2018-03-12 10:16:00

Miaka 5 tangu Papa Francisko achaguliwe kuliongoza Kanisa Katoliki!


Familia ya Mungu nchini Poland, Jumapili tarehe 11 Machi 2018 imeungana kwa pamoja kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha kumbu kumbu ya miaka mitano tangu alipochaguliwa kuliongaza Kanisa Katoliki.  Askofu mkuu Stanislaw Gadecki, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland anasema, wameamua kutekeleza kwa vitendo, ombi linalotolewa mara kwa mara na Baba Mtakatifu Francisko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kumkumbuka kwa sala na sadaka yao, katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Muasisi wa wazo hili ni Rafal Orzechowski, mwanachama wa chama cha utume wa sala cha “Lednica” huko Grayewo, nchini Poland ambaye alibahatika kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ta Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2017, huko Poland. Baba Mtakatifu alimhakikishia kwamba, angemkumbuka katika sala na sadaka yake, kwa masharti kwamba, hata yeye katika utume wake wa sala, aendelee kumkumbuka na kumwombea. Tangu wakati huo, Rafal Orzechowski ameendelea kusali kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Baba Mtakatifu, lakini wakati huu, ameamua kuishirikisha familia ya Mungu nchini Poland, kwani “kizuri unakula na ndugu zako.”

Askofu mkuu Stanislaw Gadecki, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Poland anakaza kusema, huu ni mwaliko endelevu wa sala na sadaka kwa ajili ya Baba Mtakatifu Francisko, kwa kukumbuka kwamba, ilikuwa ni tarehe 13 Machi 2013 alipoteuliwa na Baraza la Makardinali kuliongoza Kanisa Katoliki akaamua kujikita katika mambo makuu matatu: Amani, Maskini na Mazingira! Hivi ni kati ya vipaumbele vya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro katika kipindi cha miaka mitano ya utume wake.

Baraza la Maaskofu Katoliki, litakusanyika kusali kwa pamoja, siku hii, kwa kuwaunganisha wakleri, watawa na waamini walei kutoka sehemu mbali mbali za Poland, ili kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa uwepo na utume wa Baba Mtakatifu Francisko, ambaye anaendelea kukabiliana na changamoto mbali mbali, ili asikate tamaa, bali atambue kwamba, sala za familia ya Mungu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, zinamsindikiza katika maisha na utume wake, ili aendelee kuwa ni kiungo cha umoja wa Kanisa, kanuni maadili na utu wema pamoja na upendo miongoni mwa familia ya Mungu. Baraza la Maaskofu Katoliki Poland linasema, kila mtu anaweza kusali mahali popote pale alipo kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko! Hata wewe unaalikwa kuungana na wale wote wanaomwombea! Jaribu nawe utafurahia matokeo yake!

Na Padre Richard Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.