2018-02-27 07:11:00

Jumuiya ya Kimataifa ishikamane ili kupambana na changamoto mamboleo


Tunawezaje sasa kujenga maisha ya siku za usoni yenye kukirimiana na kushirikishana, iwapo dunia inaonekana kushamiri kwenye mipasuko na kinzani? Tunawezaje leo kulisha wanyonge na kusimamia wokovu kutoka kwenye baa la njaa, iwapo dunia inayoonekana leo kuwa kama kijiji kufuatia maendeleo ya utandawazi, ndiyo dunia hiyo hiyo inayojidhihirisha kwa mmong’onyoko wa maadili na tunu njema. Maswali haya yanarushwa na Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, katika kuhitimisha Jukwaa la Uchumi na Biashara duniani, Wolrd Economic Forum, lililofanyika hivi karibuni huko Davos, nchini Uswiss, tarehe 22 – 26 Januari 2018.

Maswali haya yamekuwa kama mwiba kwenye miili na mioyo ya washiriki wengi katika Jukwaa hilo, ambalo lilihudhuriwa na viongozi na watendaji wengi wa serikali, siasa, fedha na uchumi, jamii, usalama na dini kutoka sehemu mbali mbali ulimwenguni. Jukwaa hilo limefanyika wakati muafaka, anasema Dr. Olav Fykse Tveit, wakati ambapo dunia inaonekana kuwa na utajiri mkubwa wa kila kitu, lakini wakati huo huo watu wengi sana wanaendelea kuteseka kwa njaa, kiu na umaskini mkubwa sehemu nyingi duniani. Hali hii inashuhudia mgawanyiko, uonevu, nyanyaso na matabaka makubwa yanayotengenezwa na baaadhi ya watu wabinafsi na wanotafuta kujipatia faida kubwa bila kujali wengine, na hivyo kuwa tayari kuwakandamiza wengine kwa kujinufaisha masilahi yao wenyewe.

Takwimu zinaonesha kwamba, mtu mmoja kati ya tisa duniani analala njaa kila siku, na mtu mmoja kati ya watatu anaathirika na utapia mlo. Hii ni kashfa na aibu kwa wale wote wenye nafasi katika serikali na jamii kwa ujumla, ambao wanategemewa kutatua mahangaiko hayo. Ili kuweza kushinda hali hii, ni lazima kusikilizana kwa umakini sana, kuongeza juhudi katika utendaji wa kila mmoja kupiga vita mambo hayo, kuongeza hali ya kujali na kuhurumia wengine na kusaidiana kadiri ya nafasi ya kila mmoja, anasema Dr. Olav Fykse Tveit.

Kwa upande wake Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni, anaahidi kuongeza zaidi juhudi zake za kuwahamasisha makanisa mbali mbali duniani ili kutafakari kwa kina, kujibidiisha na kujitosa kikamilifu katika kukabiliana na changamoto hizo. Juhudi hizo, ziende sambamba na fikra chanya na tafakari ya roho kuhusu sala ya ‘Baba yetu’ ambayo inasaliwa kila siku na waamini wakristo, sababu ule ‘mkate wa kila siku’ ambao wanauomba, lazima uwe ni mkate wa kushirikisha wengine pia wenye mahitaji, na hasa wanaotaabika kwa baa la njaa na umaskini wa kupindukia. Kumbe hili ni jambo la kimaadili na kiroho pia.

Ni kwa mweleko huo, Baraza la Makanisa Ulimwenguni, limekuwa na kampeni kadha wa kadha kama vile ‘chakula kwa ajili ya maisha’ na ‘Amri kumi za lishe’, katika harakati za kuhamasisha jumuiya mbalimbali katika mwanga wa imani, kutetea haki ya lishe, sambamba na haki ya kilimo bora. Pamoja na shughuli hizo, ikumbukwe pia siku ya kuombea utokomezaji wa baa la njaa duniani ambayo kwa mwaka 2017 ilikuwa tarehe 21 Mei. Ni muhimu mshikamano wa dunia nzima kuulizana maswali sahihi na kutafuta suluhu stahiki.

Wakati wa mkutano wa Jukwaa hilo, Baba Mtakatifu francisko alimtua ujumbe Professa Klaus Schwab, Mwenyekiti mtendaji wa Jukwaa la Uchumi Duniani kwa mwaka 2018, ujumbe uliosomwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Katika ujumbe huo, Baba Mtakatifu anakazia kwa namna ya pekee, utu na heshima ya binadamu na umuhimu kwa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu, kwa kuibua na kutekeleza sera na mikakati inayotoa kipaumbele kwa familia, uhuru wa binadamu na haki zake msingi, ili kweli watu waweze kuwa ni wadau wakuu wa mchakato mzima wa maendeleo yao. Nguvu za soko hazina budi kuratibiwa na haki msingi za wafanyakazi. Kumbe, mifumo ya kiuchumi haina budi kuzingatia sheria na kanuni za maendeleo endelevu ya binadamu, daima mwanadamu na haki zake msingi akipewa kipaumbele cha kwanza.

Vikwazo vya haki msingi za binadamu na upweke hasi ni mambo ambayo yanapaswa kuvaliwa njuga duniani ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano, kwa leo na kwa siku za usoni, ili kutoa mwelekeo mpya wa uchumi duniani. Sayansi na teknolojia rafiki haina budi kutumika ili kusaidia mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu; ulinzi na utunzaji bora wa mazingira Nyumba ya wote.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema, kwamba, watu wengi sana duniani, utu wao umejeruhiwa na kwamba, kuna mambo mengi yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika dimbwi la umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanapaswa kutambua kwamba, ni wajibu na dhamana yao ya kimaadili kuwashirikisha watu wengi katika mapambano dhidi ya umaskini na ukosefu wa haki msingi za binadamu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani na kwamba: ulimwengu una wajasiria mali wengi na uwezo wa kufanya mageuzi ya busara ili kuongeza tija na ubora wa huduma na bidhaa zinazozalishwa. Inawezekana kabisa kutengeneza nafasi za ajira kwa kuheshimu sheria za kazi; kwa kupambana na rushwa na ufisadi wa mali ya umma; kwa kuendeleza haki jamii na usawa katika matumizi ya faida inayopatikana.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.