2018-02-15 07:44:00

Mwilisheni upendo wa kimama katika huduma kwa wagonjwa na maskini


Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anasema ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani iliyoadhimishwa hivi karibuni, yameongozwa na kauli mbiu “Mama tazama mwanao. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake”. Baba Mtakatifu anataka mchakato wa tiba na huduma kwa wagonjwa kuhakikisha kwamba, Unazingatia kwanza kabisa utu, heshima na mahitaji msingi ya mgonjwa mintarafu huruma na upendo wa kimama, unaoneshwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa!

Baba Mtakatifu anapembua kuhusu: wito wa Mama Kanisa wa huduma kwa wagonjwa na maskini; kumbu kumbu endelevu ya historia ya huduma kwa wagonjwa sanjari na nguvu ya uponyaji inayoonesha uhusiano uliopo kati ya utume wa uponyaji na mwamko wa imani kwa wagonjwa wanaokutana na Kristo Yesu, wakiomba huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Huduma ya uponyaji inayotekelezwa na Kristo Yesu kwa wagonjwa mbali mbali inahitaji jibu la imani thabiti kutoka kwa wahusika ili kujenga na kudumisha Injili ya matumaini.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anawataka wanafamilia na wahudumu katika sekta ya afya kujenga utamaduni wa huruma, upendo na ukarimu kwa wagonjwa; fadhila ambazo pia zinaweza kumwilishwa kwenye nyumba za kuwatunza wazee, mahali penye misiba bila kusahau nyumba za watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu. Wakuze ndani mwao fadhila ya akili na upendo wa kimama ili kuweza kukabiliana na changamoto mbali mbali katika maisha na utume wao kama alivyofanya Bikira Maria.

Kanisa kama Mama na Mwalimu anayo dhamana ya kuganga na kuponya magonjwa yanayomwandama mwanadamu: kiroho yaani dhambi pamoja na magonjwa ya mwili, yanayoonesha na kudhihirisha udhaifu wa binadamu matokeo ya dhambi ya asili. Wahudumu katika sekta ya afya wawe na uwezo na ujuzi wa kushuhudia ukweli katika huduma kwa wagonjwa, chemchemi ya matumaini hata katika mateso na mahangaiko ya wagonjwa. Mawasiliano baridi yasiyokuwa na chembe ya upendo wala utu ni hatari sana kwa wagonjwa na familia zao. Wahudumu wa afya wawe tayari kuwasindikiza wagonjwa kwa upendo wa kimama katika hatua mbali mbali za maisha yao, hadi pale wanapokaribia kuhitimisha maisha yao na kurudi nyumbani kwa Baba wa milele! Iwe ni safari ya imani na matumaini na wala si ya woga na hali ya kukata tamaa. Wahudumu wa sekta ya afya watambue, wakiri na kuthamini uwezo wa tiba inayoweza kutolewa kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia! Wakiri pia mapungufu yanayoweza kujitokeza katika sekta ya tiba na kinga katika afya ya mwanadamu. Kifo laini si suluhu ya changamoto wanazokumbana nazo wagonjwa katika maisha yao. Wagonjwa na wahudumu wa afya wajenge na kuimarisha mahusiano na urafiki katika ukweli, uwazi na mshikamano.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako mwaka 1985 aliandika Barua binafsi ijulikanayo kama “Dolentium Hominum” yaani “Mateso ya watu” kwa kusema kwamba, ni ukweli usiopingika kwamba, Mama Kanisa amekuwa mstari wa mbele katika huduma kwa wagonjwa na maskini sehemu mbali mbali za dunia, kielelezo cha huduma endelevu ya uponyaji uliofanywa na Kristo Yesu, muasisi wa Kanisa. Afya njema kwa nchi zilizoendelea ni kipimo cha ubora wa maisha na maendeleo, hali inayoweza kuleta uelewa finyu kwamba, kwa mtu asiyeweza kukidhi vigezo hivi hana sababu ya kuishi na matokeo yake ndiyo dhana ya kifo laini, badala ya kujenga na kudumisha upendo na mshikamano kati ya watu!

Mama Kanisa anatambua utu na heshima ya binadamu na kwamba, katika nchi maskini, afya njema ni kukosekana kwa magonjwa. Ndiyo maana Kanisa limekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, linajikita katika tiba na kinga kwa magonjwa yanayoweza kupatiwa chanjo hasa kwa watoto wadogo, ili kupunguza vifo vya mama na mtoto. Mgonjwa anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa pamoja na kuhakikisha kwamba, haki zake msingi zinalindwa na kudumishwa. Hii ndiyo changamoto inayovaliwa njuga na Mama Kanisa ili kuhakikisha kwamba, huduma ya kinga na tiba kwa wagonjwa inakuwa ni sehemu ya vinasaba vya Injili ya upendo kwa wagonjwa na maskini anasema Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson.

Huduma ya shughuli za kichungaji kwa wagonjwa inapania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha utamaduni wa Kikristo unaojikita katika tiba, kinga na huduma makini kwa wagonjwa. Hii ni changamoto pevu inayogusa medani mbali mbali za maisha ya binadamu; sera na mikakati katika sekta ya afya; mazingira, uwezo wa kiuchumi, fursa za ajira na hali ya familia. Mama Kanisa anapenda kukumbusha kwamba, binadamu ana udhaifu na mapungufu yake, kumbe, anapaswa kusaidia na kusaidiwa katika hija ya maisha yake hapa duniani! Tiba inapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba vya sera, mipango na mikakati ya wanasiasa katika maendeleo endelevu ya binadamu, ili kuhakikisha kwamba, watu wanapata huduma na dawa muhimu katika maisha yao; mambo ambayo pengine si muhimu sana kiuchumi, lakini ni nyeti sana katika mchakato wa kutaka kuokoa maisha ya watu.

Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson anaendelea kufafanua kwamba, katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, changamoto kubwa inayojitokeza ni ukosefu wa usawa kati ya watu, ubaguzi katika masuala ya kijamii na huduma msingi bila kusahau kwamba, waathirika wakubwa wa mabadiliko ya tabianchi ni maskini na “akina yakhe pangu pakavu tia mchuzi”. Vitu vinapewa kipaumbele cha kwanza badala ya utu na heshima ya binadamu. Kanisa linapenda kukazia mchakato wa huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na mahitaji msingi ya binadamu! Binadamu anapaswa kuwa ni kiini cha sera na mikakati yote ya maendeleo endelevu na wala si vitu wala faida kubwa! Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kufanya tafiti makini zinazojikita katika tunu msingi na amana za maisha ya kiroho, daima wagonjwa na maskini, wakipewa kipaumbele cha kwanza. Huduma ya afya kwa wagonjwa na maskini, iwasaidie waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuiona sura ya Kristo Yesu anayeteseka miongoni mwa ndugu zake maskini na wagonjwa, aliowapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 








All the contents on this site are copyrighted ©.