2018-02-20 15:12:00

Papa Francisko: Kanisa Jimbo Katoliki la Ahiara limejeruhiwa vibaya!


Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la kung’atuka kutoka madarakani lililowasilishwa kwake na Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara, lililoko nchini Nigeria. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu Lucius Iwejuru Ugorji wa Jimbo Katoliki Umuahia, kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Ahiara ambalo kwa sasa liko wazi!  Taarifa iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu inasema, Baba Mtakatifu Francisko amemshukuru na kumpongeza Askofu Peter Ebere Okpaleke kwa kuchukua maamuzi mazito kiasi hiki, kielelezo cha upendo kwa Kristo na Kanisa lake.

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kati ya Mwezi Juni na Julai 2017, alipokea barua binafsi zaidi ya 200 kutoka kwa wakleri wa Jimbo Katoliki la Ahiara. Baadhi ya mapadre walionesha shida ya kisaikolojia kwa kusutwa na dhamiri zao nyofu kuweza kushirikiana na Askofu Peter Ebere Okpaleke katika maisha na utume wake kama Askofu mahalia baada ya miaka mingi ya patashika nguo kuchanika. Wengi wao walitubu na kuomba msamaha kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ambaye alisitisha adhabu aliyokuwa ameamuru itolewe kwa wakleri wa Jimbo Katoliki Ahiara.

Baraza la la Kipapa la Uinjilishaji wa watu linawataka Mapadre kufanya tafakari ya kina na kuona jinsi ambavyo wamelichafua Kanisa la Kristo na kwamba, huko mbeleni hawatarudia tena kitendo cha namna hii cha kumkataa Askofu mahalia aliyeteuliwa kiuhalali na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Baba Mtakatifu anawashukuru wakleri, watawa na waamini walei ambao wameonesha upendo na mshikamano na Askofu Peter Ebere Okpaleke kwa hali na mali. Analishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria pamoja na viongozi wote wa Kanisa waliojizatiti kuhakikisha kwamba, tatizo hili linapatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko hana nia ya kuteua Askofu mpya, bali ataendelea kufuatilia kwa karibu sana mwenendo mzima wa maisha na utume wa Kanisa mahalia, kwa kumteua Askofu Lucius Iwejuru Ugorji wa Jimbo Katoliki Umuahia, kuwa ni Msimamizi wa Kitume wa Jimbo Katoliki la Ahiara kwa kumpatia mamlaka yote ya Askofu mahalia. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, Jimbo litaanza kufufuka na kamwe halitateseka tena na vitendo hivi ambavyo vimesababisha madonda katika Fumbo la Mwili wa Kristo yaani, Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.