2018-02-15 13:26:00

Komrade Morgan Tsvangirai, nenda kapumzike, utakumbukwa na wengi!


Bwana Morgan Tsvangirai aliyekuwa na umri wa miaka 65, kiongozi mkuu wa upinzani dhidi ya Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe enzi zao amefariki dunia, Jumatano tarehe 14 Februari 2018 nchini Afrika ya Kusini alikokuwa anapatiwa matibabu na kwamba, Serikali ya Zimbabwe imeamua kugharimia shughuli zote za mazishi yake. Marehemu Tsvangirai amekuwa ni nyota kubwa ya upinzani, akiwa na ndoto ya kuingia Ikulu ya Zimbabwe, ndoto ambayo ilimsababishia vipigo, kufungwa na kushitakiwa kwa makosa ya uchochezi.

Zimbabwe itamkumbuka kwa mchango wake mkubwa katika harakati za kuleta mageuzi baada ya Rais Robert Mugabe kukaa madarakani kwa kipindi cha miaka 37 na hatimaye, kung’olewa na Jeshi, mwezi Novemba 2017. Amekuwa ni mtetezi mkubwa wa haki msingi za binadamu nchini Zimbabwe. Kama kiongozi alikuwa na mapungufu yake, lakini zaidi alipania kuhakikisha kwamba, Zimbabwe inafanya mageuzi na kuanza kujikita katika haki msingi za binadamu. Bwana Morgan Tsvangirai kwa muda wa miaka miwili amekuwa akipambana na saratani ya utumbo mkubwa, ambayo imepelekea kifo chake. Amefariki dunia wakati Zimbabwe inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu, macho ya wananchi wengi wa Zimbabwe kwa sasa yanaelekezwa kwa Rais Emmerson Mnangagwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.