2018-02-18 07:30:00

WCC: Ushuhuda wa Injili ya Amani unafumbatwa katika sala na kufunga


Hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican ametangaza kwamba, tarehe 23 Februari 2018, Ijumaa ya Kwanza ya Kipindi cha Kwaresima, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wafunge na kusali, kwa ajili ya kuombea amani duniani. Lakini kwa namna ya pekee, kuombea amani huko DRC na Sudan ya Kusini ambako watu wanateseka sana kutokana na vita, ghasia na mipasuko ya kijamii na kinzani mbali mbali.

Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwaalika hata waamini wa dini mbali mbali kuungana naye kutekeleza dhamana na wajibu huu wa kimaadili kadiri ya taratibu, sheria na kanuni za dini zao, lakini watu wote kwa pamoja, waweze kumlilia Mwenyezi Mungu ili amani ya kweli iweze kupatikana katika maeneo haya ambayo watu wake wanateseka sana kwa vita. Anasema, Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, daima anasikiliza kilio cha watoto wake, wanaomkimbilia kwa machozi na mateso makubwa wakiomba msaada wake, ili kuwaponya waliopondeka moyo na kuzingaga jeraha zao.

Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu Mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anasema, tayari amepokea mwaliko kutoka kwa Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo na kwamba, Makanisa wanachama wa Baraza hili yatashiriki kikamilifu, ili kuombea: haki, amani na maridhiano huko Sudan ya Kusini na DRC ammbako kwa sasa kunawaka moto! Takwimu zinaonesha kwamba, kuna watu zaidi ya milioni 4.3 ambao hawana makazi maalum na kwamba, kuna zaidi ya watu milioni 13.1 watakaohitaji msada wa dharura katika kipindi cha mwaka 2018.

Dr. Olav Fykse Tveit, anasema, katika kipindi cha miaka minne ya: vita, kinzani na migogoro ya vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan ya Kusini, watu zaidi ya milioni 2 wamekimbia kutoka nchini humo ili kutafuta: hifadhi na usalama wa maisha yao. Kuna zaidi ya watu milioni 7 wanaohitaji msaada wa dharura nchini Sudan ya Kusini. Waathirika wakuu ni watoto, wanawake na wazee. Hawa ni watu ambao utu na heshima yao viko hatarini kutokana na vitendo vinavyodhalilisha utu na heshima yao kama binadamu. Baraza la Makanisa Ulimwenguni kwa kushirikiana na wadau mbali mbali limekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi wa Sudan ya Kusini kwa njia ya Makanisa yake wanachama. Mshikamano wa sala na kufunga kwa ajili ya mateso na mahangaiko ya wananchi wa Sudan ya Kusini na DRC ni ushuhuda wa Injili ya Amani, inayotafutwa na watu wengi sana duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News.








All the contents on this site are copyrighted ©.