2018-02-23 07:13:00

Kanisa lisikilize kilio na kukata kiu ya maskini wanaoteseka duniani


Kanisa katika ulimwengu mamboleo halina budi kuwa macho na makini kwa kuangalia, kusikiliza na kujibu kilio cha maskini. Kanisa liwe chombo cha kukata kiu na matamanio halali ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama jibu muafaka la swali ambalo Mwenyezi Mungu anamuuliza Kaini yuko wapi Abeli ndugu yako? Jibu hili linalenga kusikiliza kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na: umaskini, ujinga, magonjwa, vita na kinzani mbali mbali za kijamii. Hiki ni kilio cha watu wanaonyimwa haki zao msingi, kiasi kwamba, utu na heshima yao kama binadamu vinawekwa rehani.

Ni watu wanaoteseka kutokana na ukosefu wa maji safi na salama; bila kusahau kwamba, wengi wao hawana hata huduma bora za afya. Ikumbukwe kwamba, elimu ni mkombozi wa maskini na wanyonge, kumbe, Kanisa linapaswa kuendelea kuwekeza katika elimu bora na makini kwa kusoma alama za nyakati kama jibu la kilio cha mahangaiko ya maskini duniani! Ni kilio cha watu wanaoteseka kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kiasi kwamba, magonjwa ya milipuko umekuwa ni wimbo usiokuwa na kiitikio!

Inasikitisha kuona kwamba, sera na mikakati ya maendeleo ya kijamii inasimikwa katika dhambi na matokeo yake, maskini wanaendelea kuogelea katika umaskini wao licha ya sera na mikakati ya kitaifa na kimataifa inayopania kuwakomboa kutoka katika hali na mazingira haya. Changamoto za kilio cha maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kinahitaji toba na wongofu wa ndani ili kusimamia kikamilifu haki jamii, utu, heshima na haki msingi za binadamu, kikolezo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu yanayogusa mahitaji mtu mzima: kiroho na kimwili.

Ni changamoto ya kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Kanisa linapaswa kuwa na ujasiri ili kuthubutu kugusa kiini cha umaskini, ujinga na maradhi, ili kujibu kilio cha mateso na mahangaiko ya maskini sehemu mbali mbali za dunia, daima likijitahidi kufuata nyayo za Kristo Yesu aliyekuwa ni mtu wa pembezoni mwa jamii tangu kuzaliwa kwake hadi kifo Msalabani. Hii ni sehemu ya tafakari iliyotolewa na Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Alhamisi jioni, tarehe 22 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya Roma, Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Kumbu kumbu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro.

Kristo Yesu alizaliwa Nazareti, mji ambao hakuwa na umaarufu hata kidogo; kana kwamba, hili halitoshi, akazaliwa kwenye pango la kulishia wanyama. Yesu alianza utume na maisha yake huko pembezoni mwa jamii, ili kuwahubiria maskini Habari Njema ya Wokovu, kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, vipofu kupata kuona tena, pamoja nakuwaacha huru waliosetwa. Akatoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, wagonjwa, vilema na wale wote waliotengwa na jamii, kiasi kwamba, hata Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wake, ulitendeka pembezoni mwa jamii na akaamua kuwatangulia kwenda Galilaya. Pembezoni mwa jamii ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa; uzoefu na mang’amuzi ya kikristo kama mahali muafaka pa kukutana tena na tena na Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Padre Josè Tolentino de Mendonca anakaza kusema, hata Ukristo umezaliwa kutoka pembezoni mwa jamii kiasi kwamba, sera, mipango na mikakati yake ya shughuli za kichungaji inapaswa kujielekeza pembezoni mwa jamii, kwa kugusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili, ili kuwatangazia watu Injili ya upendo; kuganga madonda na magumu ya maisha yao kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Kanisa halina budi kujitambulisha na watu wanaoteseka kutokana na vita, kinzani, dhuluma na nyanyaso mbali mbali; mambo yanayofifisha utu, heshima na haki zao msingi kama binadamu. Kanisa linalojifungia katika ubinafsi wake kwa kujitafuta lenyewe, litakosa dira, mwelekeo na mvuto wa kinabii! Kanisa lisikumbatie utajiri na watu matajiri, bali liwe tayari kushikamana na maskini na wale wote wanaoteseka kwa kuwa na ujasiri hata kiasi cha kuthubutu kugusa madonda, kiu na njaa inayomwandama mwanadamu. Kanisa liwe tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini kwa kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma na mapendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Ikumbukwe kwamba, uinjilishaji wa kina unafumbatwa katika ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, ili kuliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ni Msamaria mwema katika shida na mahangaiko ya binadamu!  Sakramenti ya Altare iwawezeshe viongozi wa Kanisa kuiona Sakrementi hii kati ya ndugu zao maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ili kuwatangazia Injili ya huruma, upendo na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni Injili inayosimikwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Kanisa lithubutu kukutana na kujadiliana na binadamu katika mahitaji yake msingi. Kanisa lioneshe uwepo wake kama Mama na Mwalimu tayari kupangusa machozi yanayowafumba watu macho kutokana na magumu mbali mbali ya maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.