2018-03-27 09:49:00

Hati ya Utangulizi wa Sinodi: Vijana wafurahishwa na Kanisa!


Wajumbe wa vijana waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayoadhimishwa mjini Vatican mwezi Oktoba 2018 wametoa “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” itakayowasilishwa kwa Mababa wa Sinodi kama sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi”. Huu ni muhtasari wa maisha na matamanio yao halali kwa Mama Kanisa na Jamii katika ujumla wake.Vijana wa karne ya ishirini na moja, wanakabiliana na changamoto na fursa ambazo ziko ndani na nje yao wenyewe, na kadiri ya mazingira wanamotoka. Mama Kanisa anapaswa kuangalia jinsi ambavyo atasaidia kuwaongoza, kuwainua na kuwaimarisha vijana katika maisha yao.

Ni hati ambayo inashuhudia hali halisi, watu, imani na mang’amuzi ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia na wala si mafundisho mapya ya kitaalimungu. Itakuwa ni “Instrumentum Laboris” yaani “Hati ya kutendea Kazi” kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Vyanzo vingine ni muhtasari kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na Sinodi za Makanisa ya Mashariki. Haya ni matunda ya utamaduni na sanaa ya Kanisa kutaka kuwasikiliza vijana kwa umakini mkubwa! Sekretarieti kuu imekusanya na kuhariri majibu ya maswali dodoso yaliyotumwa na vijana kwa njia ya mitandao ya kijamii pamoja na mchango uliotolewa na washiriki wa Semina ya Vijana Kimataifa, iliyoandaliwa na Sekretarieti kuu ya Sinodi kunako mwaka 2017.

Umati mkubwa wa vijana umeshiriki kwa njia ya mitandao ya kijamii na hivyo itakuwa ni sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi” kwa Maaskofu. Ni matumaini ya vijana kwamba, Kanisa pamoja na taasisi mbali mbali zitaweza kujifunza kuwasikiliza vijana. Haya yamebainishwa hivi karibuni na Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu “Hati ya Utangulizi wa Sinodi.”  Anasema, wawakilishi wa vijana wakati wa uzinduzi wa utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, walipata bahati ya kukaa, kuzungumza na kusikilizwa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye amewataka vijana kuwa wadau wakuu wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Watambue kwamba, wao ni matumaini ya Kanisa linalopaswa kupyaishwa kwa: uwepo, karama na mapaji ya vijana katika maisha na utume wake!

Wawakilishi wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia anasema, Kardinali Baldisseri kwa muda wa juma zima wameishi, wamesali, kutafakari na kufurahia maisha kwa pamoja kama ndugu, licha ya tofauti zao msingi za kidini, kitamaduni na mahali wanakotoka. Vijana wameonesha vipaji vyao kwa kuchangia mawazo na duku duku zao; wasikivu na wavumilivu kwa mawazo yaliyokuwa yanatolewa na vijana wengine na hatimaye, wakakubaliana mambo msingi yanayopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na hayo ndiyo yaliyoandikwa kwenye “Hati ya Utangulizi wa Sinodi”. Vijana wamejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya vijana wenzao kiasi hata cha kudiriki kufanya kazi hata nyakati za usiku, ili kufikia malengo waliyojiwekea! Kimsingi vijana wamedadavua changamoto na fursa katika maisha ya vijana wa kizazi kipya; imani na wito, mang’amuzi pamoja na wajibu wa Kanisa kuwasindikiza vijana katika maisha yao. Wamekazia malezi, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Mama Kanisa kama sehemu ya utume wake kwa vijana.

Vijana wanatamani kuona Kanisa likitekeleza dhamana na utume wake katika misingi ya ukweli na uwazi; upole na unyenyekevu, kiasi hata cha kuthubutu kukiri makosa na mapungufu ya watoto wa Kanisa pale yanapojitokeza. Vijana wanatamani kuwa na mashuhuda watakaowasindikiza katika maisha na miito yao, watakaowasaidia kupambana na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Baba Mtakatifu Francisko amewakumbusha vijana kwamba, wazee wana ndoto, lakini vijana wana maono! Vijana wanataka kuona Kanisa linalojikita katika majadiliano katika ukweli na uwazi; ukarimu, mchakato wa upyaisho, utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini. Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anahitimisha mazungumzo yake kwa kusema, vijana wameonesha ari na moyo mkuu, upendo na imani kwa Kanisa kwa sababu wanahamasishwa kuwa kweli ni wadau wa mchakato wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana.

Sr. Nathalie Becquart amelipongeza Kanisa kwa kutoa nafasi kwa vijana kuweza kudadavua changamoto, fursa na mambo msingi katika safari ya maisha yao, lakini kikubwa zaidi ni pale ambapo Kanisa limeonesha nia ya makusudi kabisa ya kutaka kuwajengea vijana imani na kuwasikiliza katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi, kama sehemu muhimu sana ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Hili limekuwa ni tukio la kihistoria kwa vijana wengi, waliothubutu kuonesha kipaji cha ubunifu, ukarimu, kusikiliza, umoja na udugu.

Kwa upande wake, Percival Holt anakaza kwa kusema, vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wamegusia fursa, changamoto na matamanio yao halali, ingawa wanatoka sehemu mbali mbali za dunia zinazohitaji kuvaliwa njuga na Mama Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yanahitaji elimu makini, kanuni maadili na utu wema ili kuwawezesha vijana kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Ukosefu wa haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu; ukosefu wa fursa za ajira ni mambo yanayowachanganya sana vijana, kiasi kwamba, wanahitaji wandani halisi na madhubuti watakaowasindikiza katika hija ya maisha yao, ili kuendelea kuwa ni vyombo vya matumaini katika ulimwengu mamboleo unaosheheni changamoto mbali mbali!

Naye Laphidil Twumasi anasema, vijana wameshirikishwa kikamilifu, kiasi kwamba, wamechangia mawazo yao katika makundi mbali mbali kadiri ya lugha; wakasaidiana na vijana mahiri katika mitandao ya kijamii ili kuandaa “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” ambayo kwa hakika ni matunda ya ushirikiano wa vijana wengi na wala hakuna ambaye ametelekezwa pembezoni mwa jamii. Vijana wanasema, wanalipenda na wanataka kuona Kanisa likistawi na kusonga mbele kama Sakramenti ya wokovu wa walimwengu, lakini, sauti ya vijana halina budi kusikilizwa kwa makini na hatimaye, kufanyiwa kazi!

Kijana Briana Santiago amedadavua kuhusu mchango wa mitandao ya kijamii katika utangulizi wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Vijana walitumiwa maswali dodoso na wakayajibu na muhtasari wake kutolewa! Vijana wameguswa sana kutoka katika undani wa maisha yao, wameonesha udhaifu, nguvu na matumaini yao kwa Kanisa. Hawa ni vijana ambao wengi wao wanatoka katika familia, vyama vya kitume na Parokia ambazo zimetoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa vijana. Tofauti za kidini, kitamaduni, rangi na mahali anapotoka kijana, zimekuwa ni utajiri mkubwa unaofumbatwa katika matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.