2018-02-15 08:14:00

Miaka 160 tangu Bikira Maria alipomtokea Mt. Bernadetha, Lourdes!


Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu anasema, ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko kwa Maadhimisho ya Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani hapo tarehe 11 Februari 2018 yameongozwa na kauli mbiu “Mama tazama mwanao. Na tangu saa ile mwanafunzi yule akamchukua nyumbani mwake”. Huu ni ujumbe wa imani, matumaini na mapendo kwa wagonjwa, ili kusimamia haki zao msingi. Bikira Maria ni chombo na shuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo, ambaye yuko tayari kuwapangusa machozi, watoto wake wote wanaomkimbilia kwa ulinzi na tunza yake ya kimama, bila kukatishwa tamaa hata na magonjwa ya muda mrefu pamoja na upweke hasi!

Ilikuwa ni tarehe 11 Februari 1858, yaani miaka 160 iliyopita, Bikira Maria alipomtokea Mtakatifu Bernadetha Soubirou huko Lourdes, Ufaransa na huo ukawa ni mwanzo wa hija waamini kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Lourdes, ushuhuda unaotolewa kila siku katika Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes. Ni tukio ambalo limeacha alama ya kudumu katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes ni kitovu na shule ya tasaufi ya Bikira Maria.

Kardinali Lorenzo Baldisseri anaendelea kufafanua kwamba, Kristo Yesu kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, amevunjilia mbali giza la dhambi na mauti na hivyo kuwakirimia waja wake nguvu ya kuweza kubeba vyema Misalaba katika maisha yao. Msalaba katika maisha ya Kikristo ni alama ya ushindi na utukufu wa Kristo Yesu unaofumbatwa katika fadhila ya utii, unyenyekevu, imani na matumaini. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Siku ya 26 ya Wagonjwa Duniani kwa Mwaka 2018 anasema kwamba, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwapatia pia mitume na waandamizi wao nguvu ya uponyaji na kwamba, Kanisa linaendeleza huduma hii kwa huruma na mapendo na kwamba, inapaswa kupyaishwa na kumwilishwa kutoka katika familia, parokia hadi kufikia taasisi za huduma ya afya.

Wagonjwa wa muda mrefu, walemavu na wazee wanapaswa kuangaliwa zaidi kwa jicho la upendo na kwamba, kuna haja pia ya kuwa na sera makini za huduma kwa wagonjwa. Wadau wa huduma ya afya watambue kwamba, wanashiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa wagonjwa, changamoto kwao ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kumwilisha tunu msingi za maisha ya Kikristo kama ushuhuda unaotajirisha huduma kwa wagonjwa. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Barua yake binafsi “Dolentium hominum”  yaani “Mateso ya watu” iliyochapishwa kunako mwaka 1985 alianzisha rasmi Baraza la Kipapa la Huduma ya wafanyakazi katika sekta ya afya na kunako mwaka 1993 akaanzisha Siku ya Wagonjwa Duniani. Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, yakawa “Makao Makuu ya Wagonjwa Duniani”. Hapa ni mahali ambapo waamini wanaonja huruma na upendo wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, katika mwanga wa imani na matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu! Huduma kwa wagonjwa inawashirikisha wadau mbali mbali kuanzia katika familia hadi katika hospitali, vituo vya afya na nyumba za kutunzia wagonjwa na wazee.

Wakati huo huo, Askofu Jacques Benoit-Gonnin wa Jimbo Katoliki la Beauvais, lililoko Kaskazini mwa Ufaransa, ametambua muujiza aliotendewa Sr. Bernadette Moriau, mwenye umri wa miaka 78, baada ya kuponyeshwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua, baada ya kufanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Lourdes, kunako mwaka 2008. Chama cha “Bureau Mèdical International du Lourdes” yaani “Chama cha Madaktari wa Kimataifa cha Lourdes”, kimetambua na kukiri kwa uwepo wa muujiza huu ambao kwa sasa ni muujiza wa 70 kufanywa kwa maombezi ya Bikira Maria wa Lourdes. Jopo la madaktari limeridhishwa kwamba, hakuna maelezo ya kisayansi yanayoweza kutolewa juu ya kuponywa kwa Sr. Bernadette Moriau.

Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu akiwa nchini Ufaransa amepata pia fursa ya kugusia kuhusu maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana, itakayoadhimishwa mwezi Oktoba, 2018 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Vijana, Imani na Mang’amuzi ya Miito”. Itakuwa ni fursa kwa Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa vijana; kwa kuwarithisha vijana imani na Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Hii itakuwa ni Sinodi ya matumaini ya vijana wa kizazi kipya. Haya ni matumaini yanayofumbatwa katika maisha na utume wa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Kanisa litaendelea kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa urithishaji wa imani, matumaini na mapendo kwa watoto wake. Vijana wanao wajibu wa kuipokea zawadi hii na kuimwilisha katika vipaumble vya maisha yao, ili hatimaye, kuitolea ushuhuda kama wafuasi wamisionari wa Kristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!
All the contents on this site are copyrighted ©.