2018-02-15 09:57:00

Kwaresima ni kipindi cha mapambano ya maisha ya kiroho!


Mwaliko wa Kristo katika Dominika ya kwanza ya Kwaresima ni huu: “Tubuni na kuiamini Injili”. Yeye ndiyo hiyo Injili, ndiye habari njema ambayo anatualika tuiamini. Napenda tuanze tafakari yetu kwa kipindi hiki kwa kuongozwa na maneno ya sala ya ufunguzi ya Dominika hii yanayosema: “Ee Mungu utujalie kuifahamu siri ya Kristo na kupata manufaa yake katika mwenendo mwema wa mfungo wa Kwaresima”. Sala hii inaonesha hamu yetu ya kufunuliwa siri ya fumbo la Kristo, yaani kumwelewa vema Kristo na nafasi yake katika safari yetu hii ya toba. Kwa maneno mengine, bila kumwelewa vema Kristo itakuwa vigumu kuyapata matunda au manufaa ya majira haya ya toba yaani kugeuza mwenendo wetu kwa toba na kujivika Kristo. Yeye alikuwa kama sisi na aliyashinda majaribu, ushuhuda wa uwezo uliofichika ndani mwetu dhidi ya shetani.

Kwa fumbo la Umwilisho Kristo amechukua ubinadamu wetu. Wakati wa kipindi cha Noeli tulimtaja sana kwamba amakuwa kama sisi, amekuwa mtu halisi. Hii haimuepushi na ghasia na misukosuko ambayo tunakumbana nayo ikiwamo udhaifu wa kibinadamu. Alikuwa kama sisi katika hali zote; alisikia njaa, alikasirika, alifurahi, alikula nk. Kristo pia hakuepushwa na vishawishi vya shetani. Somo la Injili ya leo linatuonesha wazi kwamba “alikuwako nyikani siku arobaini, hali akijaribiwa na shetani”. Hivyo ni dhahiri alipita katika mazingira ya vishawishi ambavyo Mwinjili Marko haviweki wazi kama katika Injili nyingine pacha, ambazo huviweka katika makundi matatu ambayo ni mahitaji ya lazima ya kimwili, cheo au madaraka au ukuu wa kiulimwengu na mali (Rej Mt 4:1 – 11).

Kristo anakuwa kielelezo kwetu kwa namna ya kukabiliana na vishawishi hivi na kumpatia Mungu kipao mbele. Baada ya ushindi wake ndipo anapotualika kwa kututaka kutubu na kuamini katika Injili. Hapa ndipo tunapoona mantiki ya sala yetu ya Mwanzo inayoonesha hamu yetu ya kumfahamu vyema Kristo ili kuanza inavyostahili majira haya ya neema na kupata matunda yake. Tunamwona Kristo anayepita katika majaribu ya mwovu shetani akitoka yu mshindi, ishara ya uwezo huo wa kimungu unaofichika ndani mwetu sisi wanadamu. Anatufunulia kwa namna nyingine kutambua kile ambacho dhambi hufanya ndani mwetu, yaani kutuwekea ukungu akili zetu na kutokuuona huo uwezo tulionao tangu awali wa kusema ndiyo kwa Mungu tu na siyo kwa kitu kingine.

Injili ya Dominika hii inazidi kufunua jambo jingine la muhimu la kuzingatia. Hii ni nafasi ya Roho Mtakatifu. Injili inaanza kwa kusema “Roho alimtoa Yesu aende nyikani”. Hii inamaanisha aliingia nyikani akiwa amejaa Roho Mtakatifu ishara ya uwepo wa Mungu au uzima wa kimungu ndani mwake. Ndiye Roho huyo ambaye Kristo aliahidi atakuwa mlinzi na mhimarishaji wetu katika safari yetu hapa duniani tukielekea kwa Baba (Rej Yoh 16:13). Kristo alibaki mwaminifu kwa Mungu na kumpatia nafasi ya kwanza kwa sababu alikuwa ameungana naye. Hapa tunaona nafasi ya sala katika maisha yetu ya kikristo, tendo ambalo linapendekezwa pamoja na matendo mengine mawili yaani kufunga na matendo ya huruma wakati wa majira haya ya toba. Kwa njia ya sala zetu tunajazwa na uwepo wa Mungu ndani mwetu na hivyo kutoka mshindi katika majaribu ya shetani ni dhahiri.

Kipindi cha Kwaresima ni wakati wa kugeuza mienendo yetu na kuamsha lile ambalo ni la thamani lililomo ndani mwetu. Kwa ubatizo kama anavyotukumbusha Mtume Petro tuliokolewa na kufanywa wapya. Maji ya ubatizo yanakuwa kinyume na maji ya wakati wa gharika ambayo yaliangamiza uhai. Maji haya yanakuwa chanzo cha uhai kwetu na uthibisho wa ahadi ambayo Mungu alimwahidia Nuhu katika somo la kwanza kwamba hatamdhuru tena. Zaidi ya hayo Mungu anatuthibitishia utayari wake wa kutukomboa kwa kutuambia kwamba tutakapomuita yeye atatusikiliza, atatuokoa na kututukuza. Sasa tunataka tupewe nini tena? Nafasi hiyo inatuletea ukombozi wetu tena kwa bei chee kabisa; tusiache mbachao kwa msala upitao.

Tuingie sasa katika mapambano haya ya kiroho kwa kujiamini kwani tunaye Kristo kama kielelezo chetu cha kutoka tukiwa washindi. Hatukuumbwa kwa ajili ya kushindwa na shetani na tunapomwacha Mungu tukidhani tunaungana na shetani, yeye naye hutuacha na tunabaki tunahangaika tu. Ujasiri wetu uhamshwe na haiba tuliyo nayo ndani mwetu, tunu ambayo inachochewa, kutiwa nguvu na kuwezeshwa na uwepo wa Roho wa Mungu ndani mwetu. Roho huyu ndiye anayetukumbusha daima wema wa Mungu na kutupatia uwezo wa kuudhirisha katika maisha yetu.

Kila mmoja anapaswa kuingia ndani ya nafsi yake na kutafuta kile kinachomtia kiza na kumtoa nje ili asiutambue uwepo wa Mungu. Ni kitu gani hicho? Je ni kujitetea kwako kuwa unapokea kilicho stahili yako huku unamfumbia macho jirani yako? Hii inatufanya kujilimbikizia mali na vitu vingi vya anasa ambavyo kitaratibu za kidunia unaweza kuona si dhuluma kwani umepata kwa njia za haki lakini unafumba macho na kutomwona ndugu yako jirani. Je! Hujibu kama walivyotutahadharisha Maaskofu wa Tanzania katika ujumbe wao kwa Kwaresima kwa Mwaka 2018 tukisema: “Mimi ni mlinzi wa ndugu yangu?” Je! Ni uchu wa madaraka na mali ambao unanifumba macho hata kushindwa kuiona kweli katika utumishi wangu? Au Je! Ni tamaa ya kujilimbikizia mali ambayo inanipelekea kukosa hata chembe ya huruma katika kuwanyonya na kuwaangamiza wenzangu?

Mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.