2018-03-16 13:06:00

Wanavyuo Tanzania waandaliwe katika kujiajiri binafsi!


Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema ni umuhimu mfumo wa ufundishwaji wa wanafunzi wa vyuo vikuu nchini Tanzania ukaboreshwa ili wanapomaliza waweze kujiajiri. “Kumekuwa na tatizo kubwa la wasomi wetu kuwa na mtazamo kwamba wanapomaliza masomo yao lazima waajiriwe. Upo umuhimu wa kubadili mtazamo huo kwa kuwapa mbinu zitakazowawezesha kujiajiri.” Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo, Ijumaa, Machi 16, 2018, alipokutana na kufanya mazungumzo na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam Prof. William Anangisye, ofisini kwake mjini Dodoma.

Amesema wanafunzi hao wanapomaliza wanatarajiwa wawe na uwezo wa kubuni mbinu mbalimbali za kujiajiri na kuondokana na mtazao wa kusubiri ajira za kuajiriwa maofisini. Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kuchukua kauli mbiu ya Rais Dkt. John Magufuli ya uchumi wa viwanda kwa kuanzisha kilimo cha mazao mbalimbali yatakayotoa malighafi za viwandani. Pia Waziri Mkuu amesema wasomi hao wanaweza kujikita katika shughuli za uchimbaji wa madini au usindikaji wa mazao mbalimbali, hivyo tayari watakuwa wamejiajiri kwa sababu ajira si za ofisini pekee. Aidha, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kumpongeza Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam aliyestaafu Profesa Rwekaza Mukandara kwa kazi nzuri aliyoifanya kipindi cha uongozi wake.

Kwa upande wake, Profesa Anangisye amesema mzigo aliopewa wa kuiongoza taasisi hiyo si mwepesi, hivyo ameahidi kufanya kazi kwa bidii na hatokwenda kinyume na matarajio ya Serikali ya Awamu ya Tano. Kiongozi huyo amesema, katika kuhakikisha wanaboresha masomo chuoni hapo wameanzisha skuli ya kilimo na uvuvi, hivyo wanatarajia kuanzisha mashamba ya mfano kwa ajili ya mazao mbalimbali.

IMETOLEWA NA:

OFISI YA WAZIRI MKUU,

S. L. P. 980

IJUMAA, MACHI 16, 2018.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.