu akapata kigugumizi. ‘Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda.’ Yesu akridhika na akamrudishia Petro cheo chake na kupewa majukumu: ‘Lisha wanakondoo wangu.’‘Chunga kondoo zangu.’ ‘Lisha kondoo zangu.’

Yesu amempyaisha Petro hadi ameweza kujibu swali la upendo. Upendo ndiyo thamani kuu iliyo ndani ya kila mmoja wetu, yaani: Huruma na Upendo wa Mungu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Ee Bwana ninajiunga nafsi yangu na ile ya Petro na kusali pamoja naye: “Bwana mimi sistahili kuaminiwa tena. Wewe unirudishie kuaminiwa (imani) nawe nilikokupoteza. Unipyaishe na kuniongoza kwenye: uhuru na utu wa kweli ili niweze kukujibu kwa hiari yangu kutoka ndani kwamba ninakupenda wewe kwa dhati.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.
All the contents on this site are copyrighted ©.