2018-03-20 10:05:00

Papa: Kazi ya Askofu ni kufundisha, kuongoza na kutakatifuza!


Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, ambamo Askofu aliyewekwa wakfu anapewa dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu ni kielelezo cha ukuhani mkuu, kilele cha huduma takatifu. Maaskofu kwa namna iliyo ya juu kabisa, hushika nafasi ya Kristo Yesu mwenyewe, aliye mwalimu, mchungaji na kuhani na kwamba, Maaskofu wanatenda kazi yao katika nafsi yake. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Maaskofu wanafanywa walimu kweli na halisi wa imani, makuhani na wachungaji.

Baba Mtakatifu Francisko, katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, tarehe 19 Machi 2018 amewaweka wakfu Maaskofu wakuu wateule watatu, aliowateuwa hivi karibuni kuwa wawakilishi wa Vatican sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni Askofu mkuu Waldemar Stanislaw Sommertag, Askofu Mkuu Alfred Xuereb pamoja na Askofu mkuu Josè Avelino Bettencourt.

Baba Mtakatifu katika mahubiri yake amefafanua kazi na wajibu wa Maaskofu katika maisha na utume wa Kanisa kwa kusema, kwamba, hawa wamewekwa wakfu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Yesu sanjari na kuendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo, Kuhani mkuu na wa milele. Kristo kwa njia ya Maaskofu, anaendelea kutangaza Habari Njema na kuwatakatifuza waja wake kwa njia ya Sakramenti za imani, kiasi hata cha kuliwezesha Kanisa kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kristo anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa busara na hekima, kazi inayopaswa kutekelezwa na Maaskofu wanapowaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili hatimaye, waweze kufikia furaha ya maisha ya uzima wa milele.

Baba Mtakatifu amewaalika Maaskofu wenzake, kuwapokea Maaskofu wapya waliowekwa wakfu katika Urika wa Maaskofu ambao unawashirikisha katika umoja wa kiaskofu kwa nguvu ya utakaso wa Kisakramenti na kwa ushirika wa kihierarkia pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maaskofu wapya wametakiwa kuonesha nidhamu na heshima kubwa kwa Daraja waliyoipokea kama wagawaji wa Mafumbo ya Mungu, mashuhuda wa Injili ya Kristo na mitume wa Roho Mtakatifu anayetakatifuza, mwaliko kwa waamini kuwasikiliza Maaskofu wao kwa dhati kabisa kama ushuhuda wa kumsikiliza Kristo mwenyewe!

Maaskofu wakuu wapya wamekumbushwa kwamba, wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu wa Mungu na hivyo kuwekwa wakfu kwa ajili ya mambo ya Mungu. Hili si Daraja kwa ajili ya kujitafutia mali na malimwengu yake, wala si jukwaa la kisiasa, bali Uaskofu ni kwa ajili ya huduma na kwamba, wanapaswa kukikimbia kishawishi cha kutaka kuwa Wafalme na watawala. Maaskofu watangaze Neno la Mungu; wawaonye watu na kufundisha kwa ari na moyo mkuu tunu msingi za Kiinjili.

Kwa njia ya sala na sadaka yao, wawatakatifuze watu wa Mungu ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa utakatifu katika Kristo Yesu. Dhamana ya kwanza ya Askofu ni kusali, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanasali daima kama sehemu ya utekelezaji wa wito wao. Wamekabidhiwa na Mama Kanisa dhamana ya kuwa ni walinzi na waadhimishaji wa Mafumbo ya Kanisa; wakuu wa familia ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu, Mchungaji mwema anayewafahamu Kondoo wake kwa majina na wao wanamtambua kiasi kwamba, akawa tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili yao!

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwapenda watu wao kwa dhati, lakini zaidi waoneshe umoja na mshikamano na wakleri, wadau wakuu katika utume wao kama Maaskofu. Wakleri wawe na fursa ya kuweza kukutana na kuzungumza na Maaskofu wao bila mizengwe mizengwe. Maaskofu wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; watu wanaohitaji kuonjeshwa huruma pamoja na kupewa msaada wanaohitaji.

Maaskofu wajitahidi kushirikiana na kushikamana na waamini walei katika maisha na utume wao; kwa kuwasikiliza na kuwathamini. Waoneshe ari na moyo wa majadiliano ya kiekumene na kidini; kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya Makanisa mengine yanayohitaji pia msaada wa hali na mali. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu kukesha na kusali katika upendo kama mashuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambao wamewekwa wakfu ili kuwa waalimu, makuhani na wachungaji. Roho Mtakatifu awasaidie Maaskofu kudhibiti udhaifu wao wa kibinadamu kwa kuambata huruma na neema ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.