2018-03-20 15:14:00

Askofu mkuu Piero Pioppio ateuliwa kuwa Balozi wa ASEAN.


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Piero Pioppio kuwa Balozi mpya wa Vatican kwenye Shirikisho la Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, A.S.E.A.N. Ataendelea pia kuwa Balozi wa Vatican nchini Indonesia. Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 29 Septemba 1960 Jimboni Savona na Noli, nchini Italia. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 29 Juni 1985 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimboni Acqui, nchini Italia. Alijiendeleza zaidi na kujipatia shahada ya uzamivu katika masomo ya taalimungu.

Tarehe Mosi, Julai 1993 akaanza utume wake katika masuala ya kidiplomasia mjini Vatican. Tangu wakati huo, akatumwa nchini Korea, Chile na baadaye akarejeshwa tena kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican. Tarehe 25 Januari 2010, Baba Mtakatifu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na kuwekwa wakfu hapo tarehe 18 Machi 2010. Akateuliwa kuwa Balozi wa Vatican nchini Cameroon na Equatorial Guinea. Tarehe 8 Septemba 2017, Baba Mtakatifu Francisko akamteua kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Indonesia. Tarehe 19 Machi 2018, Baba Mtakatifu Francisko akamteua pia kuwa Balozi wa Shirikisho la Nchi za Kusini Mashariki mwa Asia, A.S.E.A.N. yaani “Association of Southerneast Asian Nations” lililoanzishwa kunako tarehe 8 Agosti 1967 ili kukuza ushirikiano wa kiuchumi sanjari na kuimarisha amani na utulivu katika Ukanda huu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.