2018-03-07 15:04:00

Wananchi zaidi ya 270, 000 Papua New Guinea wanahitaji msaada!


Tetemeko la ardhi lililoikumba Papua New Guinea hivi karibuni limesababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Zaidi ya watu 270, 000 wanahitaji msaada wa dharura. Tetemeko hili limesababisha uharibifu mkubwa wa miundo mbinu kiasi kwamba walau asilimia 65% za majengo ya afya na shule yameharibiwa vibaya sana. Serikali inaangalia uwezekano wa kufuta mwaka wa masomo nchini humo kutokana na ukosefu wa miundo mbinu.

Baba Mtakatifu Francisko kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya watu hawa, katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, katibu mkuu wa Vatican kwenda Papua New Guinea anasema, anapenda kuwaweka mikononi mwa huruma ya Mungu, wananchi wote waliopoteza maisha yao kutokana na tetemeko hili! Anawaombea wote walioguswa na kutikiswa na tetemeko hili faraja na kwamba, yuko karibu nao kwa njia ya sala na sadaka yake, hasa katika kipindi hiki kigumu. Anawatakia ari na moyo mkuu wale wote wanaoendelea kutoa msaada wa dharura kwa waathirika wa tetemeko hili huko Papua New Guinea.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.