2018-03-20 14:33:00

Papa Francisko: Katika ukavu wa maisha ya kiroho, angalieni Msalaba


Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahamasisha waamini wanapokabiliana na ukavu wa maisha ya kiroho, kujitahidi kuangalia Fumbo la Msalaba, badala ya kuporomosha matusi na kashfa dhidi ya Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Waisraeli kule Jangwani, kiasi cha kumkasirisha Mungu na wakakiona cha mtema kuni! Wayahudi walimlalamikia Mungu pamoja na mtumishi wake Musa kwa kuwapandisha kutoka Misri, ili wafe Jangwani, kwa njaa na kiu! Ni watu wenye shingo nguvu waliosahau wema na ukarimu wa Mungu katika safari yao Jangwani, walipokuwa na kiu akawapatia maji pale Meriba na kuwalisha kwa manna iliyoshuka kutoka mbinguni.

Baba Mtakatifu ameyasema haya wakati wa mahubiri yake, Jumanne, tarehe 20 Machi 2018 kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Amesikitika kusema kuwa malalamiko haya yalitolewa na Waisraeli walipokuwa wanakaribia kwenye Nchi ya ahadi, iliyojaa maziwa na asali, lakini walikuwa na woga mkubwa dhidi ya wenyeji wa nchi hii, kiasi cha kuanza kusita na kupoteza matumaini! Ni watu wenye shingo nguvu walioanza kuangalia nguvu yao ya kibinadamu na kusahau jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu alikuwa amewakomboa kwa mkono wenye nguvu kutoka utumwani Misri. Walikuwa na kumbukumbu potofu juu ya masufuria ya nyama na makapu ya vitunguu swaumu, wakasahau kwamba, huko walikuwa ni watumwa. Baba Mtakatifu anawataka waamini kuwa na kumbu kumbu endelevu juu ya wema, huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao ya kila siku na kamwe wasimpatie nafasi Shetani, Ibilisi kuwavuruga! Shetani ni alama ya sumu katika maisha ya kiroho. Nyoka wa Shaba aliyetengenezwa na Musa akawa ni kimbilio la wale waliokuwa wameumwa na nyoka ni ishala ya Msalaba inayoleta wokovu kwa binadamu wote.

Musa katika maelezo haya anatabiri kuhusu Fumbo la Msalaba, ambalo ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ufunuo, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kristo Yesu, baada ya kuinuliwa juu amewavuta watu wengi kwakwe! Fumbo la Msalaba ni utukufu wa Mwana mpendwa Mungu unaojifunua kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake kutoka kwa wafu! Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, katika utupu wa maisha na mahangaiko yao ya ndani, kumkimbilia Kristo Yesu pale Msalabani, ili kuguswa na huruma, upendo na upya wa maisha unaobubujika kutoka katika mti wa Msalaba. Baba Mtakatifu anawaalika wazazi na walezi kuuangalia Msalaba kwa jicho la imani, matumaini na mapendo; ili kwa njia ya Madonda yake Matakatifu, waonje huruma, upendo na msamaha wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.