2018-03-21 16:09:00

Sinodi ya Vijana! Hakuna kulala, Jumapili wanawasilisha hati kwa Papa


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuona Kanisa linajizatiti katika ujenzi wa wa utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza, kuwathamini, kuwaongoza na kuwasindikiza katika hija ya maisha yao, ili kweli waweze kuwa ni “majembe” yanayotumainiwa katika maisha na utume wa vijana, tayari kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu! Baba Mtakatifu anataka kutoa kipaumbele cha kwanza kwa vijana katika maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, inayoongozwa na kauli mbiu: “Vijana, imani na mang’amuzi ya miito”.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, hii ni Sinodi ya vijana, kwa ajili ya vijana pamoja na vijana, kwani wao ndio wadau wakuu katika maadhimisho haya na kwamba, tayari wamekwisha anza kuonesha “cheche” za ushiriki wao kwa kutoa maoni, kilio na matumaini yao kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake na kwamba, wanatarajia kumkabidhi Baba Mtakatifu Francisko, Hati ya Utangulizi wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, Jumapili ya Matawi, wakati wa maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Duniani, inayoadhimishwa mwaka huu katika ngazi ya kijimbo!

Kardinali Baldisseri anaendelea kufafanua kwamba, wawakilishi wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watamkabidhi Baba Mtakatifu: matatizo, hofu, mashaka, changamoto, fursa na matumaini ya vijana wa kizazi kipya, ili Mababa wa Sinodi, waweze kuyatafutia ufumbuzi muafaka, tayari kupyaisha uso wa Kanisa kwa tunu msingi za maisha na wito wa vijana waliokomaa kiimani, kiutu na kimaadili! Maadhimisho haya yamewakusanya wawakilishi wa vijana kutoka katika kada mbali mbali, madhehebu na dini mbali mbali, ili kwa pamoja waweze kulisaidia Kanisa kuibua mbinu mkakati wa utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anakazia sana utamaduni na sanaa ya kuwasikiliza vijana, kwani wao ndio wahusika wakuu katika mchakato mzima wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Vijana nao wanapaswa kusikilizana wao kwa wao na kujenga tabia ya kuwasikiliza na kuwathamini wazazi na walezi wao kama sehemu ya mchakato wa utekelezaji wa hija ya pamoja inayofanywa na Mama Kanisa katika kipindi cha Mwaka 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.