2018-02-20 07:57:00

Viongozi wakuu wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Sahel wanakutana Dakar


Baraza Kuu la Mfuko wa Yohane Paulo II Ukanda wa Sahel, ulioanzishwa kunako mwaka 1984 ili kupambana na kuenea kwa Jangwa na Sahara, limeanza mkutano wake wa mwaka tarehe 19 Februari 2018 na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 23 Februari 2018 huko Dakar, Senegal. Mfuko huu kwa sasa unasimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu. Katika mkutano huu Monsinyo Segundo Tejado Munoz, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anashiriki kama mtazamaji wa kudumu kutoka Vatican.

Maaskofu wanaoshiriki mkutano huu ni wale wanaotoka Burkina Faso, Senegal Mauritania, Niger, Cape Verde, Ciad, Gambia, Guinea Bissau na Mali, wanaongozwa na Askofu Sanou Lucas Kalfa kutoka Burkina Faso ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti. Ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani unashiriki kwani, wao ndio wafadhili wakuu wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ukanda wa Sahel. Miradi inayopembuliwa na kujadiliwa kwa mwaka 2017 ilikuwa ni 127 iliyo gharimu kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 2.3. Hadi kufikia mwaka 2016 jumla ya miradi 3, 200 ilipitishwa na kugharimiwa kwa kiasi cha Dola za Kimarekani zaidi ya milioni 38.

Miradi inayotekelezwa kwa niaba ya Khalifa wa Mtakatifu Petro ni ile ya kupambana na Jangwa la Sahara, ili kuweza kuboresha mazingira, nyumba ya wote kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko. Ni miradi inayopania kuinua ubora na tija katika sekta ya kilimo ili kuweza kuwa na uhakika wa usalama wa chakula; maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu. Mfuko huu unafadhili pia miradi ya teknolojia rafiki kwa ajili ya nchi wanachama wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ukanda wa Sahel.

Tangu kuanzishwa kwake, Mfuko huu umekuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Ukanda wa Sahel kwani umesaidia kutoa mafunzo kwa wataalam; umegharimia mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene katika huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu, inayogusa mahitaji yake msingi kiroho na kimwili. Sehemu kubwa ya watu wanaofaidika na mradi huu ni waamini wa dini ya Kiislam, lengo likiwa ni kujenga umoja na mshikamano katika huduma. Hali ngumu ya maisha inayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika umaskini inasababishwa kwa kiasi kikubwa na vita, kinzani na migogoro ya kijamii; athari za mabadiliko ya tabia nchi pamoja na misimamo mikali ya kidini na kiimani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.