2018-03-05 10:07:00

Mtumishi wa Mungu Padre Pernet ni shuhuda wa Injili ya upendo!


Baba Mtakatifu Francisko ameandika utangulizi wa kitabu ambacho kimetungwa na Mwandishi wa habari wa Gazeti la “La Stampa” Bi Paola Bergamini kinachosimulia maisha ya Padre Stefano Pernet, muasisi wa Shirika la Masista Wadogo wa Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, aliyetangzwa kuwa Mtumishi wa Mungu na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1983. Historia ya maisha ya Padre Stefano Pernet inafumbatwa katika ushuhuda wa Injili ya upendo inayomwilishwa katika sura za watu mbali mbali kwa njia ya sadaka na majitoleo yao pasi na kikomo. Ni Padre aliyejisadaka kusaidia familia maskini nchini Ufaransa baada ya mapinduzi ya Ufaransa yaliyosababisha mateso na mahangaiko ya watu wengi.

Hii ni sadaka ya maisha ambayo kamwe haiwezi kupimwa kwa mizani ya binadamu, bali ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, mchakato wa uinjilishaji mpya unafumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Huu ni mshikamano wa Injili ya upendo kwa maskini na wagonjwa wanaoteseka: kiroho na kimwili. Padre Stefano Pernet aliwaambia watawa wake, kunako mwaka 1867 kwamba, maskini wanaposhikwa na magonjwa ya: kiroho na kimwili; ni watu wanaotelekezwa kiasi hata cha kukosa msaada wanaohitaji katika maisha yao! Kumbe, watawa wanapaswa kuwa ni Wasamaria wema, wanaojisadaka kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu kama hawa!

Baba Mtakatifu Francisko katika utangulizi wa kitabu hiki, anawataka watawa wa Shirika la Masista Wadogo wa Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni kupiga hatua kubwa zaidi katika maisha na utume wao, daima wakijitahidi kusoma alama za nyakati ilikuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali: Wawaangalie hata wale ambao wamemwasi Mwenyezi Mungu kwa sababu zao binafsi au kwa vile tu walishirikiana na watu waliokengeuka. Hii inatokana na ukweli kwamba, watawa hawa wamejijengea heshima kubwa miongoni mwa watu wa Mungu kutokana na utamaduni wao wa kusikiliza kwa makini na kutenda kadiri ya changamoto za Kiinjili.

Ni kwa njia ya ushuhuda wao, watu wengi wamevutiwa sana na maisha yao, kiasi kwamba, uwepo wao tu unatosha kuleta faraja kwa watu! Ni watawa ambao wamezisaidia familia kuamsha tena ndani mwao ari na moyo wa sala pamoja na kukuza tunu msingi za maisha ya Kikristo! Ni watawa wanaohudumia kwa moyo na unyenyekevu mkuu, kiasi cha kuwasha moto wa upendo kwa wale wote wanaopata huduma yao! Huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu ni kivutio kikuu katika huduma! Huu ndio ushuhuda ambao ni urithi na amana kutoka kwa Mtumishi wa Mungu Padre Stefano Pernet, muasisi wa Shirika la Masista Wadogo wa Bikira Maria Mpalizwa Mbinguni, linaloendeleza ushuhuda huu sehemu mbali mbali za dunia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.