2018-02-14 15:46:00

Jangwa ni mahali pa mapambano ya maisha ya kiroho!


Tulipoanza kipindi cha kwaresima tulianza kwa kujipaka majivu – majivu ni alama na ukumbusho. Kama alama yatukumbusha mabaki na majivu huonesha masikitiko, shida, taabu na alama ya toba. Angalia Ayubu – 42:6 alipopoteza kila kitu, alikaa juu ya majivu n.k. Majivu hubaki baada ya moto kuunguza kila kitu. Baada ya dhambi ya asili kilichobaki ni dhambi. Ni kama ukumbusho wetu sote mahali tulikotoka – sura ya pili ya Kitabu cha Mwanzo – kuwa tuliumbwa toka mavumbi. Pamoja na tofauti zinazoweza kuwepo kati yetu n.k – siku ya majivu tunakumbushwa kuwa wewe ni udongo na udongoni utarudi. Katika tendo kama hilo – majivu huwa sasa mwaliko wa toba, kumrudia Mungu na kupokea maisha mapya. Mwaliko wa Isaya – toeni, tena si majivu bali mafuta.

Kwaresima yatuita tuingie katika hali ya jangwa. Jangwa ni mahali pa uzao wa watu wa Mungu wa Agano la Kale. Wayahudi toka utumwani Misri wanaingia nchi ya ahadi kama taifa moja chini ya Mungu. Ni jangwani walifanyika Taifa la Mungu kwa njia ya agano. Katika mahangaiko yao, walipomwasi Mungu n.k – manabii wanawakumbusha warudi jangwani ili kujikumbusha wao ni nani, vifungo vyao, ahadi ile, wito wao na utume wao kama njia tena ya kuiamsha imani yao na kuimarisha tena agano lao na Mungu. Manabii Eliya na Yohane Mbatizaji walikuwa watu wa jangwani: waliishi jangwani, walikula vyakula vya jangwani na wakaishi maisha yasiyo na makuu ya jangwani.

Katika Injili ya leo tunasoma – Mk. 1:12-13 – mara Roho akamtoa aende nyikani. Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na shetani, naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia. Ni wapi tena zaidi ya jangwani ambapo twaweza kukutana na Roho Mtakatifu na pia shetani, wanyama wa pori na pia malaika? Jangwani Yesu anapata muda wa kutofautisha sauti ya Mungu anayopaswa kufuata na ile ya shetani ambayo ni kishawishi. Ni sauti ngapi tuzisikiazo tangu tuamkapo hadi tuingiapo kitandani usiku? Ni kwa jinsi gani tunaweza kutofautisha miito mbalimbali?

Jangwa ni sehemu kubwa ambayo hizi sauti zinabaki nyuma. Jangwani tunapata nafasi ya kujifahamu nguvu zetu na udhaifu wetu. Pia tunaweza kuisikia na kuifahamu sauti ya Mungu. Jangwani Yesu alikutana na wanyama wakali na malaika. Wanyama wakali na pia malaika wapo katika kila mmoja wetu. Katika hali zetu tunashindwa kutambua wanyama wakali na hivyo tunabaki vipofu na kujisikia hovyo au tunashindwa kutambua malaika ndani yetu na hivyo kukata tamaa. Maisha jangwani yanatupa nafasi tena – kuangalia tulikotoka, tulipo na tuendapo. Kwaresima yatupa nafasi ya kutengeneza  jangwa na kuangalia maisha yetu. Uelewa huu hutusaidia kujua kuwa kwaresima ni kipi cha kusema ndiyo kwa Mungu na hapana kwa shetani.

Tunaona katika Somo la kwanza, kuwa Mungu anafunga agano na Nuhu na watoto wake baada ya gharika. Mwandishi anaelewa agano hili kwa mtu wa kwanza kuwa ni kilelezo cha agano – Mwa. 1:28-30. Hili Agano la kwanza liliharibiwa na dhambi ya mwanadamu. Akiangalia ubaya wa dhambi, Mungu anasikitika kwa kumwumba mwanadamu na moyo wake ukaumia – Mwa. 6,6. Gharika yaonekana kama Mungu anaingilia kati kwani mwanadamu kamkana yeye. Zuri na jema zaidi ni kuonekana kwa matumaini – Nuhu anapendelewa na Mungu – Mwa. 6,8. Hivyo zama inapita. Nuhu na familia yake wanamngojea Bwana. Naye Bwana anafanya tena kitu. Anafanya tena agano na hao watu. Ni kama Mungu anasema tena ya zamani yamepita. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Tuanze upya na upinde wa mvua unakuwa alama yao. Na katika Agano hili – Mungu anafanya agano na kila kiumbe na hapa mwisho viumbe vyote vitafanywa upya – Rum. 8:18-22. Ufahamu wa agano hili kati yetu na viumbe vyote ni alama ya upya wa agano hili.

Katika Injili tunamwona Yesu akiwa Jangwani kwa siku 40, mwanzo wa Kwaresima. Inahusisha pia kuonekana kwake Galilaya na mwanzo wa utume wake. Hii pia ni mwanzo mpya.  Kwamba Yesu – uwepo wake ni mwanzo mpya na unakubalika na wote wenye imani katika maandiko matakatifu na kumkubali kama Mwana wa Mungu.Tungesoma sehemu iliyotangulia tungesikia habari juu ya ubatizo wa Yesu. Mungu anatangaza rasmi kuwa Yesu ni mwanaye mpendwa tumsikilize yeye. Huyu Mungu-mtu – sasa anawatembelea watu wake. Pia katika Injili – Roho Mtakatifu alishuka juu yake Yesu kama hua. Katika kuandika huku kwake Yesu kukaa na wanyama pori – analinganisha maelezo ya Isa.  11,6 – mbwa mwitu atakaa na mwanakondoo, na chui atakaa na mtoto. Kama ilivyo katika Nuhu, yote yaonekana kuanza upya. Pamoja na yote tunayoweza kufanya katika kipindi hiki cha kwaresima, la msingi zaidi ni kule kuwa tayari kuanza upya. Jambo moja ni hakika – upendo wa Mungu uko mlangoni ili kutuimarisha na kutupa heri.

Tumsifu Yesu Kristo,

Padre Reginald Mrosso, C.PP.S.
All the contents on this site are copyrighted ©.