2018-03-02 14:08:00

Vigogo wa sayansi ya afya ya binadamu na watunga sera kukutana Vatican


Baraza la Kipapa la Utamaduni kwa kushirikiana kwa karibu sana na Mfuko wa “Unite To Cure”, pamoja na wadau wengine, kuanzia tarehe 26-28 Aprili 2018, kwa pamoja wataadhimisha mkutano wa nne kimataifa mjini Vatican utakaojikita katika mchakato wa maendeleo ya sayansi na teknolojia inayopania kuboresha afya ya binadamu; kuzuia na kuponya magonjwa; kulinda na kudumisha mazingira bora kwa kuzingatia tamaduni, tunu msingi za maisha ya kiroho na athari zake katika jamii husika! Kauli mbiu ya mkutano huu ni “Mpango mkakati wa maboresho ya huduma ya afya duniani”.

Kwa maneno mengine, hili litakuwa ni Jukwaa la sayansi na teknolojia kwa ajili ya maboresho ya huduma ya afya anasema Dr. Robin Smith, Rais wa Mfuko wa “Unite To Cure”. Ni jukwaa litakalowashirikisha wadau mbali mbali, kama vile: wataalam wa afya, watunga sera na mikakati ya huduma ya afya pamoja na ushuhuda kutoka kwa wagonjwa wenyewe ili kwa pamoja waweze kuibua mbinu mkakati utakaosaidia mchakato wa maboresho ya afya duniani. Lengo ni kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni pamoja na Monsinyo Tomasz Trafny, Afisa mwandamizi wa Idara Sayansi na Imani, Baraza la Kipapa la Utamaduni wanasema, ulimwengu mamboleo unakabiliwa na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia katika tiba ya mwanadamu, hali inayochangia kwa kiasi kikubwa matumaini ya watu kupata huduma bora zaidi, lakini pia wasi wasi na mashaka kuhusu utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maendeleo ya sayansi na teknolojia hayana budi kuzingatia pia kanuni maadili na utu wema, masuala jamii, imani na mapokeo ya watu, ili kweli sayansi iweze kuwa ni kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Tamko la “Gaudium et spes” yaani “Kanisa katika Ulimwengu mamboleo” wanakaza kusema, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa maskini na wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa za wafuasi wa Kristo Yesu pia! Watu wote wanagusa na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Baraza la Kipapa la Utamaduni linajikita zaidi katika kukoleza majadiliano ya kina na wadau mbali mbali katika masuala tamaduni, elimu na sayansi.

Mtakatifu Yohane Paulo II, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na Papa Francisko ni viongozi wa Kanisa wanaoendelea kulihamasisha Kanisa kujikita katika majadiliano na wadau mbali mbali katika: falsafa, sayansi na taalimungu, ili kukoleza majadiliano kati ya imani na sayansi ili hatimaye, waamini waweze kuwa na ufahamu mpana zaidi wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Wawezeshaji wakuu katika mkutano huu watakuwa ni: Meghan McCain, Dr. Sanjay Gupta, Meredith Vieira, DR. Mehmet Oz pamoja na Dr. Max Gomez. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na wajumbe watakaoshiriki katika mkutano huu. Mkutano huu unapania kuwakusanya: wataalam na wanasayansi magwiji kutoka katika sekta ya afya, viongozi wa Serikali, viongozi wa kidini na wanasayansi wagunduzi, wanaoendelea kutoa matumaini kwa maisha bora kwa siku za usoni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.