2018-03-10 06:30:00

Kwaresima ni kipindi cha mapambano dhidi ya dhambi na mauti!


Ndugu msomaji na msikilizaji wa Vatican News, karibu katika tafakari ya Neno la Mungu katika Dominika ya nne ya Kwaresima. Hii pia ni dominika inayoitwa dominika ya furaha (laetare) kwa sababu inawaalika waamini kuoona Kipindi cha Kwaresima ambacho sasa kimefikia nusu ya kipindi chake, kuwa pia ni kipindi cha furaha na hivi kuwatia moyo kuendelea kwa furaha kufunga, kusali, kufanya toba na kuwasaidia wahitaji.

Masomo kwa kifupi: Somo la kwanza (2Nyak. 36, 14-16. 19-23). Kitabu cha Mambo ya Nyakati  ni kitabu kinachoiangalia upya historia ya taifa teule, Israeli, na kuitafasiri katika mwanga wa Agano. Na kwa ujumla wake kinaonesha kuwa katika historia ya waisraeli kwenye safari ya ukombozi, pale walipoishi kiaminifu katika Agano walifurahia nyakati za amani na ustawi na pale ambapo walikiuka agano walipitishwa katika nyakati ngumu. Somo la leo linaendelea wazo hili. Linachukua tukio la Waisraeli kupelekwa utumwani Babeli na kuonesha kuwa ni matokeo ya makosa ya mtawala wao aliyeitwa Zedekia pamoja na makosa ya wakuu wa makuhani na watu wote dhidi ya Agano. Yanatajwa makosa mawili; kwanza ni kufanya machukizo mbele ya Bwana na pili ni kutokusikiliza sauti ya nabii wa Mungu iliyowaita watubu, wamgeukie Bwana. Wakakaa na shingo ngumu na hawakutubu.

Wakiwa katika kipindi hicho kigumu, kwa kinywa cha nabii Yeremia unatoka unabii unaowaonesha wamerejeshwa kwao toka utumwani. Huu ni unabii unaoonesha kwao kuwa tayari Mungu amekwishafungua mlango wa msamaha endapo watatambua makosa yao na kurudi kwake kwa kufanya toba. Somo la pili (Ef 2, 4-10) Mtume Paulo anazungumza juu ya uhusiano uliopo kati ya dhambi, kifo na neema ya Mungu. Mtume Paulo anasisitiza kuwa dhambi huleta kifo, na ndivyo ilivyokuwa. Kiroho amekufa. Katika umauti huo, ni Kristo aliyemkomboa mwanadamu. Na hapa Mtume Paulo anakazia kuwa kazi hiyo ya ukombozi aliyoifanya Kristo, kwa mwanadamu ni zao la neema tu kwa maana kwamba mwanadamu amejaliwa bila mastahili yake. Kama mwanadamu alivyokuwa amekufa kwa dhambi hapo awali, hata sasa anayeishi katika dhambi amekufa kiroho. Anahitaji neema ya ukombozi, ndiyo imani na wongofu kwake Kristo Bwana wetu.

Somo la Injili (Yoh. 3,14-21) ni mazungumzo kati ya Yesu na kiongozi mmoja wa dini ya kiyahudi aliyeitwa Nikodemo. Injili ya leo inaleta sehemu ya mazungumzo hayo marefu ambapo Yesu analinganisha tukio la Musa kumwinua nyoka wa shaba jangwani na tukio linalokuja la yeye kuangikwa msalabani. Maneno yanayotumika ni kuinuliwa na kutukuzwa, ambayo ni maneno Yesu anayotumia mara kwa mara kuashiria kifo chake msalabani “saa ya kutukuzwa mwana wa Adamu ... nk). Ni kutukuzwa huku ndio sababu ya yeye kuja ulimwenguni ili kama vile nyakati za Musa wale walioangalia nyoka wa shaba walipona kutoka sumu ya nyoka basi hata sasa wale wanaomwangalia msalabani kwa jicho la imani wapone kutoka katika sumu ya ibilisi ambayo ni giza la maisha ya dhambi. Kwa maana kama anavyozidi kueleza waliompokea na wanaoendelea kumpokea yeye wapo kwenye mwanga bali wasiompokea wapo katika giza.

