2018-02-21 09:37:00

Kiu ya Yesu inamwilishwa katika imani, matumaini na mapendo!


Mababa wa Kanisa daima wameiona “Kiu ya Yesu” kwamba, ilijikita katika kutimiza mapenzi ya Baba yake wa mbinguni kwa njia ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko kutoka kwa wafu! Mtakatifu Agostino anasema, Yesu alikuja kwa watu wake, lakini hawakumpokea kwa imani na matokeo yake wakakosa uaminifu kwake, hali ambayo ilimsababishia mateso makali sana moyoni mwake. Yesu katika maisha yake, ameonesha kiu mara tatu: kwanza kabisa alipokutana na kuzungumza na Mwanamke Msamaria aliyemwomba maji yanayobubujikia maisha ya uzima wa milele.

Yesu anasema kwamba, yeye ni chakula cha uzima wa milele na yeyote ajaye kwake hataona njaa kabisa, naye anayemwamini hataona kiu kamwe. Mwishoni, Yesu alitoa mwaliko kwa wale wote wenye kiu waende kwake, wanywe pasi na malipo! Ni maneno ambayo bado yanaendelea kutoa mwaliko kwa waamini kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yao, daima wakiendelea na dhamana na wajibu wao waliojitwalia wakati walipopokea Sakramenti ya Ubatizo. Waamini wanahimizwa kumwendea Kristo Yesu kama sehemu ya hija ya imani ya maisha yao inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu linalomwilishwa katika matendo ya huruma kama alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Kristo Yesu anaendelea kulia kwa sauti kuu “Nina kiu”, zawadi ambayo inapaswa kupokelewa kwa moyo wa shukrani!

Haya ndiyo yaliyojiri katika tafakari ya Padre Josè Tolentino de Mendonca kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na Sekretarieti kuu ya Vatican, Jumanne jioni, tarehe 20 Februari 2018 huko Ariccia, nje kidogo ya Roma. Anasema, “Kiu ya Yesu” iilikuwa inafafanua zaidi maisha ya kiroho kuliko ilivyoeleweka na wasikilizaji wake kwa mara ya kwanza, yaani alikuwa anawaalika kupokea zawadi ya Roho Mtakatifu, ambaye aliwapatia wafuasi wake, alipokuwa Msalabani, lakini zaidi, Siku ile ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume, wakapata ari na jeuri ya kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa Msalabani amefufuka kwa wafu!

Yesu ndiye anayeweza kuzima kiu ya maisha ya kiroho kwa kusadaka maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Kiu ya Yesu ni changamoto kwa waamini kutoka katika ubinafsi wao, tayari kumpatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wao. Yesu kwa kuchomwa mkuki ubavuni, humo ikatoka damu na maji, alama za Sakramenti za Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II anasema, Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, aliteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kielelezo makini cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Yesu aliyamimina maisha yake kama zawadi kwa Kanisa lake, ili liweze kuwa ni kielelezo cha upendo wake usiokuwa na kipimo!

Padre Josè Tolentino de Mendonca anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa kwa nyakati zote ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu unaomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama alivyofanya Mama Theresa wa Calcutta. Huyu ni “mwanamke wa shoka”. Aliyejisadaka usiku na mchana ili kuzima kiu ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Mama Theresa akasukumwa kuanzisha Shirika la Wamisionari ambalo litajikita katika kutekeleza Mashauri ya Kiinjili kama kielelezo cha huduma ya upendo kwa maskini na wanyonge zaidi. Hawa ni watu wanaomdhihirisha Kristo ambaye bado anaona kiu kati ya maskini! Kiu ya Yesu ni alama ya upendo unaomwilishwa katika huduma, mateso na mahangaiko ya ndani kama njia ya kushiriki pia maisha na utume wa Kristo Yesu. Hakuna Pasaka pasi na Ijumaa Kuu!

Kristo Yesu kwa njia ya Roho Mtakatifu anaendelea kusema kwamba, anaona kiu ya: Upendo, Ukweli, Faraja na Wokovu, ili kuwawezesha waja wake kuendelea kuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya upendo; Umoja na mshikamano wa dhati unaowatambulisha wote kuwa ni watoto wa Baba mmoja, licha ya karama na zawadi mbali mbali kutoka kwa Roho Mtakatifu, ambazo kimsingi, zinapania kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Roho Mtakatifu ni mhimili mkuu katika mchakato mzima wa uinjilishaji, kwani daima analikumbusha na kuliongoza Kanisa katika mambo msingi ya maisha na utume wake.

Roho Mtakatifu anawataka wakristo kuendelea kutangaza na kushuhudia Injili ya furaha hata katika mateso, dhuluma na nyanyaso wanazokabiliana nazo katika maisha na utume wa Kanisa. Kanisa lazima liwe ni alama ya Injili ya matumaini kwa watu wa Mataifa. Roho Mtakatifu ni nguvu ya Mungu inayowapatia waamini maana ya utume wao unaomwilishwa katika upendo ili kupambana na umaskini, magonjwa na ujinga, utume ambao umevaliwa njuga na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni changamoto ya kuondokana na ubinafsi unaoweza kuwa ni kikwazo cha kukua na kukomaa kwa uhuru wa ndani, ili hatimaye, waamini waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya amani bila kukwepa matatizo na changamoto za maisha. Jumuiya za Kikristo ziwe ni chemchemi ya huruma, mapendo, faraja na matumaini kwa watu waliokata tamaa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.