2018-03-05 07:00:00

Wanawake ni majembe ya nguvu katika ujenzi wa Kanisa Amerika ya Kusini


Professa Guzman Carriquiri, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, CAL, anasema, tume yake itakuwa na mkutano wa mwaka kuanzia tarehe 6-9 Machi 2018, hapa mjini Vatican kwa kuongozwa na kauli mbiu “Mwanamke, mhimili wa ujenzi wa Kanisa na Jamii Amerika ya Kusini”. Hii ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati alipokutana na kuzungumza na wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Amerika ya Kusini huko mjini Gogotà wakati wa hija yake ya kitume! Aliwakumbusha kwamba, matumaini ya Amerika ya Kusini yanafumbatwa katika sura ya mwanamke.

Hii ni dhamana nyeti inayolitaka Kanisa na jamii katika ujumla wake, kuhakikisha kwamba, wanawake wanafahamika, wanaheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kushirikishwa katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake, ili waweze kuchangia katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Bila mchango wa wanawake, Kanisa Amerika ya Kusini litapoteza nguvu yake ya kujipyaisha tena. Dhamana na utume wa wanawake ndani ya Kanisa unajidhihirisha wazi kwa njia ya Bikira Maria; Kanisa pamoja na “wanawake wa shoka” ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kuhakikisha kwamba, wanarithisha: imani na tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii kwa watoto wao.

Baba Mtakatifu akiwa nchini Perù alionesha masikitiko yake makubwa kutokana na nyanyaso na dhuluma ambazo wanawake wanakumbana nazo katika maisha na utume wao kutokana na utamaduni wa mfumo dume ambao umepitwa na wakati! Hawa ni wanawake ambao wameendelea kujizatiti katika kulinda na kuzitegemeza familia zao katika huduma ya elimu, afya na ustawi katika ujumla wake. Wanawake bado wanabaguliwa hata katika maeneo ya kazi na kwamba, hawa ndio waathirika wakuu wa balaa la umaskini, mauaji ya wanawake pamoja na nyanyaso ambazo zinakwenda kinyume kabisa cha utu na heshima yao.

Itakumbukwa kwamba, wajumbe wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini, CAL ni: Makardinali na Maaskofu, lakini kwa mwaka huu, Tume imewaalika baadhi ya wanawake kutoka Amerika ya Kusini, wanaotekeleza dhamana na majukumu yao katika medani mbali mbali za maisha kutoa tafakari, uwepo, uzoefu na mang’amuzi yao katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake, kama sehemu ya mchakato wa kutajirisha. Professa Ana Maria Bidegain atapembua kuhusu: vizingiti na nguvu katika kuwaendeleza wanawake kadiri ya mazingira ya Amerika ya Kusini.

Kwa upande wake, Professa Guzman Carriquiri, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini atashirikisha kuhusu wanawake wa shoka walioleta mageuzi na mabadiliko ya kitamaduni huko Amerika ya Kusini. Kardinali Francisco Robles atajikita katika tema ya uwepo wa Bikira Maria; dhamana na nafasi ya wanawake katika mchakato wa uinjilishaji Amerika ya Kusini. Kardinali Marc Ouellet,  Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini atazungumzia kuhusu “Mwanamke mintarafu mwanga wa Fumbo la Utatu Mtakatifu na Kanisa”. Baadaye yatafuatia majadiliano kuhusu ukweli wa maisha ya wanawake kama mihimili ya ujenzi wa Kanisa. Mwishoni mwa mkutano huu, hapo tarehe 9 Machi 2018, wajumbe wanatarajiwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko. Itakumbukwa kwamba, tarehe 8 Machi ni Siku ya Wanawake Duniani, kumbe, wajumbe wa wanawake wanaofanya kazi zao mjini Vatican watapata chakula cha pamoja na washiriki wa mkutano wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya

Amerika ya Kusini. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna wanawake 700 wanaofanya kazi mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.