2018-03-01 13:36:00

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Roho na sadaka ya umisionari


Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka 2018 linagusia maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara na kilele chake kitakuwa ni Jumapili tarehe 7 Oktoba 2018 badala ya tarehe 2 Oktoba 2018 kama ilivyokuwa imetangazwa hapo awali! Vatican News katika sehemu hii ya kwanza, inapenda kukushirikisha roho na sadaka ya umisionari.

Wamisionari waliokuja kuinjilisha Tanzania ya sasa walifika Zanzibar mwaka 1860 wakitokea Jimbo la Reunion. Miaka minane baadae, Wamisionari wa Shirika la Roho Mtakatifu, wakisukumwa na shauku ya kuinjilisha maeneo mapana zaidi, walisafiri kutoka Zanzibar na kutia nanga katika mji wa Bagamoyo mnamo mwaka 1868, ambapo walianzisha jumuiya ya kwanza ya wakristo ambao wengi wao wakiwa ni wale waliokombolewa kutoka utumwani.  Hivi jumuiya hii ya kwanza ya Wakristo ikawa na sifa ya kukombolewa, si tu kiimani, bali hata kijamii.  Hawa walifanywa kuwa watu huru kiroho, kimwili na kiutu. Mwanzo huu wa imani Zanzibar na Bagamoyo umekuwa mlango wa imani kwa maeneo yote ya ukanda huu wa Maziwa Makuu. Kwa upande wao, Wamisionari wa Afrika wlijielekeza maeneo ya Magaharibi ya Tanganyika na kuvuka maziwa yote makuu. Nao Wamisionari Wabenediktini, baadaye, walielekea maeneo ya Kusini mwa Tanganyika. Makundi haya matatu yalifuatiwa na wamisionari wa Mashirika mengine waliosambaa maeneo mbalimbali ya tanganyika.

Roho ya umisionari: Kanisa kwa asili yake ni la kimisionari.  Umisionari ndiyo mtima wa Kanisa, na mmisionari hajitumi bali anatumwa.  Mmisionari wa kwanza ni Bwana Wetu Yesu Kristo. “Kama vile Baba alivyonituma mimi, nami nawatuma ninyi” (Yn 20:21). Kisha wale wote waliomvaa Kristo kwa Ubatizo nao kwa muda wao, hali zao na mazingira yao wanatumwa kuendeleza utume wa Kristo.  Wanatumwa kuujenga Ufalme wa Mungu.  Anayetumwa hapeleki ujumbe wake, haendi kujihubiri mwenyewe, bali anapeleka ujumbe wa yule anayemtuma.  Ujumbe unaobeba utume wetu uko wazi: “Enendeni basi, mkawafanye watu wa mataifa yote wawe wanafunzi wangu” (Mt 28:19).  Sisi tulimpokea Kristo na kufanyika kuwa wanafunzi wake tunatumwa kuwafanya mataifa yote pia kuwa wanafunzi wake.  Bwana Yesu anayetutuma anatuelekeza ni kwa namna gani tunaweza kuutekeleza wajibu na utume huo mkubwa: “Mkiwabatiza kwa jina la Baba, na la Mwana, na la Roho Mtakatifu.  Wafundisheni kuyashika maagizo yote niliyowapeni” (Mt 28:19b-20).

Sadaka ya umisionari: Umisionari ni kutoka: “Enendeni basi”. Bwana wetu Yesu Kristo hakuwaambia mitume wake wakae wangojee watu waje.  Hapana.  Tokeni mkakutane wa watu walipo.  Tendo la kutoka katika mazingira tuliyozoea, hali, maisha na usalama tulionao inadai kuwa tayari kutoa sadaka.  Wamisionari waliokuja kwetu waliacha yote: jamaa, mali, usalama, raha, n.k.; wakaja kukabiliana na adha, magonjwa, hatari na hata kifo kilichotokana na maradhi ya nchi za ukanda wa joto (tropikali), kushambuliwa na wanyama na hata kushambuliwa na maharamia.  Walitoa sadaka kubwa.

