2018-03-16 06:37:00

Vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii! Msiogope!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, kwa maadhimisho ya Siku ya 33 ya Vijana Duniani ambayo kwa Mwaka 2018 inaadhimishwa kwa ngazi ya kijimbo, inaongozwa na kauli mbiu “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu”. Lk. 1:30. Maadhimisho ya Mwaka 2018 kwa ngazi ya Kijimbo yatafanyika tarehe 25 Machi, Mama Kanisa anapoadhimisha Jumapili ya Matawi, mwanzo wa maadhimisho ya Juma kuu, Kanisa linapofanya kumbu kumbu ya: Mateso, kifo na Ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu!

Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha ambalo limepewa dhamana ya kuandaa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani linasema, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwaalika vijana kujiaminisha kwenye ulinzi na tunza ya Bikira Maria kama sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2018. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuorodhesha woga, wasi wasi na mashaka yanayowaandama katika maisha, wanapotafakari ujumbe wa Malaika Gabrieli alipokuwa anampasha Bikira Maria habari kwamba, atakuwa Mama wa Mungu! Baada ya majadiliano ya kina, mwishoni Malaika Gabrieli akamwambia Bikira Maria“Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu”. 

Maadhimisho ya Siku ya 34 ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 yataongozwa na kauli mbiu “Tazama mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Baba Mtakatifu katika maandalizi haya anapenda kuwatafakarisha vijana taalimungu ya maisha mintarafu utenzi wa Bikira Maria “Magnificat”  ili kuwatia moyo vijana wa kizazi kipya kusonga mbele kwa imani na matumaini bila ya kukata wala kukatishwa tamaa kwa kuangalia kumbu kumbu ya historia yao ya zamani, bali wawe na ujasiri ili kukabiliana na changamoto mamboleo, daima wakiwa na imani na matumaini kwa mambo ya mbeleni!

Maandalizi haya yanakwenda sanjari na maandalizi ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, ambayo yatafanyika mwezi Oktoba 2018 kwa kuongozwa na  na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito”. Utangulizi wake unafanyika kuanzia tarehe 19 Machi 2018, Mama Kanisa anapoadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Yosefu, mchumba wake Bikira Maria na Msimamizi wa Kanisa la Kiulimwengu. Maadhimisho haya yanakwenda sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitano, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa la Kristo!

Hatima ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana ni hapo tarehe 25 Machi 2018, Jumapili ya Matawi, siku ambayo wawakilishi wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wataungana na Baba Mtakatifu Francisko kuadhimisha Siku ya 33 ya Vijana Duniani ambayo kwa mwaka 2018 inaadhimishwa kwa ngazi ya kijimbo! Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Bikira Maria wa Lourdes, tarehe 11 Februari 2018 alizindua mchakato wa vijana kujiandikisha kwenye maadhimisho ya Siku ya XXIV ya Vijana Duniani. Baba Mtakatifu anawataka vijana kufanya tafakari ya kina kuhusu imani na mang’amuzi ya wito wao, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.