2018-03-29 14:15:00

Askofu Ngalalekumtwa asema, wito wa kipadre unahitaji walezi makini!


Vijana waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana hivi karibuni, wamedadavua changamoto na fursa katika maisha ya vijana wa kizazi kipya; imani na wito, mang’amuzi pamoja na wajibu wa Kanisa kuwasindikiza vijana katika maisha yao. Wamekazia malezi, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya utume wake kwa vijana. kwa hakika, vijana wanatamani kuona Kanisa likitekeleza dhamana na utume wake katika misingi ya ukweli na uwazi; upole na unyenyekevu, kiasi hata cha kuthubutu kukiri makosa na mapungufu ya watoto wa Kanisa, pale yanapojitokeza. Vijana wanatamani kuwa na mashuhuda watakaowasindikiza katika maisha na miito yao, watakaowasaidia kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha vijana kwamba, wazee wana ndoto, lakini vijana wana maono!

Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika mahojiano maalum na “Vatican News” anafafanua kuhusu umuhimu wa Mapadre katika maisha na utume wa Mama Kanisa kwani hawa ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa. Ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika huduma makini hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Anapenda kumshukuru Mungu mwingi wa huruma na mapendo, ambaye amezijalia seminari na nyumba nyingi za malezi na miito ya kipadre kuwa na vijana wanaotamani kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Anasikitika kusema kwamba, hata katika neema hii, bado nchini Tanzania kuna majimbo ambayo yana ukame wa miito ya kipadre!

Ni matumaini na hamu kuu ya moyo wa Askofu Ngalalekumtwa kuona kwamba, Seminari na nyumba za malezi ya kipadre na kitawa zinapata walezi makini, wenye moyo wa kujituma na kujisadaka bila ya kujibakiza kama mfano hai wa Kristo Kuhani Mkuu, ili hatimaye, waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda makini wa kazi ya malezi na majiundo ya mapadre ili kweli Mwenyezi Mungu aweze kusifiwa, kuabudiwa, kutukuzwa na kuheshimiwa na binadamu aweze kutakatifuzwa, kupata wokovu na maisha ya uzima wa milele. Ili kufikia lengo hili, anasema Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, walezi wanapaswa kuwa kweli ni wachungaji wema, watakatifu, waadilifu na wanyofu kwa mfano wa Kristo Yesu anajitambulishwa kuwa ni “Mlango wa Uzima” na “Mchungaji Mwema” ambaye anautoa uhai wake kwa ajili ya kondoo wake. Analiombea Kanisa liweze kupata walezi watakatifu na Seminari kupata mahitaji yake msingi ili kuwezesha mchakato mzima wa malezi na majiundo kutekelezwa kadiri ya sera na mikakati inayobainishwa na Mama Kanisa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.