2018-03-14 09:45:00

Baraza la Makanisa Ulimwenguni: Utume unafumbata sadaka na ushuhuda


Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC., linaloyajumuisha Makanisa wanachama zaidi ya 348, kuanzia tarehe 8-13 Machi 2018; limeadhimisha Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni, uliokuwa ukifanyika kwenye kilima cha Ngurdoto, Jijini Arusha, Tanzania, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Imekuwa ni fursa kwa wajumbe kujikita katika utume wa Biblia; Warsha iliyopania kuwajengea wajumbe uwezo wa kushughulikia changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazojitokeza kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.

Wajumbe wamehimizwa kuwa na mwelekeo mpya, yaani: kutoka katika kinzani na mipasuko na kuanzisha mchakato wa mawazo mapya yanayojikita katika malezi na majiundo makini ya kimisionari tayari kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu! Wajumbe wamepata fursa ya kushiriki katika maadhimisho ya Ibada na Liturujia ya Neno katika Makanisa mbali mbali ya Kikristo yaliyoko Jijini Arusha na hivyo, kupata nafasi ya kuonja jinsi ambavyo Injili ya Kristo inavyoendelea kutamadunishwa katika maisha na tunu msingi za watu!

Wameonja ukakasi na ugumu wanaopambana nao wamisionari katika mchakato mzima wa umwilishaji wa Injili katika mazingira ya watanzania, lakini zaidi Jijini, Arusha. Askofu Julius J. Laizer wa Kanisa la Kitume la Naivera amewaalika wajumbe kupanda miti kuzunguka eneo la Kanisa lake, kama kumbu kumbu endelevu ya mkutano wa uinjilishaji ulimwenguni uliokuwa unafanyika Jijiji, Arusha. Wajumbe wameshuhudia pia mchakato wa uinjilishaji wa kina unaotekelezwa kwenye Parokia ya “Tokeo la Bwana, Burka”, Jimbo kuu la Arusha, kwa kujikita katika shughuli mbali mbali zinazopania kuboresha hali ya maisha ya waamini na wananchi katika ujumla wake. Padre Peter Pinto anasema, Parokia yake inatoa huduma ya maisha ya kiroho, yaani: maadhimisho ya Ibada na Sakramenti za Kanisa; huduma ya afya, elimu, mikopo nafuu na michezo kwa vijana wa kizazi kipya. Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki nchini Tanzania linaadhimisha Jubilei ya miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara inayoongozwa na kauli mbiu “Jubilei ya Miaka 150 ya uinjilishaji, Furaha ya Injili.”

Wajumbe wote wa mkutano wa uinjilishaji ulimwenguni wameshiriki katika Ibada iliyoongozwa kwenye Kanisa la Kiorthodox, Jijini, Arusha lililoanzishwa kunako mwaka 1953 na kwa sasa linaendelea na utume wake katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina hususan katika sekta ya elimu, ili kuwajengea wanafunzi uwezo mkubwa wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Askofu mkuu Fredrick Onael Shoo amesema, utume wa kwanza kabisa wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Kaskazini mwa Tanzania ulianzishwa kunako mwaka 1893 huko Nkwarungo Kusirye-U. Leo hii licha ya kutoa huduma ya maisha ya kiroho, lakini pia linatoa huduma ya elimu, afya pamoja na kuendesha Kituo cha Watoto Yatima. Dr. Olv Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, WCC anawapongeza waamini wa Kanisa la Kiinjili la Kiluteri Tanzania kwa kuwa mstari wa mbele katika kutunza vyema mazingira nyumba ya wote! Wamekumbushwa kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, utofauti wao ni utajiri na zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu! Kumbe, kwa pamoja wanayo dhamana na wajibu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira, kielelezo cha kazi ya uumbaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.