Tafakari: Katika ujumla wake, maandiko matakatifu dominika ya leo yanagusa kipengele ambacho kipo katikati ya mapambano yetu ya Kwaresima, kipengele cha dhambi; dhambi kama uhalisia unaoleta giza na mahangaiko katika maisha ya mwanadamu na ambao unapata ukomo katika huruma na upendo wa Mungu. Masomo haya yanatukumbusha tena kwa namna inayogusa moja kwa moja kwamba dhambi ipo. Na inajidhihirisha katika namna zifuatazo: Kukiuka Agano: katika teolojia ya Agano la Kale ambayo inajionesha katika somo la kwanza leo, dhambi inaongelewa kama kukiuka Agano ambalo Mungu ameliweka na wanadamu. Ndio kusema kukiuka amri zake kumi na kukiuka miongozo yake inayotufikia kwa namna mbalimbali. Ndiyo kukiuka ahadi zetu za ubatizo, kukiuka maagano ya ndoa, kukiuka nadhiri na ahadi za maisha ya wakfu, kukiuka maelekezo na msisitizo wa dhamiri zetu na kadhalika.

Kukataa wongofu: mara nyingi tunaposikia neno wongofu huwa tunafikiria kwanza wale ambao sio wakristo kuipokea imani ya kikristo. Katika undani wake, wongofu ni kugeuka kutoka maisha ya dhambi kuelelekea maisha ya neema iwe ni kwa aliyekwishaipokea imani ya kikristo au kwa ambaye hajaipokea. Kati ya makosa mawili ya Zedekia (somo la kwanza) lilikuwa ni kosa la kutokukubali kuongoka licha ya kutumiwa manabii na Mwenyezi Mungu. hata kwetu leo, pale tunapokataa kusikiliza sauti na maonyo ya Mungu yanayotufikia kwa njia mbalimbali na hasa kwa njia ya Kanisa, ni kielelezo cha dhambi. Kukataa wongofu kunaweza kusababishwa na ugumu wa moyo, hofu ya kubadilika, kukata tamaa lakini hata uzembe wa kiroho kuwa muda bado upo nitajirekebisha tu siku zijazo. Hiki ni kielelezo cha dhambi.

Uchaguzi mbaya: lugha ya kibiblia “giza na mwanga” inaashiria pia nafasi ya uchaguzi aliyonayo mwanadamu katika maisha yake. Waswahili husema kupanga ni kuchagua. Mwanadamu yuko huru kuchagua mfumo wa maisha, mwenendo na njia inayofaa. Ni muhimu kutambua kuwa katika kila anachochagua atawajibika nacho na ni muhimu pia kutambuka kuwa kila anachochagua kina matokeo yake - mazuri au mabaya. Maandiko Matakatifu leo yanatuambia kuwa pamoja na Kristo kuja ulimwenguni na kuleta mwanga wa maisha ya neema, kwa bahati mbaya wapo ambao bado wanachagua giza badala ya mwanga huo. Kuchagua giza, yaani kuchagua kubaki nje ya Kristo, ni kielelezo cha dhambi. Vielelezo hivi vya dhambi vinaletwa kwetu leo ili vitusaidie kujitathmini, tunapoendelea na kipindi hiki cha kwaresima, kipindi cha mapambano dhidi ya dhambi, tuweze kutambua namna mbalimbali ambazo dhambi inaweza kujidhihirisha katika maisha yetu na hivi kwa msaada wa Mungu tuweze kuishinda.

Neema na Huruma ya Mungu ambayo hata leo imesikika katika masomo, daima hufunua sura mpya kwetu kila tunapoisikia. Kama anavyosema Mtume Paulo pale dhambi ilipozidi ulimwenguni ndipo neema ilizidi kuongezeka. Tumeona katika somo la kwanza, tukio la uasi wa waisraeli na kupelekwa kwao utumwani linaweka katika wakati mmoja na unabii wa kurejeshwa tena nyumbani, ndiyo alama ya msamaha na kurudishiwa hadhi ya wana wa Mungu. Hii inatufundisha kuwa machoni pa Mungu mdhambi amekwisha wekewa tayari wazi mlango wa huruma na msamaha muda ule ule anapoingia dhambini. Ni yeye tu kuzingatia, kujuta na kutubu na msamaha huo utakuwa wake. Basi hima tusikae muda mrefu katika dhambi, tusifanye migumu mioyo yetu bali tuisikie sauti ya Bwana, sauti ya huruma na neema isiyofurahia kifo cha mdhambi bali inayofurahia kurudi kwake na kupata neema.

Bikira Maria Mama wa huruma, atuombee daima.

Padre William Bahitwa.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.