2018-03-17 14:14:00

Sherehe ya Mt. Yosefu, Papa Francisko kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu


Kila mwaka ifikapo tarehe, 19 Machi, Mama Kanisa anaadhimisha Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wa Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Ni nafasi muafaka ya kumtafakari kwa kina na mapana Mtakatifu Yosefu aliyeonesha na kushuhudia unyenyekevu na hekima ya hali ya juu katika mchakato mzima wa ulinzi na tunza kwa Familia Takatifu. Huyu anaitwa mtumishi mwaminifu wa Mungu. Ni uaminifu wake huo ambao unamshirikisha kwa namna iliyositirika katika historia nzima ya wokovu wetu. Matendo yake ya imani, mapendo na matumaini hayadhiiriki kwa wazi sana katika Maandiko Matakatifu lakini ni ya kupewa mkazo wa kipekee, mathalani kwa kuwa mtii katika hali ya ukimya wakati wa kuitikia sauti ya Mungu. Huyu ndiye wakili mwaminifu na mwenye busara. Kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria, “ndiyo” ya Mtakatifu Yosefu katika mpango wa ukombozi wa mwanadamu  ndiyo inayompatia ukuu. Huu ni mwanzo wa safari ya utii wa Mtakatifu wa Yosefu katika mpango mzima wa ukombozi wa mwanadamu. Yeye kama Baba mlishi ndani ya Familia Takatifu anayachukua kikamilifu majukumu yake ya kuwa mlinzi na mtegemezaji wa familia.

Baba Mtakatifu Yohane Paulo II katika waraka wake Redemptoris Custos anaongeza kwa kusema: “Kama vile Mtakatifu Yosefu alivyochukua jukumu la kumtunza kwa upendo Bikira Maria na kwa furaha akajitoa katika kumtunza Yesu Kristo, vivyo hivyo ndiyo anavyolitunza na kuliangalia Fumbo la Mwili wa Kristo, Kanisa ambalo Bikira Maria ni mfano na kielelezo”. Nafasi hii ya Mtakatifu Yosefu inatekelezwa katika hali ya unyenyekevu na ukimya kabisa. Mtakatifu Yosefu anaonesha mfano bora kabisa kwa maisha yetu ya kikristo. Daima hakusita kutimiza wajibu wake kama Baba wa familia na kuutekeleza kwa uaminifu mkubwa kabisa hata katika mazingira ambayo yalikuwa ni magumu na tete. Pia alijitoa mhanga kusafiri usiku kucha wakati wakimtorosha Mtoto Yesu ili kuilinda familia hii takatifu ya Mungu na mkono dhalimu wa mfalme Herode. Katika maisha ya familia kule Nazareti aliangaika kama Baba kuitafutia familia mahitaji yake ya kila siku na hii inathibitishwa na jinsi Kristo alivyojulikana kuwa ni “Mwana wa Seremala”. Huu ni mwaliko pia kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kujinyenyekesha mbele ya Mwenyezi Mungu. Ikumbukwe kwamba, fadhila ya unyenyekevu na heshima inayofumbatwa katika maisha ya Mtakatifu Yosefu, Baba Mlishi wa Yesu inaonesha umuhimu wa kujenga na kudumisha majadiliano yanayofumbata: ukweli, ustawi na maendeleo ya wote.

Baba Mtakatifu Francisko tarehe 19 Machi 2018 anaadhimisha kumbu kumbu ya miaka 5 tangu alipoanza rasmi utume wake kwa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujikita katika mambo makuu matatu: amani, maskini na mazingira. Kumbu kumbu hii kwa mwaka huu inapata umuhimu wa pekee kwa Baba Mtakatifu kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu wateule: Josè Avelino Bettencourt, Alfred Xuereb pamoja na Waldemar Stanisław Sommertag walioteuliwa hivi karibuni kuwa Mabalozi wa Vatican katika nchi mbali mbali. Baba Mtakatifu anatarajia kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwaweka wakfu Maaskofu wakuu wateule kuanzia saa 11:00 Jioni kwa Saa za Ulaya.

Askofu mkuu mteule Josè Avelino Bettencourt, aliyateuliwa hivi karibuni kuwa Balozi mpya wa Vatican  nchini Georgia, ataendelea pia kuwa ni mwakilishi wa Vatican nchini Armenia  pamoja na kuwa Mkuu wa Itifaki ya Vatican. Alizaliwa tarehe 23 Mei 1962 huko Azzorre, nchini Ureno. Baada ya majiundo na malezi yake ya Kikasisi, kunako tarehe 29 Juni 1993 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre, Jimbo kuu la Ottawa, Canada. Ametunukiwa shahada ya Uzamivu katika Sheria za Kanisa. Alianza utume wake katika masuala ya kidiplomasia mjini Vatican kunako tarehe 1 Julai 1999. Katika maisha na utume wake tangu wakati huo, ametoa huduma kwenye Ubalozi wa Vatican nchini DRC na baadaye, kwenye Idara ya mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa. Baadaye, Papa Mstaafu Benedikto XVI alimteuwa kuwa mkuu wa Itifaki ya Vatican, hapo tarehe 14 Novemba 2012. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Armenia mwaka 2018 na kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu.

Askofu mkuu mteule Alfred Xuereb, alizaliwa tarehe 14 Oktoba 1958 huko Gozo, Malta. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo tarehe 26 Mei 1984. Ana shahada ya Uzamivu katika taalimungu. Alianza utume wake mjini Vatican kuanzia mwaka 1991. Tarehe 1 Septemba 1995 akahamishiwa kwenye Sekretarieti kuu ya Vatican kwa ajili ya masuala ya jumla. Mwaka 2000, akateuliwa kuwa afisa katika nyumba ya Kipapa na mwaka 2007 akateuliwa kuwa ni kati ya Makatibu muhtasi wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na tarehe 15 Machi 2013 akateuliwa kuwa Katibu muhtasi wa Papa Francisko.

Askofu mkuu mteule Waldemar Stanisław Sommertag kutoka Jimbo Katoliki la Pelpin, nchini Poland, alizaliwa kunako tarehe 6 Februari 1968. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 30 Mei 1993. Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Nicaragua, hapo tarehe 15 Februari 2018.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.