2018-03-07 14:30:00

WCC: Utunzaji bora wa mazingira ni wajibu wa wote kimaadili!


Baraza la Makanisa Ulimwenguni linaadhimisha Mkutano mkuu wa Uinjilishaji Ulimwenguni, unaofanyika Jijini Arusha, Tanzania, kuanzia tarehe 8-13 Machi 2018; kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kutembea katika Roho: tunaitwa kuwa wafuasi wanaobadilika”. Huu ni mkutano unaoyashirikisha kwa namna ya pekee kabisa, Makanisa Barani Afrika, kama wenyeji wa mkutano huu wa kimataifa, unaofanyika wakati huu, ambapo kuna utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, ambayo wakati mwingine yanatishia misingi ya haki, amani, maridhiano pamoja na utunzaji bora wa nyumba ya wote.

Bwana Ernst M. Conradie kama sehemu ya tafakari yake kwa ajili ya maadhimisho ya mkutano huu anasema, athari za mabadiliko ya tabianchi zimechangia kwa kiasi kikubwa: maafa, umaskini na majanga katika maisha ya watu! Hiki ni kikwazo kikuu cha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Hii ni changamoto ambayo imevaliwa njuga na Shirikisho la Mabaraza ya Makanisa Kusini mwa Afrika, “South African Council of Churches, SACC”. Makanisa yaliichukua changamoto hii ili kuifanyia kazi kama sehemu ya tafakari inayoweza kubadilisha mtindo wa maisha ya waamini kwa kufanya toba na wongofu wa kiekolojia, ili kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote!

Mapambano dhidi ya umaskini, ujinga, magonjwa na ukosefu wa ajira hayana budi kwenda sanjari na mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Kuna baadhi ya mashirika na makampuni makubwa ya kitaifa na kimataifa yanayofaidika sana kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kumbe, hayatakuwa tayari kuhakikisha kwamba, Bara la Afrika linapata teknolojia rafiki ili kupunguza hewa ya ukaa inayochafua mazingira kwa kiasi kikubwa na hivyo kuwatumbukiza watu wengi zaidi katika umaskini wa hali na kipato! Kipaumbele chao kitakuwa ni demokrasia, kinzani na mipasuko ya kijamii; haya si mambo msingi. Uchafuzi wa mazingira anasema Ernst M. Conradie  unafifisha uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma kwa jamii; unahatarisha misingi ya haki, amani na maridhiano na kwamba, rasilimali za nchi zinakwapuliwa bila utaratibu na matokeo yake ni madhara makubwa kwa siku za usoni. Haki jamii ni muhimu sana katika kujenga na kudumisha mafungamano ya kijamii katika medani mbali mbali za maisha.

Rasilimali na utajiri wa nchi vinapaswa kutumiwa vyema kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuliko mtindo wa sasa ambao sehemu kubwa ya utajiri na rasilimali za dunia zinamilikiwa na watu wachache ndani ya jamii kwa ajili ya mafao yao binafsi! Uchafuzi wa mazingira ni suala la kimaadili linalopaswa kuvaliwa njuga na waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema. Haya ni mapambano endelevu kama ilivyo kwa janga la Ukimwi na balaa la njaa duniani. Hapa kunahitajika wongofu wa kiekolojia, uthabiti wa kanuni maadili na utu wema na ujasiri unaomwilishwa katika uongozi bora unaozingatia sheria, kanuni na taratibu. Lengo ni kudumisha misingi ya haki, amani na mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu yanayofumbatwa katika upatanisho na haki msingi za binadamu. Haki na amani ni kati ya vipaumbele vinavyopaswa kutolewa na familia ya Mungu Barani Afrika.

Jumuiya ya Kimataifa tarehe 22 Aprili 2016 kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani iliweka sahihi kwenye makubaliano ya
itifaki ya kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi, matokeo ya mkutano kuhusu athari za mabadiliko ya tabianchi uliofanyika Jijini Paris, Ufaransa. Kumbe, mchakato wa haki, amani, upatanisho na maridhiano hauna budi kuvaliwa njuga na Jumuiya ya Kimataifa kwani hakuna nchi ambayo inaweza kuishi peke peke kama kisiwa! Utawala bora, mabadiliko ya mtindo wa maisha ni mambo msingi katika kudumisha mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.