2018-03-21 15:07:00

Monsinyo Dario Eduardo Viganò ang'atuka kutoka madarakani!


Baba Mtakatifu Francisko amekubali ombi lililowasilishwa kwake na Monsinyo Dario Edoardo Viganò la kutaka kung’atuka kutoka madarakani kama Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Mawasiliano mjini Vatican na kwamba, hadi uteuzi mwingine utakapofanyika, Monsinyo Lucio Adrian Ruiz atakaimu nafasi yake! Baba Mtakatifu anampongeza Monsinyo Viganò kwa kufikia maamuzi machungu kiasi hiki na kumwomba hata akiwa nje ya ofisi za Sekretarieti ya Mawasiliano kuendelea kusaidia shughuli za mageuzi kama zilivyobainishwa na Baraza la Makardinali Washauri na kupitishwa na Baba Mtakatifu mwenywe!

Tangu wakati huu, Gazeti la L’Osservatore Romano litakuwa ni sehemu ya muundo mpya wa vyombo vya mawasiliano vinavyomilikiwa na kuendeshwa na Vatican sanjari na Kiwanda cha Uchapaji cha Vatican. Baba Mtakatifu anamshukuru na kumpongeza Monsinyo Viganò kwa jitihada zote alizofanya kwa moyo wa unyenyekevu na ushirikiano wa dhati na wasaidizi wake wa karibu sanjari na Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu anahitimisha shukrani zake kwa Monsinyo Viganò kwa kusema, mageuzi ndani ya Kanisa yanafumbatwa katika ari na moyo wa huduma na wala si mabadiliko ya miundo mbinu!

Kwa upande wake, Monsinyo Dario Edoardo Viganò katika barua aliyomwandikia Baba Mtakatifu Francisko anasema, tangu mwaka 2015 tangu alipomkabidhi dhamana na wajibu wa kuongoza Sekretarieti ya Mawasiliano Vatican katika mchakato mzima wa mageuzi, licha ya: utendaji na nia njema iliyokuwepo, lakini bado ameonekana kuwa ni kikwazo na mzigo katika utekelezaji wa mageuzi ya Sekretarieti kuu. Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kumwamini na kwamba, anapenda kujiweka kando ili kuhusu kushika kasi zaidi kwa mageuzi ndani ya Vatican yanayohitaji upyaisho wa rasilimali watu; toba na wongofu wa ndani unaofumbatwa katika maisha ya kiroho, kiutu na kitaaluma. Anasema, kwa kukaa kwake pembeni katika mchakato wa mageuzi ya Vatican, kutamwezesha kuzaliwa tena kutoka juu kama ilivyokuwa kwa Nikodemu, ili Kanisa liweze kuendeleza mchakato wa mageuzi kwa kupenda kwa dhati, kuishi na kuhudumia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.