2018-03-24 14:13:00

Vijana tumieni karama zenu kumpenda Yesu na kuwahudumia maskini!


Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu ambamo, Mama Kanisa anaadhimisha kwa namna ya pekee, Fumbo la Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kwa ajili ya ukombozi mwa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Ni wakati muafaka wa kutafakari: huruma, upendo na msamaha wa Mwenyezi Mungu kwa binadamu anayeogelea katika lindi la dhambi na utumwa wa shetani, Ibilisi. Juma kuu linawawezesha waamini kukutana na Kristo Yesu, ufunuo wa Uso wa huruma ya Mungu, upendo na msamaha wa kweli, tunu msingi zinazowawezesha waamini kukua na hatimaye, kukomaa katika imani, huku wakishirikiana na kushikamana na majirani zao.

Lengo ni kupata furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo Mfufuka, changamoto na mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza katika ukarimu kama kielelezo cha utimilifu wa maisha! Kuanzia tarehe 25 Machi yaani Jumapili ya Matawi hadi tarehe 1 Aprili, 2018, Sherehe ya Ufufuko wa Bwana kutoka kwa wafu, Jukwaa la Wanafunzi 2, 500 kutoka Vyuo Vikuu, “Forum Univ 2018” chini ya mwamvuli wa "Praelatura Sanctae Crucis et Opus Dei “Jimbo la Kitume la Kazi ya Mungu” kwa kifupi “Opus Dei” wanashiriki katika maadhimisho ya Juma kuu hapa mjini Roma. Jukwaa hili lilianzishwa kunako mwaka 1968 na Mtakatifu Josemarìa Escrivà muasisi wa “Opus Dei” ili kuwasaidia wanafunzi kutakatifuza maisha yao, ili hatimaye, waweze kuyatakatifuza malimwengu!

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, anawataka vijana wa Jukwaa la Vyuo Vikuu, kushiriki kikamilifu katika tukio hili la maisha na utume wa Kanisa kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana itakayoadhimishwa mjini Vatican, mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”. Ni wakati muafaka wa kumwangalia na kumtafakari tena Mtume Yohane, Mwanafunzi aliyependwa sana na Kristo Yesu, aliyemkabidhi kwa Bikira Maria kuwa Mama yake na Mama wa Kanisa. Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wale wote wanaokutana na Kristo Yesu, kumbe, Mtakatifu Yohane, anaweza kuwasaidia vijana kumtambua Yesu anayepita katika maisha ya ujana, ili waweze kuwa tayari kumfuasa kwa ari na moyo mkuu.

Mtakatifu Josemarìa Escrivà kama sehemu ya wosia wake, anasema Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote kumfuasa Kristo Yesu kwa furaha na bashasha ili kumpenda na kumtumikia Mungu pamoja na jirani bila ya kujibakiza hata kidogo. Kwa ufupi Mtakatifu Josemarìa anawataka waamini kumtafuta, kumkumbatia na kumpenda Kristo Yesu katika maisha yao, daima wakijitahidi kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano yao na Kristo Yesu, kwa kujitahidi kutekeleza mapenzi yake katika uhalisia wa maisha yao.

Mtakatifu Josemarìa Escrivà anawataka waamini kujitahidi kufanana na Yesu ili waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vyake kwa ajili ya jirani zao. Anawataka kumtafuta Kristo Yesu katika maisha ya sala, Sakramenti za Kanisa, Matukio mbali mbali ya maisha pamoja na wale wote wanaowazunguka, lakini zaidi maskini na wale wote waliosahauliwa, watu ambao ni sura ya Kristo. Baba Mtakatifu anawataka vijana kutoka katika ubinafsi wao kwa kushinda kishawishi cha kutaka raha mustarehe na mambo ya dunia, tayari kuanza safari ya kukutana na maskini, ili kuwahudumia kwa kutumia karama na mapaji yao. Hii ndiyo njia muafaka ya kumfuasa Kristo na kuwa na moyo unaosheheni upendo wa dhati mbele yake. Baba Mtakatifu analiombea Jimbo la “Opus Dei” na miradi yake yote, ili daima wasikie na kuonja upendo wa Kristo anayewaita kujisadaka katika huduma makini kwa maskini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.