2018-03-09 14:55:00

Mapadre waungamishaji ninyi ni vyombo, sikilizeni na toeni mang'amuzi


Sakramenti ya upatanisho ni muhimu sana kwa maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapojiandaa kwa ajili ya kuadhimisha Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, inayoongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya miito” na utangulizi wake kuanza kutimua vumbi tarehe 19 Machi hadi Jumapili ya Matawi, Kanisa linapoadhimisha Siku ya Vijana Kimataifa, lakini katika ngazi ya kijimbo! Hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa, tarehe 9 Machi 2018 wakati alipokutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na Majandokasisi wanaojiandaa katika maisha na utume wa Upadre, waliokuwa wanashiriki katika mafunzo ya ndani yaliyoandaliwa na Idara ya Toba ya Kitume kuanzia tarehe 5 – 9 Machi, 2018 kwa kutambua kwamba, Sakramenti ya Upatanisho ni kiini cha maisha na utume wa Mapadre.

Hawa ni mapadre vijana kwa ajili ya vijana wenzao wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na kwamba, kutokana na umri wao kuwa karibu, wanaweza kuwa ni vyombo na mashuhuda wazuri wa majadiliano na vijana wenzao katika mchakato wa ujenzi wa utu na wito wa Kikristo. Lakini, mapadre vijana watambue udhaifu na vikwazo vinavyoweza kujitokeza wanapokuwa wanatekeleza dhamana na wajibu wao, changamoto kwa mapadre vijana ni kuendelea kujizatiti katika kujipatia uzoefu na mang’amuzi ya huduma ya upatanisho, yanayofumbatwa kwa kuwasikiliza waamini kwa muda mrefu zaidi.

Baba Mtakatufu Francisko anawataka mapadre waungamishaji kujenga na kudumisha utamaduni na sanaa ya kusikiliza kwa makini, hasa vijana wanaokimbilia kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu. Kama anavyokaza kusema, mapadre waungamishaji watambue kwamba, wao ni vyombo vya huruma ya Mungu na kumbe, wasiwe ni wamiliki wa “dhamiri ya waamini” wanaokimbilia huruma na upendo wa Mungu katika Sakramenti ya Upatanisho. Watambue kwamba, wanapojenga mahusiano na vijana, wao bado wanajenga, wanalea na kutaka kuimarisha utu wao, kumbe wanaweza kuathirika sana!

Mapadre waungamishaji ni vyombo vya upatanisho unaowataka kuwa wanyenyekevu kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu anayewawezesha kufanya mang’amuzi. Kama vyombo vya upatanisho wanatekeleza kwa ukamilifu utume mintarafu utume wa Kristo Kuhani Mkuu, wakitambua kwamba, wao kwa hakika ni “watumishi wasiokuwa na faida”! Mapadre waungamishi wajenge sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini maswali na dukuduku ya waungamaji kabla ya kukimbilia kutoa majibu. Bila kuwahamasisha vijana kuuliza maswali msingi, mapadre waungamishaji wanaweza kupoteza dira na mwelekeo wa utume wao. Wanaitwa kwanza kabisa: kuwa ni watu wanaosikiliza kwa makini waungamaji wanaokuja mbele yao katika ubinadamu wao; pili, kuwa wasikivu pia kwa Roho Mtakatifu. 

Mambo haya msingi yanawawezesha mapadre waungamishaji kuwa na mang’amuzi ya wito yanayoweza kuwapatia vijana nafasi ya kusikiliza suati ya Mungu katika maisha yao; Mungu anayezungumza kutoka katika undani wa dhamiri zao nyofu na kwa njia ya Neno lake. Mambo haya yatawasaidia vijana kuanza hija ya wito wao, kwa kusoma alama za nyakati zinazojitokeza katika maisha ya vijana; kwa kuangalia karama, mapaji, ubora bila kusahau matamanio halali ya ujana wake. Kwa njia ya matukio mbali mbali katika maisha; kwa sala endelevu hata vijana wa kizazi kipya wanaweza kusema, “Sema Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia”.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, kwa njia hii, Mahakama ya huruma ya Mungu inakuwa ni fursa makini ya kukutana mwamini na padre muungamishaji, hata kama kila mtu ana mwelekeo tofauti wa wito wake. Wito unaibuliwa na kujengwa katika mahusiano ya dhati kabisa na Kristo Yesu. Kwa njia hii, padre muungamishaji anakuwa ni daktari wa maisha ya kiroho na hakimu wa huruma ya Mungu; anakuwa ni mchungaji na baba wa maisha ya kiroho; anakuwa kwa hakika anasema Baba Mtakatifu mwalimu na mlezi.

Padre muungamishaji anapaswa kuwa ni shuhuda anayejisadaka kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za ndugu zake katika Kristo Yesu. Wawe ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kama unavyojidhihirisha katika mfano wa Baba mwenye huruma kwa Mwana mpotevu aliyetubu dhambi zake na kuamua kurejea tena nyumbani kwa Baba yake. Padre muungamishaji ni shuhuda wa uzoefu wa huruma ya Mungu ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwapatia waja wake. Kutokana na changamoto zote hizi, Baba Mtakatifu Francisko mwishoni, anawataka mapadre na waungamishaji watarajiwa kuwa ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu; wanyenyekevu na wasikivu wa vijana na mapenzi ya Mungu katika maisha yao; kwa kuheshimu dhamiri na uhuru wa waamini wanaokimbilia kwenye Mahakama ya huruma na upendo wa Mungu, kwani Mungu anapenda na kuthamini uhuru wao. Daima wapende kuwaaminisha waamini wanaotubu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, kimbilio la wakosefu na Mama wa huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.