2018-03-15 13:44:00

Oyaaa! Vijana waanza kutinga timu Vatican kwa maadhimisho ya Sinodi


Baba Mtakatifu Francisko tarehe 4 Oktoba 2017 alitangaza kwamba, kuanzia tarehe 19 Machi 2018 Sherehe ya Mtakatifu Yosefu mchumba wake Bikira Maria, hadi tarehe 24 Machi 2018, kunaadhimishwa utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana inayoongozwa na kauli mbiu: “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Hii ni safari ya maisha ya Kanisa katika kujenga utamaduni wa kuwasikiliza vijana, kuwajali, kuimarisha imani pamoja na kusikiliza changamoto zinazotolewa na vijana wa kizazi kipya. Ndiyo maana Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, hitimisho la utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana litakuwa ni sehemu ya “Hati ya Kutendea Kazi" "Instrumentum Laboris" itakayowasilishwa kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu itakayoadhimishwa rasmi mwezi Oktoba, 2018.

Kanisa linataka kuboresha sera na mikakati ya maisha na utume kwa vijana wa kizazi kipya, ili waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake, sanjari na kufanya maamuzi magumu katika maisha yao, kwa kuwajibika kwa dhati bila kukwepa, baada ya kujengewa uwezo wa kujiamini! Hati ya Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, inatoa mwaliko kwa vijana wote, ili waweze kupata utimilifu wa furaha ya maisha, kwani Kanisa limekabidhiwa dhamana ya kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili.  Huu ni mwaliko wa kuwasaidia vijana ili kupata mang’amuzi kuhusu miito mbali mbali ndani ya Kanisa kama: watu wa ndoa, watawa na mapadri, ili kwa njia ya mwanga wa imani, wawe tayari kushuhudia utimilifu wa furaha katika miito yao.

Ratiba elekezi inaonesha kwamba, wawakilishi wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wanaanza “kutinga timu” kuanzia sasa na Jumapili tarehe 18 Machi 2018 watapokelewa na kusajiliwa kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu na baadaye wataadhimisha Ibada ya Misa kwa pamoja, mwanzo wa kufahamiana. Jumatatu tarehe 19 Machi 2018, Siku kuu ya Mtakatifu Yosefu Mchumba wake Bikira Maria, sanjari na kumbu kumbu ya miaka mitano tangu Baba Mtakatifu Francisko alipoanza utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, vijana wataanza mkutano wao chini ya uongozi wa Kardinali Lorenzo Baldisseri; watakutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu ambaye pia atasikiliza shuhuda za vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakatifu “apata wasaa wa kupiga michapo na vijana hawa” na baadaye watapewa maelekezo ya maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi na mwishoni watagawanyika katika makundi madogo madogo ili kurahisisha shughuli hii.

Jumanne, tarehe 20 Machi 2018, rataiba elekezi inaonesha kwamba, vijana watapata nafasi ya kusali na kutafakari katika makundi madogo madogo na kwamba, siku nzima itakuwa ni kazi ya makundi kadiri ya lugha zao. Jumatano, tarehe 21 Machi 2018, baada ya sala na tafakari, wawakilishi wa vijana wataandaa muhtasari utakaotumika kuandika muswada wa hati ya mwisho wa maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana na hatimaye, muhtasari huu utawasilishwa kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Alhamisi tarehe 22 Machi 2018, baada ya sala na tafakari, vijana watawasilisha onesho la video na muswada wa hati ya mwisho. Vijana watapata nafasi ya kuupitia muswada huu katika makundi na hatimaye, wawezeshaji wakuu watawasilisha muswada huu kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu. Ijumaa, 23 Machi 2018 vijana wataendelea kutoa maoni yao juu ya muswada wa hati ya mwisho. Waswahili wanasema, hapa ni kazi na dawa! Jioni vijana watapata nafasi ya kutembelea Makatakombi ya Mtakatifu Calistus yaliyoko mjini Roma, wataadhimisha Njia ya Msalaba na baadaye jioni wataangalia tena muswada wa hati ya mwisho.

Jumamosi, tarehe 24 Machi 2018, baada ya sala na tafakari, vijana watapitia muswada na hatimaye kuupigia kura na huo ndio utakuwa mwisho wa maadhimisho ya utangulizi wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, lakini jioni, vijana watatembelea Castel Gandolfo, Ikulu ndogo ya zamani, ambayo sasa ni Jumba la Makumbusho ya Vatican na baadaye wamealikwa kwa chakula cha jioni, kilichoandaliwa na Jimbo Katoliki la Albano, nje kidogo ya Roma. Jumapili ya Matawi, tarehe 25 Machi 2018, Kanisa litaadhimisha Siku ya 33 ya Vijana Duniani ambayo kwa mwaka huu inaadhimishwa katika ngazi ya Kijimbo kwa kuongozwa na kauli mbiu “Usiogope Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu” Lk. 1:30. Vijana kutoka ndani na nje ya Roma, wataungana na Baba Mtakatifu Francisko kwa ajili ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili ya Matawi, mwanzo wa kumbu kumbu ya: Mateso, kifo na hatimaye, ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.