2018-02-14 06:55:00

Baba Mtakatifu Francisko atoa tiba muafaka kwa magonjwa ya kiroho


Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kipindi cha Kwaresima ni wakati muafaka wa kujiandaa ili kuadhimisha Pasaka ya Bwana, muda wa neema na kisakramenti cha wongofu wa ndani kinachotangaza na kutekeleza uwezekano wa kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa moyo na maisha yote! “Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa” (Rej. Mt. 24:12) ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa mwaka 2018. Katika ujumbe huu, Baba Mtakatifu anazungumzia kuhusu manabii wa uongo, moyo uliopooza kwa ubaridi; umuhimu wa sala, matendo ya huruma na kufunga ili kuwasha moto wa Pasaka kwa kuabudu Ekaristi Takatifu na kujipatanisha na Mungu na jirani kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho!

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kauli mbiu “Na kwa sababu ya kuongezeka kwa maasi, upendo wa wengi utapoa” ilitolewa na Kristo Yesu kwenye mjini Yerusalemu, kwenye Mlima wa Mizeituni, huko ambako Yesu aliteswa na kabla ya mateso yake, aliwafunulia wafuasi wake mwanzo wa taabu na mateso ambayo jumuiya ya waamini zingeweza kukumbana nazo na katika mazingira ya taabu na magumu, wangeweza pia kujitokeza manabii wa uongo watakaowadanganya wengi ili kuzima ndani ya mioyo ya watu upendo ambao ni kiini cha Injili.

Baba Mtakatifu baada ya kuchambua hali zote hizi zinazo sababisha upendo wa wengi kupoa, anasema, Kanisa: Mama na Mwalimu kwa kufuata tiba muafaka, ambayo wakati mwingine ni chungu kama “dawa ya mchunguti”, lakini anapenda ukweli, anawapatia watoto wake dawa ya kutumia wakati wa Kipindi cha Kwaresima yaani: Sala, Matendo ya huruma na Kufunga. Kwa kutoa nafasi ya pekee kwa maisha ya sala wakati wa Kwaresima, moyo wa binadamu upata nafasi ya kugundua siri za uongo na mambo madanganyifu, ili hatimaye, kutafuta faraja ya Mungu, ambaye ni Baba yao, anayependa kuwakirimia maisha!

Matendo ya huruma humsaidia mwamini kuondokana na tabia ya uchoyo na ubinafsi ili kugundua uwepo wa jirani ambaye anapaswa kushirikishwa matendo haya ya huruma ambayo, Baba Mtakatifu anasema, yanapaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya Wakristo, kama ilivyokuwa kwa Wakristo wa Kanisa la mwanzo. Huu ndio ushauri ambao Baba Mtakatifu anataka kuutoa kwa Wakristo wote wakati huu, ili kweli waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma kwa jirani zao kama ilivyokuwa kwa Jumuiya ya Wakristo wa Yerusalemu. Mahusiano na mafungamano ya kila siku kijamii yafumbatwe kwa mfano huu. Matendo ya huruma  kwa wakati huu ni njia muafaka ya kumwilisha upendo wa Mungu kwa waja wake na kwamba, Mwenyezi Mungu anapenda kuwatumia waamini kama vyombo vya msaada; msaada ambao utawarudia tena kwa wakati muafaka, kwani Mwenyezi Mungu ndiye chemchemi ya ukarimu.

Baba Mtakatifu Francisko mwishoni mwa ujumbe wake wa Kwaresima kwa mwaka 2018,  anazungumzia kuhusu kufunga, nguvu inayonyong’onyeza ghasia na kumpatia mwamini nafasi ya kukua na kukomaa katika utu wema. Ni fursa ya kukamilisha kile kinachopungua katika mahitaji msingi ya jirani zake! Waamini wawe na ujasiri wa kutambua na kuonja magumu ya watu wanaoteseka kwa baa la njaa, ili waweze kuguswa na ile kiu ya njaa ya wema inayotulizwa na maisha ya Mwenyezi Mungu. Kufunga kunawaamsha waamini na kuwafanya kuwa makini zaidi kwa Mungu na jirani; inaongeza ari ya kutaka kutekeleza mapenzi ya Mungu kama njia pekee ya kuzima njaa ya maisha ya binadamu!

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wazo hili litaweza kuwafikia pia waamini wa dini mbali mbali pamoja na watu wenye mapenzi mema; watu ambao wako tayari kumsikiliza Mwenyezi Mungu, ili waweze kuungana na waamini wenzao kufutilia mbali matendo yanayopooza upendo moyoni mwa mwanadamu, ili kumlilia Mwenyezi Mungu, hatimaye, waweze kufunga na kujinyima, ili sadaka yao waweze kuwapatia ndugu zao wenye mahitaji makubwa zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Vatican News!

 
All the contents on this site are copyrighted ©.