2018-02-14 08:09:00

DRC: Haki msingi za binadamu na utawala wa sheria viko mashakani!


Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya, Comece, inaonesha mshikamano mkubwa katika kuunga mkono juhudi za Baraza la Maaskofu, Kamati Maalum ya Waamini Walei, DRC, “Comitè Laic de Coordination, CLC, na Jumuiya za Kijamii nchini DRC, katika kutafuta njia za amani ili kuhakikisha taratibu za kukabidhi madaraka ya Rais wa DRC kwa njia ya demokrasia zinafanikisha. Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya inatoa mwaliko kwa wana harakati wote na kila mwenye nafasi kutazama kwa ukaribu wa pekee matokeo ya kijamii na uvunjwaji wa haki msingi za binadamu, kwa watu wa Jamhuri ya watu wa Congo, wanaohangaika kupata serikali ya kidemokrasia yenye kujali na kuheshimu uhuru wa kuongea na utu wa binadamu.

Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya, Comece, inatia shime Jumuiya ya Umoja wa Ulaya kufuatilia kwa makini na ukaribu mkubwa hali tete iliyopo nchini DRC, kwa kuonesha wazi baadhi ya matukio ya kusikitisha nchini humo. Wiki chache zilizopita, watu wameuwawa kwa kushambuliwa na vikosi vya usalama vya DRC, makanisa yameshambuliwa, wakleri na watawa wametiwa chini ya ulinzi kwa sababu tu wamevalia njuga utume wa Kanisa wa kutafuta na kutetea haki na amani. Tukio la hivi karibuni ambalo bado limeacha vidonda na maumivu makubwa kwa wapenda amani na watetea haki kokote duniani, ni lile la terehe 21 Januari 2018, ambapo raia wa nchi hiyo wakiwa katika maandamano ya amani kudai uchaguzi kufanyika kadiri ya Katiba, walishambuliwa na vikosi vya usalama na kusababisha vifo vya watu 6 na mamia kuumizwa vibaya.

Wito wa Tume ya Mabaraza ya Maaskofu Jumuiya ya Ulaya, Comece, unakuja siku chache baada ya Bunge la Jumuiya ya Ulaya kugusia uvunjwaji wa haki nchini DRC, na kuhimiza wahusika kuzingatia kile ambacho Baba Mtakatifu Francisko amekuwa akisisitiza sana, juu ya kuepuka kila aina ya ghasia, unyanyasaji na kinzani zinazopelekea watu wengi wanyonge kupoteza maisha au kuumizwa vibaya. Kumbe ni muhimu kuzingatia Makubaliano ya Saint-Sylvester.

Makubaliano ya Saint-Sylvester ni makubaliano yaliyofikiwa kati ya Serikali ya Rais Kabila na vyama vya upinzani, mnamo tarehe 31 Disemba 2016. Makubaliano haya yalifanikishwa kwa usuluhishi wa Baraza la Maaskofu nchini DRC, ambapo ilikubaliwa kwamba: iundwe serikali Mseto ya mpito ambayo ingeandaa uchaguzi mkuu kabla ya mwisho wa mwaka 2017, yaani mwaka mmoja baada ya Rais Joseph Kabila kuwa amemaliza muda wake wa uongozi ambayo ilikuwa ni tarehe 20 Disemba 2016; pili ilikuwa kwamba Rais Kabila asigombee tena nafasi ya urais kwani alikwishaitumikia Ofisi hiyo kwa vipindi viwili, vinginevyo itakuwa uvunjifu wa katiba; tatu ilikuwa ni kuachiliwa kwa wafungwa wa kisiasa; na nne ilkuwa ni uhuru wa vyombo vya habari na uhuru wa kujieleza.

Haya yote hayakuzingatiwa na serikali ya Rais Kabila, sababu ile serikali ya mseto ya kujumuisha vyama vyote vya upinzani ili kuandaa uchaguzi mkuu haikuundwa; uchaguzi sasa umepangwa kuwa ni tarehe 23 Disemba 2018 badala ya mwaka uliopita; Rais Kabila bado anaonekana kunuia kugombea tena urais kinyume cha Katiba, ingawa amekuwa akikana hilo; halafu vyombo vya habari na raia kwa ujumla wananyimwa uhuru wa kujieleza na zaidi sana wanashambuliwa vìbaya na utu wao kukanyagwa. Mfano wazi ni jinsi ambapo Kamati ya Waamini Walei nchini DRC, “Comitè Laic de Coordination, CLC, walipoandaa maandamano ya amani katika miji mbali mbali ya nchi ya Congo mnamo tarehe 31 Disemba 2017 na tarehe 21 Januari 2018; maandamano yaliyojaa umwagaji wa damu kwa kushambuliwa na vikosi vya usalama vya serikali ya Rais Kabila.

Kamati hiyo maalum ya Waamini Walei nchini DRC imesema kwamba, kwa sasa haitaandaa maandamano mengine hivi karibuni ili kupata muda wa kuchukua miili ya marehemu ambao baadhi bado imeshikiliwa na vyombo vya usalama, na pia kupata muda wa kutosha kuwahudumia majeruhi wengi wa matukio ya uvunjwaji haki hivi karibuni. Hata hivyo, Kamati hiyo imesisitiza kwamba, maandamano bado yapo pale pale mpaka kieleweke. Hapa ndo utaona jinsi gani bana ba Congoo balivyopania kumnyenyekesa Kabila, kwa imani kwamba Panya hawezi kumkula nyau.

Kwa kuonesha nafasi kubwa ya Kanisa Katoliki nchini DRC, Vyama na Jumuiya za Kijamii vimejumuika na kutafuta mtu atakayesaidia kuhakikisha usalama na amani nchini humo hasa baada ya kipindi cha uchaguzi, na wa kwanza katika orodha hiyo ya watu 12, ni Kardinali Laurent Monsengwo Pasinya, Askofu mkuu wa Kinshasa. Kufuatia hali hiyo tete nchini DRC na ile ya Sudani ya Kusini, Baba Mtakatifu Francisko, baada ya Sala ya Malaika wa Bwana siku ya Jumapili tarehe 4 Februari 2018, aliwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema, na kutangaza kuitenga siku ya Ijumaa tarehe 23 Februari 2018, katika kipindi cha Kwaresima, kuwa ni siku ya kufunga na kuombea amani duniani, na kwa namna ya pekee nchi za DRC na Sudani ya kusini.

Na Padre Celestine Nyanda

Vatican News!








All the contents on this site are copyrighted ©.