2018-02-20 16:16:00

Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke asimulia yaliyomsibu kwa miaka 5


Askofu Peter Ebere Okpaleke wa Jimbo Katoliki Ahiara, Nigeria aliyeng’atuka kutoka madarakani, tarehe 19 Februari 2018, amewaandikia barua ya kichungaji wakleri, watawa na waamini walei akieleza kwa kina na mapana umuhimu wa kutubu na kumwongokea Mungu, tayari kujipatanisha. Kwa kipindi cha miaka mitano amekabiliana na changamoto za kukataliwa kuwekwa wakfu na hatimaye kuingia Jimboni mwake kama mchungaji mkuu licha ya jitihada za Baba Mtakatifu Francisko, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria.

Baadhi ya watu wameonesha moyo mgumu na kushindwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kutenda kazi yake. Kutokana na changamoto zote hizi anasema Askofu Peter Ebere Okpaleke njia muafaka kwake ni kung’atuka kutoka madarakani kwa kuzingatia ustawi, mafao na maendeleo ya familia ya Mungu Jimboni Ahiara ili kutoa nafasi kwa waamini waaminifu waliodhibitiwa na baadhi ya wakleri kupata tena huduma za kiroho. Ni matumaini yake kwamba, uamuzi huu utasaidia kwa kiasi kikubwa kufufua ari na moyo wa uinjilishaji mpya unaohitajika kwa namna ya pekee kwa wakleri wa Jimbo hili baada ya kuonesha utovu wa nidhamu na kukosa utii kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Anamwomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo amsamehe mapungufu yake kama yalikuwepo! Anawashukuru wote waliomsaidia katika kipindi chote hiki cha mapambano ya maisha ya kiroho na kwamba, wakleri wa Jimbo la Ahiara wanapaswa kutubu, kumwongokea Mungu na kujipatanisha tena na Kanisa. Anaitaka familia ya Mungu jimboni humo kushikamana kwa kutambua kwamba, wao ni watoto wa Baba mmoja, wamepokea imani moja, Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi na kwamba, kwa pamoja wanaunda familia ya Mungu!

Itakumbukwa kwamba, Askofu Peter Ebere Okpaleke aliteuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako tarehe 7 Desemba 2012 na kujiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu ili aweze kutekeleza mapenzi yake, lakini akakumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa wakleri na baadhi ya waamini walei. Kuwekwa kwake wakfu na hatimaye kusimikwa kama Askofu kukacheleweshwa sana. Baba Mtakatifu Francisko alipoingia madarakani, akaridhia uteuzi uliokuwa umefanywa na Papa Mstaafu Benedikto XVI, lakini hata hivyo bado akakumbana na “kisiki cha mpingu”. Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria likaingilia kati lakini hata nalo likakwama kutekeleza dhamana hii kadiri ya Sheria za Kanisa.

Kwa unyenyekevu mkubwa, akaomba kuongezewa muda ili kuangalia hali, lakini bado ikashindikana na hivyo kujikuta akiwekwa wakfu kama Askofu tarehe 21 Mei 2013 nje ya Jimbo Katoliki la Ahiara. Tangu wakati huo hakuweza kusimika rasmi Jimboni mwake, hadi tarehe 19 Februari 2018 alipong’atuka madarakani kwa kuomba ridhaa ya Baba Mtakatifu Francisko. Kwa miaka mitano juhudi mbali mbali zilifanywa ili kurejesha Jimbo katika hali yake ya kawaida lakini zikagonga mwamba na wala hakuweza kutia mguu Jimboni humo! Kwa hakika anasema, wakleri Jimboni humo wakashindwa kumpatia nafasi Roho Mtakatifu afanya kazi yake, ili aweze kutekeleza dhamana na wajibu wake kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ukabila usiokuwa na mvuto wala mashiko umewafumba macho kiasi cha kushindwa mpango wa Mungu katika maisha yao.

Baadhi ya wakleri na waamini waliendelea kumchafua ndani na nje ya nchi, changamoto kwa wakleri na waamini kama hawa kutambua madhara makubwa ambayo wamelitendea Kanisa la Kristo! Mapadre wakashindwa kuonesha umoja na mshikamano na Askofu wao. Baada ya tafakari ya kina, akaamua kumwandikia Baba Mtakatifu Francisko barua kuomba kung’atuka kutoka madarakani kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo. Anasema, anang’atuka kwa moyo radhi kabisa bila kubaki na kinyongo kwa mtu awaye yote. Jimbo hili litaendelea kubaki kuwa ni sehemu ya maisha na utume wake, ambao ameuhifadhi katika sakafu ya moyo wake. Anamwomba Kristo Yesu kuganga na kuponya madonda ya mpasuko uliojitokeza, ili hatimaye, aweze kuwangoza kondoo wake katika malisho ya majani mabichi, kando ya maji ya utulivu!

Askofu mstaafu Peter Ebere Okpaleke anamshukuru Baba Mtakatifu Francisko pamoja na viongozi mbali mbali wa Kanisa waliompatia ushirikiano kwa muda wa miaka mitano aliyoishi nje ya Jimbo lake teule. Anawaalika wakleri Jimboni humo kutubu na kumwongokea Mungu ili waweze kujipatanisha na Kanisa kwa kuonesha utii na imani thabiti; kujenga na kuimarisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro pamoja na kufanya tafakari ya kina kuhusu malengo yao katika maisha na utume wa Kipadre. Anawakumbusha wote kwamba wanajenga familia moja ya watoto wa Mungu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.