2018-03-26 13:22:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Nimrudishie Bwana nini?


Mwanzo wa Kipindi cha Kwaresima, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetoa ujumbe wa Kwaresima unaoongozwa na kauli mbiu “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu”. Vatican News inapenda kukuletea mfululizo wa Ujumbe wa Kwaresima ambao tayari tumekwisha zungumzia: utangulizi unaoonesha matukio muhimu yanayopaswa kutafakariwa kwa mwaka 2018 yaani:  Jubilei ya miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara; Miaka 50 tangu Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania litoe Tamko kuhusu Hatima ya Taifa la Tanzania pamoja na maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa na Vitongoji unaotarajiwa kufanyika mwaka 2019.

Katika sura ya kwanza tumewashirikisha kuhusu roho  na sadaka ya umisionari; Sura ya pili: sasa ni zamu yetu kushiriki katika mchakato wa uinjilishaji kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Sura ya tatu: kuhusu umuhimu wa kusoma alama za nyakati nchini Tanzania: kisiasa, kiuchumi na kijamii- Leo, tunapenda kujikita katika sura ya nne: Nimrudishie Bwana nini? Kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kujizatiti katika kusimamia na kutekeleza haki; kwa kupatanishwa na Mungu; kwa sala, kufunga na kutoa sadaka!

SURA YA NNE: NIMRUDISHIE BWANA NINI? Alama za nyakati katika jamii yetu ya leo, na tafakari kuhusu maswali yaliyoulizwa havina budi kutupa msukumo ambao ni kinyume kabisa na mtazamo wa Kaini. Msukumo huo ni ule unaoanzishwa na kutambua mema aliyotufanyia Mungu Baba, hasa lile jema kuu la kuletewa, kuikubali na kuiishi Injili ya Bwana Wetu Yesu Kristo kama wamisionari wake waaminifu. Na moyo huu unasimama juu ya swali “Nimrudishie nini Bwana kwa mema aliyonitendea?” (Zab. 116:12).

Neno la Bwana Mungu wetu na Baba wa Mkombozi wetu Yesu Kristo, kama linavyosomwa siku ya Jumatano ya Majivu, siku tunapoanza kipindi cha Kwarezima, lina msukumo huohuo! Masomo pamoja na Injili ya siku hiyo yanalenga katika kukabiliana na swali hilo la Kaini linalotuhangaisha kila siku! Hivyo ili kuonesha shukrani kwa moyo wa kimisionari kwa Mungu Baba, ni vema tukafanya maamuzi ya kubadilisha maisha yetu katika Kwaresima wa mwaka huu 2018. Masomo hayo yana na dhamira husika kuu kama ifuatavyo: Toba ya kumrudia Mungu ni kwa njia ya kuondoa aina yoyote ya uonevu na kutenda haki. Kukiri kuwa tu wakosefu, na tunahitaji kufanya toba. Kupatanishwa na Mungu kama watumishi wake ni kuwa tayari kwa lolote hata kama ni kuchekwa au kuhangaishwa na ulimwengu. Sala, kufunga na kutoa sadaka vifanyike bila ‘kujipigia debe’!

Maamuzi na Utekelezaji ngazi ya Parokia na Jumuiya: Hivyo basi, katika kujibu swali ‘Nimrudishie nini Bwana?’, maswali yafuatayo yanapendekeza kitu gani kifanyike: Neno la Mungu linasema nini kwa Jumuiya na Parokia yetu kuhusu: Toba na thamani ya uhai wa watoto wetu, vijana wetu na familia zetu? Toba na haki za binadamu katika mila, desturi, siasa, sheria na uchumi? Kama wadhambi tuna wajibu gani mbele ya Mungu na mbele ya binadamu wenzetu? Jumuiya na Parokia yetu inaweza kufanya nini ili kurekebisha na kukuza: Moyo na tabia ya usikivu kwa sauti ya Mungu anayetuuliza kuhusu hali ya bindamu kama ndugu zetu? Moyo na tabia ya kujali utu, hadhi na haki za binadamu wenzetu, hasa wanyonge na wanaogandamizwa? Kuchangia katika mabadiliko ya kisiasa, kijamii na kiuchumi ili maendeleo ya kweli yapatikane kadiri ya tunu za Ufalme wa Mungu?

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, 2018.
All the contents on this site are copyrighted ©.