2018-03-12 09:23:00

Papa Francisko: Maskini ni amana na utajiri wa Jumuiya ya Mt. Egidio


Professa Andrea Riccardi, akiwa kijana mbichi bado, hapo tarehe 7 Februari 1968 alianzisha Jumuiya ya Mtakatifu Egidio yenye Makao yake Makuu mjini Roma na kujikita katika  mambo makuu matatu yaani: Sala, Maskini na Amani duniani. Kanisa kuu la Bikira Maria wa Trastevere yakawa ni makao makuu ya sala, maisha na utume wao sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, inapaswa sasa kujielekeza zaidi katika kuendeleza karama yake bila wasi wasi wala hofu; daima ikishirikiana na Mama Kanisa kwa ajili ya kutafuta na kudumisha Injili ya amani duniani.

Huu ni mchakato unaopaswa kujikita kwa namna ya pekee kabisa katika Tafakari ya Neno la Mungu na kuendelea kusoma alama za nyakati ili kukuza na kudumisha utandawazi wa mshikamano na maisha ya kiroho unaofumbatwa katika mtazamo wa Uso wa huruma. Jumuiya hii inapaswa kuwa na ari na mwamko mpya zaidi wa Kiinjili ili kukabiliana na changamoto mamboleo, kwa kuwa na moyo wazi kwa wote bila ubaguzi kwa kisingizio cha uadui, ili kuendeleza maisha hadi kufikia utimilifu wake! Huu ni muhtasari wa hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 11 Machi 2018 kama sehemu ya mwendelezo wa Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, ambayo imeenea sehemu mbali mbali za dunia.

Baba Mtakatifu anapenda kukazia tena na tena karama ya Jumuiya ya Mtakatifu Egidio inayofumbatwa katika: Sala, Maskini na Amani; karama ambayo imeendelea kukua na kukomaa katika kipindi cha miaka hamsini iliyopita. Changamoto iliyoko mbele yake kwa wakati huu ni kuhakikisha kwamba, wanaiwekeza ili iweze kuzaa matunda mengi zaidi ili kung’oa hofu, mashaka na hasira dhidi ya wahamiaji na wageni, maskini na watu ambao wanaotofautiana nao kwa sababu mbali mbali. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iwe ni mahali pa kukuza na kudumisha karama hizi kwa ajili ya kuendeleza maisha.

Wanachama wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio wanapaswa kutambua kwamba, safari ya maisha na utume wao kwa siku za usoni inaambatana na Kanisa, kama sehemu ya mchakato wa mwendelezo wa matunda ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Mababa wa Mtaguso wanakaza kusema, ilimpendeza Mwenyezi Mungu kuwatakatifuza na kuwaokoa watu, siyo mmoja mmoja na pasipo muungano kati yao, bali kwa kuwaunda kama taifa moja, lenye kumjua katika ukweli na kumtumikia kitakatifu. Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ni matunda ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican yanayojikita katika ujumbe na roho yake!

Baba Mtakatifu Francisko ameipongeza Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa kusali na kuwahudumia wananchi wanaoteseka kutokana na vita sehemu mbali mbali za dunia, lakini kwa namna ya pekee kabisa wananchi kutoka Siria. Baadhi ya waathirika wa vita kutoa Siria wamefanikiwa kuingia na kupata hifadhi nchini Italia kutokana na juhudi za Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kwa kutumia “Njia ya ubinadamu”. Hata baada ya Jumuiya ya Kimataifa kuona athari za vita zilizojitokeza katika karne ya ishirini, lakini bado inaendelea kutumbukia katika mantiki ya vita. Neno la Mungu ni mwanga katika giza; linatoa matumaini ya amani pamoja na kuwasaidia waamini kuendelea kujiamini bila woga hata kama wanapambana na nguvu za giza.

Neno la Mungu linapaswa kuwa ni dira, mwongozo na taa inayoangazia mapito yao, kwa kuwalinda dhidi ya vishawishi vya sera na mikakati mamboleo; Neno la Mungu limewaokoa kutoka katika hofu na mashaka, kumbe, Jumuiya ijitahidi daima kupenda: kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika maisha na utume wake. Neno la Mungu ni chemchemi ya huruma na faraja kwa maskini, wahanga wa vita na majeruhi katika maisha! Neno la Mungu liwasaidie wanajumuiya kusonga mbele kwa imani na matumaini, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati, tayari kumwilisha imani katika matendo, changamoto na mwaliko kutoka kwa Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iwe ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini; na kwamba, kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani na uhasama. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi. Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao.

Baba Mtakatifu Francisko anaitaka Jumuiya ya Mtakatifu Egidio kuadhimisha Jubilei ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwake kwa moyo wa Kikristo zaidi, kwa kujikita katika imani inayomwilishwa katika ari na mwamko mpya wa Kiinjili, kwa kuwa na ujasiri na uvumilivu endelevu katika utekelezaji wa utume wake sehemu mbali mbali za dunia. Jumuiya iwe ni na huruma kwa waathirika wa vita pamoja na mabadiliko ya tabianchi ili kweli, Injili iwe ni mwandani wa maskini, tayari kuvunjilia mbali kuta za utengano, ili kujenga madaraja ya kuwakutanisha na kuwaunganisha watu mbali mbali!

Jumuiya ya Mtakatifu Egidio iendelee kushikamana na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa kuwapatia nafasi ya kwenda katika shule ya amani! Wawe karibu sana na wazee wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, lakini kwao wawe ni marafiki bila kusawahau waathirika wa vita, njaa na magonjwa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, maskini wawe ni amana na utajiri wa Jumuiya ya Mtakatifu Egidio, kwani wote ni wa Kristo, dira na mwongozo wa kuyaangalia ya mbeleni kwa ari na moyo mkuu, wakijitahidi kudumu katika sala, huduma kwa maskini pamoja na kutafuta ili hatimaye kuendeleza amani duniani! Kwa mtindo huu wa maisha, kwa hakika, Mwenyezi Mungu ataendelea kuambatana nao katika hija ya maisha yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.