2018-03-06 08:16:00

Wakristo Barani Afrika! Sasa ni zamu yetu kuwa wamisionari!


Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi wangu! Hii ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2018 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara na kilele chake ni hapo tarehe 7 Oktoba 2018. Kanisa nchini Tanzania linafanya kumbu kumbu ya miaka 50 ya Tamko la Maaskofu Katoliki Tanzania kuhusu “Mwelekeo na Hatima ya Tanzania”. Na familia ya Mungu nchini Tanzania inajiandaa kwa ajili ya zoezi la utekelezaji wa demokrasia kama sehemu ya haki msingi za binadamu kwa uchaguzi wa viongozi wa Serikali za mitaa hapo mwaka 2019. Vatican News baada ya kutafakari kuhusu sura ya kwanza, Basi Enendeni, leo inapenda kukushirikisha sura ya pili ya ujumbe huu unaongozwa na kichwa cha maneno “Sasa ni zamu yetu.”

Baba Mtakatifu Paulo VI alipotembelea Uganda mwaka 1969 alilikumbusha Kanisa katika Afrika kwamba wakati umewadia wa kuwa wamisionari baina na miongoni mwetu. Akisemea jambo hilo nchini Uganda, Paulo VI alisema: “Kwa sasa, ninyi Waafrika mu wamisionari baina na miongoni mwenu. Kanisa la Kristo limekwisha pandwa vema na kwa uhakika katika udongo huu uliobarikiwa. ... Kwa maneno mengine, ninyi Waafrika lazima sasa, katika Bara hili, muendeleze ujenzi wa Kanisa... Kanisa kwa maumbile yake daima ni Kanisa la kimisionari”.   .... Hii ni kutaka kusema kwamba hatupaswi kudhani kuwa mmisionari ni mtu anayetoka nje ya nchi kuja kwetu.  Umisionari kwa maana pana ni kumshuhudia Kristo kwa maneno na matendo yetu popote tulipo. 

Umisionari ni kuachana na ubinafsi, ni kukumbuka kuwa popote tulipo tunapaswa kutenda na kunena yale yanayojenga Ufalme wa Mungu na kusaidia kuwafanya watu wengi kuwa wanafunzi wa Kristo.  Kristo anaposema, “Nanyi mtakuwa mashahidi wangu” (Mdo 1:8), anataka kusema kama tumemsikia, kama tumemjua, na zaidi sana kama tunampenda, basi hatuwezi kuacha kumshuhudia kwa wengine.  Moto wa furaha wa kumjua Kristo utatusukuma kuhakikisha tunafanya kila tunavyoweza ili mwana wa mtu atakapokuja akute bado kuna imani duniani (Rej. Lk 18:8)

Jambo hili linadai ujasiri wa imani utokao kwa Roho Mtakatifu.  Ndiyo maana Mitume wa Yesu hata walipokamatwa, kuteswa na kufungwa hawakurudi nyuma: “Hatuwezi kuacha kusema juu ya mambo yale tuliyoyaona na kuyasikia” (Mdo 4:20). Baba Mtakatifu Francisko, katika Waraka wake wa kitume Furaha ya Injili (Evangelii Gaudium, 14), anapendekeza mambo haya yafuatayo yatubidishe: Mosi, Kuwasaidia waamini wakue kiroho ili waweze kupokea upendo wa Mungu kwa utimilifu zaidi katika maisha yao. Pili; Kuwasaidia wabatizwa ambao maisha yao hayaonyeshi wajibu wa ubatizo, ambao hawana uhusiano wa maana na Kanisa na hawapati tena faraja inayotokana na imani. Tatu; Umuhimu wa kuihubiri Injili kwa wale ambao bado hawamtambui Yesu Kristo au daima wamemkataa.

Hii ndiyo namna bora kabisa ya kuwa “katika hali ya umisionari daima” (EG, 25), na ndiyo namna ya kudhirisha kuwa sasa ni zamu yetu nasi kuhubiri yale tuliosikia na kuyaona. Bidii ya kufanya mambo hayo matatu yaliyotajwa na Baba Mtakatifu Fransisko itatuepusha na tabia ya Kaini ambaye hakujali wala hakuona kuwajibika juu ya mustakabari wa ndugu yake Abeli. Hivyo basi, kuwa mmisionari kunahitaji sana moyo wa kujali kabisa hatima ya wokovu ya kila binadamu kwa kumjali katika nyanja zote za maisha yake kiroho, kiakili, kimwili na kijamii. Bila ya kuwa na moyo wa kujali, tutakuwa wakatili kama Kaini alivyokuwa kwa ndugu yake Abeli!

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.