2018-02-24 08:28:00

Kwaresima: Fungeni na kujikatalia fahari ya macho inaponza!


Mahubiri ya Kipindi cha Kwaresima yanayotolewa na Padre Raniero Cantalamessa kwa Mwaka 2018 yanaongozwa na kauli mbiu “Wala msiifuatishe namna ya dunia hii”. Rum.12: 2. Katika mada hii amechambua kuhusu: Wakristo na dunia; kipeo cha kuyakimbia malimwengu na raha zake; Dunia na mambo yake inapita kwa haraka. Hii ni changamoto ya kutaka kuleta mabadiliko ulimwenguni na ndani ya Kanisa, lakini mabadiliko haya yanaanza katika maisha ya mtu binafsi kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, mwaliko wa kipindi hiki cha Kwaresima.

Dunia inapaswa kueleweka kwa mapana yake yaani yanayozingatia nyakati na mahali ndiyo maana Yesu aliwaambia wafuasi wake “Enendeni ulimwenguni kote”. Hii ni dhana inayofumbata pia tunu msingi za kimaadili. Ndiyo maana Yohane Mtume anawaalika Wakristo kutoipenda dunia wala mambo yake, kwani kwa kufanya hivi watashindwa kumpenda Mungu kutokana na tamaa ya mwili, macho na kiburi. Pamoja na mapungufu haya yote, lakini dunia ni sehemu ya kazi ya uumbaji, inayopendwa na kuokolewa na Mungu kama inavyojidhihirisha katika Fumbo la Pasaka. Wakristo watambue kwamba, wao wako duniani lakini si wa dunia hii, ndiyo maana Kristo Yesu katika Sala yake ya Kikuhani aliwaombea wafuasi wake kulitambua hili na kulifanyia kazi. Wakristo wanapaswa kuwa ni mashuhuda wa Injili ya Kristo kwa maneno na matendo yao, kama kielelezo cha imani tendaji.

Wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, tayari kusaidia mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu kwa harufu nzuri ya utakatifu wao, ndiyo maana baadhi ya Mababa wa Kanisa walikimbilia jangwani ili kujitenga na malimwengu na hivyo kupata nafasi ya kujitakatifuza na kuyatakatifuza malimwengu kwa kuungana na Mwenyezi Mungu zaidi katika maisha yao. Ni maisha yanayofumbatwa katika kufunga na kusali pamoja na kujikita katika tunu msingi za Kiinjili. Kukimbia ulimwengu ni mchakato wa kuachana na vishawishi, mizizi na nafasi ya dhambi kwa kujikita katika kutenda haki na kuwa na kiasi katika maisha.

Padre Raniero Cantalamessa anaendelea kufafanua kwamba, kipeo cha kuikimbia dunia kina pata kilele chake katika karne ya ishirini, baada ya watu wengi kumezwa na kuyaambata malimwengu, kiasi cha tunu msingi za Kiinjili kuwekwa rehani. Huu ukawa ni mwanzo wa taalimungu ya kuyatakatifuza malimwengu kwa kuwa na mwelekeo chanya zaidi ikilinganishwa na hapo awali. Lengo ni kuhakikisha kwamba, waamini wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu kwa kumkataa Ibilisi na mambo yake yote, changamoto ambayo ilivaliwa njuga na wakleri pamoja na watawa katika maisha na utume wao.

Huu ulikuwa ndio mwanzo wa “Taalimungu ya Kifo cha Mungu” kutaka kufifisha tunu msingi za Kiinjili kwa kuzama katika ukanimungu. Wakristo wakatakiwa kusimama kidete ili kutokubali hata kidogo kumezwa na malimwengu, bali daima wajitahidi kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, kwa kuwa wema na watakatifu badala ya kumezwa na kugubikwa na ubinafsi. Walitakiwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo; kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Imani ni mahali ambapo Mkristo anakutana na dunia pamoja na Fumbo la Maisha ya Kristo na utume wake, mambo ambayo yamefichwa kwa watu wenye hekima na busara, lakini wakafunuliwa watoto wadogo. Imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake, inakuwa ni kielelezo cha ushindi dhidi ya malimwengu kwani wanaongozwa na Kristo Yesu.

Watu wanaomezwa na malimwengu wanakosa nguvu ya maisha ya kiroho, ndiyo maana Mama Kanisa, mwanzoni mwa Kipindi cha Kwaresima anasema “Amka, wewe usinziaye, ufufuke katika wafu, na Kristo atakuangaza”. Wakristo wanakumbushwa kwamba, dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele. Mafanikio ya mambo ya kidunia yanajikita zaidi katika utajiri wa fedha na mali; afya na mafanikio katika maisha, lakini yote haya yanapita kama ndoto ya mchana na kifo kitakuwa ni mchungaji wao daima.

Padre Raniero Cantalamessa anawahamasisha waamini: kufunga na kujikatalia fahari ya macho inayopambwa kwa picha zinazorushwa na vyombo vya mawasiliano ya jamii. Kufunga kusiwe ni kuacha pombe na chakula kama inavyozoeleka na wengi. Kwaresima iwe ni fursa ya kuwa na ustaarabu wa kutumia vyema na kwa kiasi, maneno, chakula na vinywaji, lakini zaidi kusaidia kufunga na kudhibiti tamaa ya macho na kiburi cha maisha ya binadamu. Tamaa ya macho ilimwangusha Mfalme Daudi na ndivyo inavyojitokeza hata katika mitandao ya mawasiliano ya kijamii kwa sasa. Picha zina nguvu ni kama sumu ya nyoka mkali. Kufunga, kusali, matendo ya huruma na tafakari ya kina, iwe ni sehemu muhimu sana ya maandalizi ya maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, kwa kuyaacha malimwengu na fahari zake, ili kujikita katika mchakato wa kuyatakatifuza!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.