Na jambo kubwa ni kwamba walitoa sadaka hiyo kwa furaha.  Ari na kiu yao ilikuwa kutekeleza agizo la Kristo: “Enendeni basi”.  Walitamani kufika hata miisho ya dunia ili kuwafanya watu wamjue, wampende na wamtumikie Mungu na hivi kufanyika kuwa wanafunzi wake.  Ndiyo maana hata pale ambapo wengi wao walipofariki kutokana na adha tulizoona hapo juu, bado wengine walikuja tu kwa furaha bila woga. Kwani katika kujitoa maisha yao kama sadaka walipata faraja ya ahadi ya Kristo kwa wale wote wanaoitikia mwito wa “Enendeni basi!”. Wamisionari hao waliifahamu ahadi ya Kristo na ndiyo maana hiyo ilikuwa faraja yao. Petro anapomwuliza Yesu, “Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata tutapata nini basi?” (Mt 19:27).  Yesu anamjibu akitoa ahadi bora kabisa: Aliyeacha vyote kwa ajili ya jina lake, “atapokea mara mia, na kuurithi uzima wa milele” (Mt. 19:29).

Bwana Yesu anapowatuma wanafunzi wake alipokuwa anakaribia kupaa Mbinguni, aliwaambia, "… enendeni ulimwenguni mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa Jina la Baba na la Mwana na la Roho Mtakatifu, nanyi wafundisheni kuyashika mambo yote niliyowaamuru ninyi. Hakika Mimi niko pamoja nanyi sikuzote, hadi mwisho wa nyakati. Amen” (Mathayo 28:19-20). Maneno haya ya Yesu yanaonesha upendo wa hali ya juu aliokuwa nao Mungu kwa wanadamu, kutupa nafasi ya kuwa wana wa Mungu. Kumfahamu Mungu kwa kuacha njia zetu mbaya. Yesu hakuwaambia wanafunzi wake wasubiri watu wawafuate, ili wapate kuwafundisha na kuwabatiza, lakini aliwaambia wawafuate watu walipo, na kuwafundisha juu ya Ufalme wa Mungu na kuwabatiza katika Utatu Mtakatifu, yaani: Baba, Mwana na Roho Mtakatifu.

Maagizo haya ya Yesu yalifuatwa na kwa sababu hiyo watu wote duniani tumepata kumjua Mungu wa kweli kupitia kwa Mwanae. Bahati kubwa namna gani! Yesu anatutaka wote tupate kuwa wamisionari kwa wenzetu, kwani ijapokuwa tumepata kumjua Mungu,  na kuwa Wakristo, yafaa kujiuliza ni mara ngapi tunamuishi Kristo? Ni mara ngapi tunaonekana kwa watu wengine wasiomjua Kristo bado kuwa sisi tu wana  wa Mungu kwa pendo la kuitwa wana wa Mungu? (1 Yoh 3:1). Mtakatifu Yohane Mwinjili katika Waraka wake wa kwanza kwa watu wote anasema: “Wapenzi, sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa; lakini twajua ya kuwa atakapodhihirishwa, tutafanana naye; kwa maana tutamwona kama alivyo.  Na kila mwenye matumaini haya katika yeye hujitakasa, kama yeye alivyo mtakatifu” (1Yoh 3:2-3).

Ni dhahiri kila mmoja wetu anatamani na kuweka tumaini lake katika kumuona Mungu. Lakini, Je, mara ngapi tunamwona Mungu kupitia ndugu zetu na wale wanaotuzunguka? Je, kumuona Mungu ni Kanisani tu au hata kwenye jamii? Haya ni maswali ambayo kila  mmoja wetu anapaswa kujiuliza. Kazi alizotupa Mungu ni kwa ajili ya utukufu wake. Kazi ni huduma, kwa maana unafanya kazi unayofanya ili kumsaidia mtu mwingine. Je, huyo unayemsaidia anaonja upendo wa Kristo ndani yako?  Anapata kumsifu na kumshukuru Mungu kupitia wewe? Kama jibu ni hapana, basi yafaa kujitafakari kwa upya. Umisionari ni zawadi, ni sadaka ni upendo unaozidi hali yetu  ya kibinadamu. Ni kule kumpendeza Mungu na kutamani kila anayekuzunguka aonje pendo la Mungu. Umisionari wa sasa si kama ule uliokuwa miaka 150 iliyopita, ambapo kuinjilisha ilikuwa ni muhimu na lazima kwani watu hawakuwa wakimjua Mungu wa kweli. Unijilishaji ulifanikiwa, ijapokuwa kwa kukabiliana na changamoto nyingi, kwa ajili ya upendo na ujasiri wa kimungu wamisionari hawa waliokuwa nao. Uinjilishaji mpya leo hii unalenga kuwasaidia Wakristo kuuishi Ukristo kadiri ya mazingira ya leo, na kufanya hivyo kwa matendo, na hivyo kuwa kielelezo cha kweli cha imani.

Na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania.
All the contents on this site are copyrighted ©.