2018-03-17 09:43:00

Mapambano dhidi ya biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya!


Takwimu zinaonesha kwamba, waathirika wakuu wa matumizi haramu ya dawa za kulevya ni watoto na vijana wenye umri kuanzia miaka 15-35 na kwamba, madhara yake ni makubwa sana kwa kiafya kwani yanachangia kuenea kwa magonjwa kama Ukimwi na Kifua kiuu na hivyo kudidimiza nguvu kazi ya taifa. Vijana wengi wamekuwa ni mzigo mkubwa kwa familia, jamii na taifa katika ujumla wake kutokana na vitendo vya kihalifu na hivyo kupelekea kuchafua sifa njema ya familia na jamii zao. Ni vijana ambao wamechakaa kama “jani la mgomba” si mali kitu tena: kiroho na kimwili, kiasi hata kutengwa na jamii pamoja na familia zao, kwani wanakuwa kweli ni watu hatari! 

Lakini, Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya sera na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya, analitaka Kanisa kuwasikiliza kwa makini vijana hawa wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili kuwajengea uwezo na dhamiri nyofu itakayowawezesha kukataa katu katu kishawishi cha kutumbukia au kutumbukizwa katika matumizi haramu ya dawa za kulevya! Takwimu zinaonesha kwamba, “mateja wa dawa za kulevya” hudhoofisha nguvu kazi ya taifa na hivyo kukwamisha jitihada za maboresho katika medani mbali mbali za maisha ya watu!

Baba Mtakatifu anatambua fika madhara ya matumizi haramu ya dawa za kulevya na hivyo anawataka vijana wa kizazi kipya kuachana kabisa na tabia ya: kutumia, kusambaza na kuuza kwani waathirika wengi ni vijana wenzao. Baba Mtakatifu anawaalika vijana walioathirika na matumizi haramu ya dawa za kulevya kujitokeza katika taasisi zilizopewa dhamana na jukumu la kutoa tiba kwa waathirika kama wao, ili waweze kupatiwa ushauri nasaha pamoja na tiba, itakayowawezesha kuanza kundika ukursa mpya wa matumaini katika maisha yao. Baba Mtakatifu Francisko ili kuwasaidia Mababa wa Sinodi kusikiliza kilio cha waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ameamua kuwaalika vijana wawili: mvulana na msichana, walioathirika kwa matumizi haramu ya dawa za kulevya, ambao kwa sasa wanaendelea kupata ushauri nasaha na matibabu kutoka katika Kituo cha Mshikamano cha Don Mario Picchi, nchini Italia, CelS kushiriki katika maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Vijana, inayoadhimishwa hapa mjini Vatican kuanzia tarehe 19 hadi 25 Machi 2018.

Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka wa Huruma ya Mungu anasema, Roberto Mineo, Rais wa Kituo hiki, kinachopania kutoa ushauri nasaha kwa waathirika wa matumizi haramu ya dawa za kulevya; mitandao ya kijamii kama vile interneti, ulevi wa kupindukia na biashara ya ngono; ulafi, michezo ya kamari na upatu. “Mradi wa utu na heshima ya binadamu” unaofumbatwa katika falsafa ya Don Mario Picchi unaonesha kuwepo kwa mafanikio makubwa, kwani, unawajengea vijana uwezo wa kujiamini na kujitambua; kwa kuwaheshimu na kuwatambua watu wengine tayari kujenga sanaaq na utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi. Huu ni mwaliko wa kuheshimu na kuthamini tofauti msingi zinazojitokeza kati yao kuwa ni tunu na utajiri mkubwa unaopaswa kufumbatwa na kuendelezwa na wengi, bila kubezana wala kugeuziana kisogo, bali kushirikiana na kutegemezana katika ukweli na uwazi. Miundo mbinu pamoja na uwepo wa shule za mafunzo na majiundo makini zimekiwezesha Kituo cha Mshikamano cha Don Mario Picchi kupata mafanikio makubwa katika maisha na utume wake. Lengo ni kuwasaidia watu maskini na dhaifu, ili kujiamini na hatimaye, kushiriki katika mchakato wa upyaisho wa maisha ya ujana wao! Ujana mali, lakini fainali uzeeni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.
All the contents on this site are copyrighted ©.