2018-02-20 16:40:00

UNICEF na mbinu mkakati wa kuokoa maisha ya watoto wachanga!


Hamjambo Wasikilizaji wapendwa popote pale mlipo.  Sauti ya kudai Usawa na Haki za Wanawake inakualikeni. Amkeni na tujiunge pamoja ili kulinda Amani, hadhi, Utu na kujenga Maendeleo yetu kwa ujumla.  Kutoka Vatican News, ni mimi Mtangazaji wako Pauline Mkondya nikisema, “Karibuni”. Msikilizaji, Kila mwaka karibu milioni mbili nukta sita katika miezi sita ya watoto wachanga wanapoteza maisha yao tangu siku hiyo waliozaliwa.  Hivyo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia Watoto, UNICEF, Henrietta H. Fore amesema kwamba UNICEF imeanzisha Kampeini  ya “Kila mtoto hai ni Maisha”.  Ripoti ya UNICEF, inaonyesha kuwa watoto wanaozaliwa katika nchi maskini zaidi duniani wengi kutoka Bara la Afrika wanakabiliwa na hatari ya kifo ikilinganisha na wa nchi tajiri.,wakati robo ya mwisho ya karne imeshuhudia maboresho makubwa katika afya ya watoto wakubwa, jitihada zimekuwa ndogo kutokomeza vifo vya watoto chini ya mwezi mmoja, akiongeza kwamba vifo vingi vinaweza kuzuilika.

Kati ya nchi 10 ambazo ziko katika hatari kubwa, 8 ni kutoka Kusini mwa Afrika mwa jangwa la Sahara ambako mama mjamzito ana uwezekano mdogo wa kupata msaada kwa sababu ya umaskini, migogoro au taasisi dhaifu kwa mujibu wa ripoti hiyo.  Nchi hizo 8 ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, DRC, Somalia, Lesotho, Guinea-Bissau, na Sudan Kusini. Nyingine ni Ivory Coast, Mali na Chad. Ripoti hiyo imezinduliwa sanjari na uzinduzi wa Kampeni ya kidunia iliyopewa jina la "kila mtoto hai" inayolenga kuhakikisha upatikanaji wa suluhusho la huduma bora za afya kwa kila mama na mtoto".

Zaidi ya asilimia 80 ya vifo vya watoto wachanga vinaweza kuzuilika, inasema ripoti hiyo, "kwa upatikanaji wa wakunga waliopatiwa mafunzo bora, pamoja na ufumbuzi mwingine kama upatikanaji wa maji safi, kemikali za kuua viini vya maradhi, unyonyeshaji wa maziwa ya mama ndani ya saa moja ya kwanza mtoto anapozaliwa ni muhimu, na mlo bora zaidi". Lakini uhaba wa wakunga na wafanyakazi wa afya wenye mafunzo bora ni tatizo kubwa katika mataifa yaliyo maskini. Wakati nchi tajiri kama Norway ina madaktari 18, wauguzi na wakunga kwa kila watu 10,000,  lakini nchi maskini kama Somalia ina mtaalamu mmoja tu. Tangu maboresho ya afya yanaweza kuwa ghali" ni muhimu sana kuwekeza fedha kwa njia nzuri".  Hata hivyo, kati ya nchi ambazo zimefanya maboresho makubwa ni Rwanda, ambayo zaidi ya nusu ya kiwango chake kimepungua kuanzia 1990 hadi 2016, ikionyesha kwamba "utashi wa kisiasa wa kuwekeza katika mifumo ya afya yenye nguvu ni muhimu," imesema ripoti hiyo.

Masuala ya elimu, pia yanahusika. Watoto waliozaliwa na mama wasio na elimu huwa karibu mara mbili  katika hatari ya kufa mapema, ikilinganishwa na watoto wachanga waliozaliwa na mama wenye elimu ya sekondari. Marekani kwa ujumla ambayo ina utofauti wa mapato na tofauti kubwa katika upatikanaji wa huduma za afya ilikuwa ni nchi ya 41 iliyo salama zaidi kwa watoto wachanga. Msikilizaji, kiwango cha vifo vya watoto wachanga  duniani hivi sasa bado ni kikubwa, na kinatisha sana. Tukumbuke tunda la Uhai ni haki ya wote, kwa pamoja tuilinde zawadi hii. Basi kwa maelezo haya nimefikishwa mwishoni mwa ujumbe huu.  Nawaageni na kuwatakia mfungo mwema wa Kwaresima.

Na Pauline Mkondya.

Vatican News.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.