2018-03-26 08:28:00

Papa Francisko: Siku ya 33 ya Vijana imewasha moto wa Sinodi!


Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuhitimisha Ibada ya Jumapili ya Matawi, tarehe 25 Machi 2018, ambamo waamini wametafakari kuhusu Fumbo la Mateso ya Kristo Yesu, amewasalimia na kuwatakia heri na baraka mahujaji kutoka ndani na nje ya Italia, lakini zaidi vijana waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana itakayotimua vumbi mwezi Oktoba, 2018 hapa mjini Vatican. Amewashukuru vijana wote walioshiriki kikamilifu kwa njia ya mitandao ya kijamii, hadi kufanikisha tukio hili la maisha na utume wa Kanisa kwa vijana. Baba Mtakatifu akifanya rejea kuhusu hija yake ya kitume nchini Perù hivi karibuni, amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Perù wanaoishi mjini Roma.

Maadhimisho ya Siku ya XXXIII ya Vijana Duniani kwa ngazi ya kijimbo, ambayo kwa mwaka huu yanaongozwa na kauli mbiu “Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” Lk. 1:30 ni sehemu muhimu sana ya maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana sanjari na Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 itakoadhimishwa mwezi Januari 2019, huko nchini Panamà. Katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, aliyeteuliwa na Mwenyezi Mungu kuwa Mama wa Mwanaye Mpendwa, Kristo Yesu. Bikira Maria anaendelea kufanya hija pamoja na waamini kwa kuwaongoza vijana wa kizazi kipya katika imani na udugu.

Bikira Maria, Mama wa Kanisa awasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi vyema maadhimisho ya Juma kuu. Wajifunze kutoka kwa Bikira Maria kudumisha ukimya wa ndani, wakiyaelekeza macho ya nyoyo zao na imani pendelevu kwa Kristo Yesu, kwa Njia ya Msalaba, inayowapeleka katika mwanga wa furaha ya Ufufuko wa Kristo Yesu, kutoka kwa wafu! Vijana wamemkabidhi Baba Mtakatifu Francisko “Hati ya Utangulizi wa Sinodi” itakokuwa pia ni sehemu ya “hati ya “Kutendea Kazi wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya Vijana, Mwezi Oktoba, 2018. Mwishoni, kabisa, Baba Mtakatifu amemshukuru Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu Askofu Fabio Fabene, Katibu mkuu msaidizi wa Sinodi za Maaskofu pamoja na Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu kwa kufanikisha maadhimisho haya kwa muda wa juma zima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.