2018-02-27 14:08:00

Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu aongezewa majukumu!


Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu kuwa Balozi mpya wa Vatican huko kwenye Visiwa vya Saint Lucy, Grenada na Bahamas. Ataendelea kuwa ni Balozi wa Vatican huko Trinidad na Tobago, Antigua na Barbuda, Barbados, Dominica, Jamaica, Saint Kitts na Nevis, Saint Vincent na  Grenadines, Guyana, na pia ni Mjumbe wa kitume wa Visiwa vya Antilles.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa kumi na sita, alimteua Monsinyo Fortunatus Nwachukwu kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Nicaragua pamoja na kumpandisha hadhi ya kuwa ni Askofu mkuu. Kabla ya uteuzi wake, alikuwa ni Afisa Mwandamizi wa Itifaki mjini Vatican. Askofu mkuu Fortunatus Nwachukwu alizaliwa Ntigha, Nigeria kunako tarehe 10 Mei 1960. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapadrishwa tarehe 17 Juni 1984. Alianza kutoa huduma za kitume mjini Vatican tarehe Mosi Julai 1994. Amewahi kufanya kazi katika Balozi za Vatican nchini Ghana, Paraguay, Aligeria na kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa zenye makao yake mjini Geneva.  Kunako tarehe 4 Septemba 2007, aliteuliwa kuwa ni Afisa Mwandamizi wa Protakali mjini Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.