2018-02-27 07:53:00

Watanzania: Uongozi ni huduma na sadaka kwa ajili ya watu wa Mungu!


Padre Nyirenda mara baada ya kuongoza Ibada ya Misa Takatifu Jumapili tarehe 25 Februari 2018, kwa ajili ya Umoja wa Wanafunzi Wakatoliki Watanzania Wanaosoma na kuishi Roma kwenye Kikanisa cha Makao Makuu ya Kanda ya Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia na kukazia umuhimu wa kutakatifuza maadhimisho pamoja na ushiriki wa Mafumbo ya Kanisa, kulifuatia uchaguzi wa viongozi wa Jumuiya ya wanafunzi mjini Roma.  Watanzania wamekumbushwa kwamba, uongozi ni huduma  na sadaka kwa ajili ya watu a Mungu. Ili kuweza kutoa huduma hii kikamilifu, kuna haja ya kubadilika kweli kweli na kuwa kiumbe mpya, ili kutumikia na kuokoa.

Waliochagulia kwa kishindo ni Padre Richard Kashinje, Mwenyekiti; Padre Chrispin Matale, Katibu, Sr. Maria Salome Mwanjala aliyepita bila kupingwa kutokana na huduma kwa watanzania wenzake, Padre Emmanuel Yatera, Liturujia pamoja na Padre Martin Mnyuka, Mkutubi. Tukio hili limehudhuriwa na baadhi ya Mapadre walezi na wakufunzi kutoka Seminari kuu zilizoko nchini Tanzania, ambao wako hapa mjini Roma kwa majiundo endelevu ili kusaidia mchakato wa majiundo kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya Daraja Takatifu kwa ajili ya familia ya Mungu ndani na nje ya Tanzania, wakati huu familia ya Mungu nchini Tanzania inapoadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Ukatoliki Tanzania Bara, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Miaka 150 ya Uinjilishaji, Furaha ya Injili”.

Viongozi waliong’atuka kutoka madarakani wamewashukuru na kuwapongeza walezi wao ambao wamekuwa na mshikamano wa dhati wakati wa raha na shida huku ughaibuni. Kwa namna ya pekee, wamempongeza Padre Dietrich Pendawazima, aliyemaliza uongozi wake kama Makamu mkuu wa Shirika la Wamisionari wa Consolata ambaye kwa sasa amepangiwa utume nchini Argentina kwa moyo wake wa upendo na uzalendo kwa Kanisa na watanzania wenzake. Licha ya majukumu yake mazito, lakini daima alihakikisha kwamba, anakuwepo pamoja na watanzania wenzake, mfano bora wa kuigwa.

Jumuiya ya Watanzania wanaoishi na kusoma Roma, imetumia fursa hii kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteua Askofu mkuu Protase Rugambwa kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu. Hiki ni kielelezo cha heshima na ukomavu wa Kanisa la Tanzania katika kipindi cha miaka 150 ya uwepo na huduma kwa familia ya Mungu ndani nan je ya Tanzania. Wamewashukuru na kuwapongeza Mashemasi, Mapadre na Watawa waliopewa madaraja mbali mbali pamoja na kuweka nadhiri zao za muda na za daima kwa upande wa watawa. Ni Jumuiya ambayo imeonesha umoja, upendo na mshikamano kwa wagonjwa na wale wote waliofikwa na misiba mbali mbali, kielelezo cha umoja na mshikamano wa familia ya Mungu kutoka Tanzania kwani hii ndiyo asili na utambulisho wao, na kamwe usivurugwe na watu wasioitakia Tanzania mema, ustawi na maendeleo endelevu! Umoja na mshikamano wa kitaifa ni utambulisho wa watanzania, kasoro na tofauti ndogo ndogo zinazojitokeza zisivuruge utambulisho huu, unaomezewa mate na watu wengi duniani kama mfano bora wa kuigwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.