2018-02-22 11:52:00

Papa Francisko: Waathirika wa Kamari na Upatu wapewe kipaumbele!


Michezo ya Kamari na Upatu ni donda ndugu linaloendelea kusababisha maafa na majanga makubwa katika maisha ya watu mbali mbali nchini Italia. Mchezo wa kamari na upatu ni matokeo ya myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Kamari ni dhambi kubwa inayopukutisha maisha ya watu na kudhalilisha utu wa binadamu na hivyo kuwa ni chachu ya rushwa, ufisadi na kizingiti katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Baba Mtakatifu Francisko  katika barua aliyomwandikia Monsinyo Alberto D’Urso, Rais wa Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA,” anaitaka Kamati hii, kuendelea kutoa kipaumbe cha pekee kwa waathirika. Itambue kwamba, hii ni dhamana inayotekelezwa kwa ujasiri na udumifu, ili kuwashirikisha jirani zao Injili ya matumaini na upendo.

Kamati hii ni benki yenye uhakika zaidi katika Ufalme wa Mungu. Hiki ni kipindi ambacho watu wengi wanaendelea kuathirika kwa rushwa na ufisadi, changamoto kubwa ni kuhakikisha kwamba, waathirika wanaangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo; kwa kuwasikiliza na kuwajali; pamoja na kupewa dira na mwongozo sahihi wa maisha, ili kuondokana na hatimaye, kuvunjilia mbali mnyororo wa athari za michezo ya kamari na upatu. Waathirika washirikishwe huruma na upendo wa Mungu, bila kuangalia udhaifu na mapungufu yao ya maisha. Huduma hii ni chachu makini ya matumaini kwa watu walioka tamaa ndani ya jamii, ili kuanza tena upya hija ya maisha yao inayojikita katika Injili ya matumaini.

Kwa kutambua madhara makubwa ya michezo hii, kunako mwaka 1991 Padre Massimo Rastrelli alianzisha Mfuko wa kwanza nchini Italia, dhidi ya michezo ya kamari na upatu, kiasi cha changamoto hii kuvaliwa njuga na wadau sehemu mbali mbali za Italia. Lengo ni kujenga utamaduni wa kuwasikiliza na kuwasaidia waathirika wa michezo ya kamari na upatu; kwa kuwapatia elimu makini, sheria, kanuni na taratibu zinazoweza kuwakwamua kutoka katika hali hii sanjari na kuhakikisha kwamba, waathirika wanasaidiwa kujenga na kudumisha dhamiri nyofu, itakayowawezesha kutafuta kilicho chema, kizuri na kitakatifu katika maisha.

Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II “Consulta Nazionale Antiusura, CNA,” imeweza kuzisaidia familia 25, 000 kwa kuokoa nyumba na vitega uchumi, kiasi hata cha kuweza tena kurejesha utu na heshima yao kama binadamu. Huu ni mchango mkubwa unaopaswa kuthaminiwa na kutambuliwa na wengi!  Itakumbukwa kwamba, hii ni sehemu ya hotuba iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa ujumbe wa Kamati ya Ushauri Kitaifa nchini Italia dhidi ya michezo ya Kamari na Upatu ya Yohane Paulo II, Jumamosi, tarehe 3 Februari 2018, walipokutana na kuzungumza naye mjini Vatican. Michezo ya kamari na upatu inadhalilisha na kuua; ni ugonjwa wa zamani sana, lakini bado unaendelea kuwadhalilisha watu wengi hata katika nyakati hizi.

Kumbe, kuna haja ya kujizatiti kikamilifu ili kuzuia na kuokoa maisha ya waathirika na vitega uchumi vyao; madeni makubwa ambayo mara nyingi wanashindwa kuyalipa kwa kuwapatia elimu ya kuwa na kiasi katika maisha pamoja na kujifunza kujinyima kwani kamwe mwanadamu hawezi kupata yote katika maisha. Watu waelimishwe umuhimu wa kuzingatia sheria pasi na shuruti, kujenga na kudumisha fadhila ya uaminifu, ukweli na uwazi katika maisha ya mtu binafsi na katika taasisi mbali mbali. Kuwepo na ongezeko la watu wa kujitolea ili kuwahudumia waathirika kwa kuwasikiliza, kuwashuri na kuwaongoza ili hatimaye, kuondokana na hali inayowanyanyasa na kuwatesa katika maisha, kiasi hata cha kuwanyima furaha, amani na utulivu wa ndani!

Myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa unatokana na ukweli kwamba, faida inapewa kipaumbele cha kwanza badala ya: utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu; kanuni maadili na utu wema; mshikamano na mafao ya wengi, lakini kumbe, haya ndiyo mambo ambayo yangepaswa kuzingatiwa katika sera na mikakati ya uchumi na maendeleo endelevu ya binadamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News. 
All the contents on this site are copyrighted ©.