2018-03-09 17:08:00

Huruma ya Mungu ni muhtasari wa historia ya ukombozi!


Historia ya Mungu juu ya wokovu wa mwanadamu inaonekana wazi hapa. Tunapata nafasi ya kuona Musa na wana wa Israeli na uhusiano wao na Mungu ulivyokuwa. Katika Hes. 21: 1-9 – tunapata kusikia habari juu ya nyoka wa shaba, alama ya wokovu. Hapa Mungu anatanguliza alama za wokovu watakaopewa wale watakaomtazama. Tunaona Waisraeli walivunja agano, hivyo wakaadhibiwa. Ila walipotambua kosa lao, wakafanya toba, wakapata uzima. Uzima wa kweli hupatikana kwa kumtazama Mungu wa kweli. Katika somo la Injili – Yesu anainuliwa juu na wote watakaomwangalia, watapata uzima wa milele. Yesu ni mwana wa mtu. Nabii Dan. 7: 13-14 – katika Agano la Kale anaweza kuuona ujio wa utukufu wa Mungu. Mungu aliahidi kuutoa ufalme kwa yule ambaye watu na mataifa wamwangalia na kumtumikia. Ndicho ambacho Mungu atualika leo kutazama na kuona hata kwa macho yetu. Kile ambacho nabii amekiona katika maono, twaweza kukiona kwa macho yetu leo na kukitangaza.

Hapa tunaona wazi wazi Yohane anatanguliza hali ya utukufu wa Kristo mfufuka – ameinuliwa, akafufuka na akapaa – Yoh. 8:28 na 12:32. Ni safari toka chini kwenda juu. Ndiyo matokeo tunayoyatazamia pia sisi. Kushiriki utukufu wa Kristo mfufuka. Hivyo tunaalikwa kuamini na kuamini ni kuishi upendo, huu ni uzima, uzima wa ufufuko. Je, sisi tuko katika mpango huu? Mungu anapenda, Yesu anaokoa na Roho Mtakatifu anafundisha. Tunaalikwa tuingie katika huu mpango wa wokovu wa Mungu. Pia tunaalikwa tufurahi kwa sababu ya upendo wa Mungu kwetu sisi. Tunaambiwa hivi leo katikati ya kipindi cha kwaresima. Kwa nini? Upendo wa Mungu maana yake ni nini? Upendo wa Mungu ni upendo unaotoa - Agape. Ni upendo wa kisadaka. Alijitoa kwetu. Mungu anatoa na anasamehe. Upendo huu ukikosekana basi ni kifo.

Hebu tutafakarishwe na mfano huu ili utusaidie kuona jinsi upendo wa Mungu unavyookoa. Mhubiri maarufu – Padre Munachi anatoa mfano huu – mtakatifu mmoja alimwomba Mungu amwoneshe tofauti kati ya mbingu na motoni. Mungu akamtuma malaika na akaanza kwa kumwonesha kwanza motoni. Akaona wanawake na wanaume wengi wameketi kuzunguka meza kubwa na juu ya meza palikuwa na aina mbalimbali za vyakula vizuri na vitamu. Ila hakuna hata mmoja aliyekuwa anakula. Wote walikuwa na huzuni kubwa na kulalamika. Wote wamekondeana. Yule mtakatifu akamwuliza mmoja wao – mbona hamli chakula? Akamwonesha mkono wake. Kumbe, walikuwa wameshika kijiko kirefu kuliko mikono yao. Na kwa sababu ya uchoyo wao na kukosa upendo kati yao, kila mmoja alikuwa anakazana kujilisha mwenyewe.

Kwa maana hiyo hata kama akichota chakula hataweza kukipeleka mdomoni. Kwa sababu ya urefu wa kijiko kile chakula chote humwagika chini. Hakuwepo aliyekuwa tayari kumlisha mwenzake. Halafu malaika akamchukua mbinguni na akakuta wanaume na wanawake wengi na meza na vyakula. Tofauti kubwa ni kuwa wale walikuwa na furaha kuu na vicheko. Kila mmoja alikuwa na kijiko kirefu vile vile. Wote wamenenepeana. Akamwuliza mmoja wao chanzo cha furaha yao. Akapata jibu kwamba kila anayechota chakula humlisha mwenzake. Upendo umetawala kati yao. Ndiyo sababu ya furaha yao na uchangamfu wao. Ndugu zangu, leo kanisa latualika kutafakari upendo wa Mungu kwa ulimwengu na kufurahi. Upendo wa Mungu ambao huonekana ndani ya mwanae. Ili kujibu upendo huu ni lazima kuamini pendo la Mungu lililomiminwa kwetu, kulikubali na kuliishi kama Mtakatifu Yohane asemavyo – sisi tumelifahamu na kuliamini.

Tumsifu Yesu Kristo.

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.

 
All the contents on this site are copyrighted ©.